Jifunze namna ya kutafuta Masoko kwa biashara yako

Mpango na mkakati wa masoko

Mpango wako wa masoko ni muhimu kwa ajili ya mpango mzima wa biashara yako. Mabenki na wakopeshaji wengine watataka kufahamu ni namna gani umejipanga kuzalisha fedha. Ukianzisha, mpango wa shughuli za masoko utakusaidia sana kujua mambo yafuatayo:

 • Kutathmini mahitaji ya wateja na kubuni bidhaa zinazowafaa
 • Kufikisha ujumbe kuhusu sifa za bidhaa au huduma zako kwa wateja wako
 • Kuandaa mfumo wa usambazaji wa bidhaa kuwafikishia wateja
 • Kuchagua namna bora ya kuvutia wateja
 • Kuchagua njia zinazofaa za kutangaza biashara

Kabla ya kutengeneza mpango wa masoko kwa bidhaa au huduma yako unapaswa kutafiti soko la bidhaa/ huduma yako. Tumia matokeo ya utafiti wako kama ushahidi katika shughuli zako za kila siku.

Utafiti wa masoko

Utafiti wa masoko ni mchakato wa kukusanya taarifa ambao utakuwezesha kufahamu namna ambavyo wateja unaotarajia kuwauzia bidhaa/ huduma watachukulia biashara au huduma yako.

Mfanyabiashara yeyote hufanya utafiti huu, kwa kujua (kupanga) au kutokujua. Kwa mfano, unapozungumza na wateja kuhusu biashara yako, au unapotizama bei za washindani wako tayari unafanya utafiti wa masoko. Kuufanya utafiti huu kuwa rasmi kunaweza kukupa taarifa zenye thamani kubwa kuhusu bidhaa na huduma zako, pamoja na wateja na soko unalohudumia.

Namna ya kufanya utafiti wa masoko

Ni muhimu kwanza kuweka malengo yaliyo bayana kwa ajili ya shughuli ya utafiti unayoiendea. Unapaswa kuwa na uhakika kuhusu jambo gani unahitaji kufahamu na kwa nini.

Ukishajiwekea malengo, ni muhimu kutengeneza mkakati na kuchagua mbinu za kukusanya takwimu. Aina kuu mbili za utafiti unazoweza kutumia ni utafiti wa awali na utafiti unaotegemea tafiti zingine

Utafiti wa awali

Katika utafiti wa awali unakusanya taarifa za awali ama kwa ajili yako au kwa kwa niaba ya taasisi ya kitafiti ili kujibu maswali ya kitafiti au kufikia malengo ya kitafiti. Taarifa hizi hukusanywa kwa njia ya madodoso, kufanya uchunguzi kwa kuona, ama kufanya majaribio.

Utafiti wa awali unaweza kujibu maswali yafuatayo kwa mfano:

 • Wateja wetu ni kina nani na tutawafikiaje?
 • Sehemu zinazofaa kuweka biashara
 • Mikakati ya kimasoko
 • Wateja wanahitaji bidhaa na huduma zipi?
 • Mambo gani yanaathiri maamuzi ya wateja wangu kununua? Je ni bei, huduma, urahisi, au jina/ chapa/ utambulisho n.k.?.
 • Niweke bei gani kwa ajili ya bidhaa/ huduma zangu? Matarajio ya wateja?
 • Washindani wangu ni kina nani? Wanafanyaje biashara zao? Wana nguvu gani na madhaifu gani?

Baadhi ya hasara za utafiti wa awali ni kuwa unaweza kugharimu muda mrefu na fedha nyingi, hasa pale inapobidi kutumia watu wengine kuufanya, na matokeo yake hayapatikani haraka.

Faida za utafiti wa aina hii ni kuwa unaweza kuufanya kwa kulenga makundi mahsusi (kwa mfano wateja wako, au eneo linaloizunguka biashara yako) na unaweza kutengeneza dodoso lako kujibu maswali mahsusi. Pamoja na kupunguza gharama (fedha), kufanya utafiti kwa kushiriki mwenyewe moja kwa moja kutakuwezesha kupata ufahamu mzuri wa soko la biashara yako..

Madodoso ndio namna maarufu kuliko zote za kukusanya taarifa za awali. Yanaweza yakafanyiwa kazi kupitia:

 • Barua za moja kwa moja kwa walengwa, ambapo walengwa wanapatiwa madodoso na kuyajibu kisha kurudisha kwa njia hiyo hiyo. Ufanisi wa njia hii una shaka, na unahitaji ufuatiliaji na kukumbushia
 • Utafiti kwa njia ya simu – huu una gharama ndogo ila wakati mwingine inaweza kuwa ngumu kuwafikia wateja. Pia watu wengine hawapendi usumbufu wa simu
 • Utafiti kwa njia ya tovuti. Huu unawezesha kuwashiriki kwa kujaza dodoso kwa wakati wao kupitia tovuti. Gharama yake ni ndogo
 • Kutumia usaili wa mtu mmoja mmoja au vikundi. Huu unawezesha kuuliza maswali ya ziada au kubadilisha uelekeo wa utafiti kwa urahisi pale inapohitajika

Unapotengeneza dodoso kwa ajili ya utafiti, hakikisha:

 • Linakuwa fupi na rahisi kwa kadri iwezekanavyo
 • Linavutia na linasomeka kiurahisi
 • Anza na maswali ya jumla kuelekea kwenye maswali mahsusi
 • Maswali yawe mafupi na yanayoeleweka kirahisi
 • Usiweke maswali yanayotoa muelekeo wa jibu, au yenye maneno tata, au magumu sana kujibu
 • Iwapo utatumia majibu yanayopimwa kwa namba au viwango vingine, viwe vipimo vinavyoeleweka bila utata
 • Lijaribu dodoso lako kung’amua ikiwa lina matatizo yoyote kabla ya kulitumia

Vyanzo vya kimtandao/ tovuti mbalimbali vinaweza kukupatia mfano wa dodoso na kubadilisha maswali kuendana na matakwa yako, ziko pia kampuni zinazowezesha kutengeneza na kufanya utafiti kwa njia ya mtandao.

Taarifa nzuri kuhusu wateja wako inaweza kupatikana bila kuwahusisha wateja wenyewe moja kwa moja. Kuwahoji wafanyakazi wako kunaweza kukupa majibu mazuri maana wao wanakutana na wateja kila siku na wanaweza kukupatia taarifa kuhusu:

 • Sifa za wateja (umri, jinsia, n.k.)
 • Bidhaa na huduma zinazohitajika na wateja
 • Kuridhika kwao na kiwango cha bei na ubora wa bidhaa
 • Maoni yao kuhusu washindani wako

Utafiti unaotegemea tafiti zingine

Utafiti huu unatumia taarifa zilizopo tayari kama rekodi za kampuni, tafiti zilizofanyika awali na hata vitabu na machapisho mengine na kutumia taarifa hizo kujibu maswali yanayolengwa. Utafiti huu unachukua muda mfupi kuliko utafiti wa awali na unaweza pia kuwa na gharama nafuu.

Pamoja na kuwa utafiti huu haulengi makundi mahsusi, unaweza kuleta taarifa yenye thamani kubwa na kujibu baadhi ya maswali ambayo yasingejibika kirahisi na utafiti wa awali, mfano mzuri ni kuwa unaweza kupata majibu ya maswali ambayo wateja wasingeyajibu kwa uhuru (mfano umri au kiwango cha kipato).

Yafuatayo ni baadhi ya maswali ambayo utafiti huu unaweza ukayakabili:

 • Biashara yangu inajiendesha katika hali gani za kiuchumi kwa sasa? Je hali hizo zinabadilika? (hali za kikanda, kitaifa, kimataifa)
 • Mabadiliko gani yanaathiri sekta ninayofanyia biashara yangu? Wateja wanataka nini?
 • Mabadiliko ya kiteknolojia
 • Bei za bidhaa na huduma
 • Yapo mahitaji ya bidhaa / huduma zangu Katika soko la kimataifa ambayo yataniwezesha kukuza biashara yangu?
 • Zipi zifa za kitakwimu za wateja wangu na wanaishi wapi? Idadi yao, umri, viwango vya mapato, n.k.
 • Hali ya soko la ajira ikoje?
 • Watu wangapi wana ujuzi ninaouhitaji?
 • Nitarajie kuwalipa kiwango gani waajiriwa wangu?

Kumbukumbu zilizopo za kampuni kama ankara, risiti, malalamiko rasmi ya wateja ni vyanzo muhimu vinavyoweza kutumika katika utafiti huu. Mara nyingi kumbukumbu hizi hutoa mwanga katika mambo ambayo hata utafiti wa awali huwa unayatafuta, hivyo uchambuzi wa kumbukumbu za kampuni unapaswa kufanyika kabla ya kufikiri kukusanya taarifa za awali kwa wateja. Mifano ya kutumia takwimu zilizopo za kampuni kwa ajili ya utafiti wa masoko ni kama::

 • Kutizama risiti za mauzo kuona mwenendo wa mauzo/ mahitaji ya bidhaa au huduma fulani
 • Kulinganisha risiti za mauzo na anwani za wateja ili kutathmini namna ambavyo matangazo ya biashara yamefanikiwa
 • Kuchambua malalamiko ili kufahamu maeneo ya kuboresha katika huduma kwa wateja, bei au bidhaa/ huduma zenyewe

Chanzo kingine cha taarifa ni taarifa za kitakwimu kutoka taasisi rasmi za takwimu na taasisi zingine. Takwimu hizi zinaweza kuingia katika taarifa za kichambuzi na kutoa picha za hali ya soko.

Kufahamu ni taarifa zipi za kitafiti zinaweza kusaidia biashara yako inaweza kuwa kazi ngumu, na baadhi ya takwimu zinauzwa kwa gharama kubwa. Hata hivyo, ziko pia takwimu zenye ubora na taarifa za kichambuzi ambazo zinapatikana, pamoja na mwongozo ambao unaweza kukusaidia kuchambua taarifa zilizopo.

Taarifa za idadi ya watu

Pata taarifa kuhusu idadi ya watu na tabia zake kama maeneo, umri, kipato, kiwango cha elimu, n.k.

Taarifa za kazi na ajira

Pata takwimu na uchambuzi kuhusu nguvukazi, ajira na vipato kutoka chanzo rasmi serikalini na vyanzo vya kimataifa

Hali ya uchumi

Pata taarifa za viashiria vya kiuchumi ambavyo vinaathiri utendaji wa sekta mbalimbali kiuchumi

Taarifa za kisekta

Pata taarifa ambazo zitakuwezesha kuelewa sekta yako na soma mwenendo wa kisekta ambao unaweza kuathiri biashara yako.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *