PesaKuna gharama kuanzisha biashara yoyote. Kwa hiyo, si budi kutambua namna utakavyogharimia biashara. Je, una njia za kupata fedha za kuanzishia biashara au utahitaji kukopa fedha? Kama una panga kuanzisha biashara yako mpya kama kazi ya muda wote ni busara kusubiri hadi angalau una kiasi cha fedha za kuanzishia biashara bila kutegemea mkopo.

Nchini Tanzania, kuanzisha biashara kuna ugumu kiasi ikilinganishwa na nchi nyingine. Mtu hawezi pata mkopo kutoka kwenye taasisi za fedha kama hana biashara inayojiendesha angalau kwa miezi sita. Kwa hiyo, kabla ya kuanzisha biashara hakikisha umepata fedha za kutosha kuendeshea biashara walau kwa mwaka mmoja.

Kabla ya kufikiria namna ya kupata fedha, mtu lazima awe na mapendekezo yaliyo dhahiri na bayana katika kueleza biashara kwa undani. Mtu anaweza kutumia mfano wa mpango wa biashara ulioambatanishwa

Kupata Fedha

Katika kutafuta fedha kwa ajili ya biashara, kuna misingi kadhaa mtu anaweza kutumia. Ifuatayo ni misingi hiyo:

1. Akiba ya fedha

Katika hili, mtu anaendelea kuweka akiba ya fedha ili kuwa na kiwango cha mtaji unaohitajika kuanzishia biashara husika. Baadhi ya njia za msingi zinazotumiwa na watu ni kupitia matumizi ya akaunti maalumu kama vile akaunti kikomo na akaunti maalumu. Karibu benki zote za biashara na baadhi ya taasisi za fedha hutoa huduma ya akaunti kikomo.

2. Ubia

Njia nyingine nzuri ya kuongeza fedha kwa ajili ya biashara ni kuanzisha ubia. Hapa mtu huangalia watu na biashara ambazo zinaweza gharimia biashara tarajiwa na kuwahusisha kama wabia muhimu. Hata hivyo, ili hii iwezekane, unatakiwa mkataba mzuri na makubaliano ya ubia huo yanatakiwa yaonyeshe namna ambayo kila mtu atakayehusika na biashara hiyo atakavyonufaika.

3. Familia na Marafiki

Kutumia wanafamilia na marafiki ni njia nzuri mbadala ya kukuza mtaji wa biashara. Hapa mtu anayependa kuanzisha biashara anaweza kutafuta msaada wa fedha kutoka kwa wote wanafamilia na marafiki ambao wanaweza kusaidia jitihada zake.

4. Udhamini wa Fedha

Wajasiriamali Wadogo, wa Kawaida na wa Kati wanaweza kupata mikopo kwa ajili ya biashara zao kwa kutumia udhamini wa fedha. Nchini Tanzania, serikali imeunda mpango wa udhamini kwa Wajasiriamali Wadogo, wa Kawaida na wa Kati katika taasisi za fedha ili kuwezesha ukopeshwaji wa waagiza bidhaa nje wapate huduma kubwa na nzuri kutoka katika taasisi hizo.

Katika mpango huo, taasisi za fedha zinathibitishiwa kwamba endapo mfanyabiashara atakwepa kulipa deni, mpango utalipa sehemu ya hasara. Kwa hiyo, wajasiriamali tajwa ambao ni wazawa wanaojihusisha na uagizaji bidhaa nje ya nchi wanaweza kunufaika na mpango huo wa kupata fedha ili kupanua biashara zao.

Wajasiriamali wanaostahili

o Biashara iwe imesajiliwa na inamilikiwa na raia wa Tanzania

o Iwe ni miradi ya kibiashara yenye faida, ambapo ni msingi wa kuombea uwezeshwaji wa mkopo

o Kuwa tayari kutoa dhamana ya lazima pamoja na dhamana binafsi kwa matakwa ya kuruhusu dhamana ya mpango

o Awe ameomba uwezeshwaji wa mkopo kutoka katika taasisi ya fedha kuhusiana na miradi stahiki ambapo taasisi hiyo ya fedha imeomba dhamana kutoka katika mpango huo.

Vyanzo vya dhamana ya fedha kwa mikopo Tanzania

Benki Kuu ya Tanzania

Tel: +255-22-2233000-20

Benki ya Maendeleo ya Afrika (African Development Bank)

Tel: +255 (22) 2125281

+255 (22) 2125286

CRDB Bank

Tel: 022-2116714/2133067

 

5. Mikopo

Njia nyingine ya kupata fedha ni kupata mkopo kutoka kwa mabenki na taasisi ndogo za kifedha (Orodha imeambatanishwa ya mabenki na tasisi za kifedha zinazotoa mikopo kwa wajasiriamali tajwa). Kwa kawaida, nyingi ya tasisi hizi zina utaratibu maalumu kwa wajasiriamali tajwa na hasa viwango vilivyowekwa na mahitaji ya kupata mikopo kwa ujumla.

Ili kuweza kupata fedha kutoka kwenye taasisi ndogo za fedha na mabenki, kuna matakwa kwa ujumla ambayo si budi mtu ayatekeleze. Yafuatayo ni matakwa hayo:

Lazima awe Mtanzania mwenye umri wa miaka 18 au zaidi

Lazima awe na leseni ya biashara (nakala halisi na nakala kivuli)

Lazima awe na taarifa ya fedha katika biashara yake

Lazima awe na Hati ya Kibali cha Kodi (nakala halisi na nakala kivuli)

Lazima awe na barua ya maombi ya mkopo aliyoandikiwa meneja wa tawi husika

Barua ya utambulisho wa makazi kutoka kwa kiongozi wa serikali za mitaa na barua ya mdhamini

Nakala ya utambulisho binafsi/kitambulisho cha kupiga kura/pasi ya kusafiria na utambulisho wa mdhamini

Picha za ukubwa wa pasi na mdhamini (nakala tano kwa kila mmoja) zenye usuli wa buluu

Dhamana kama ilivyoainishwa na taasisi ya fedha husika, kwa kawaida vinavyotumika ni mali isiyohamishika kama vile nyumba, shamba na vitu vingine kama gari na mali zenye thamani kama itakavyoainishwa na chanzo cha fedha

Kabla ya maombi ya mkopo, kuna masuala kadhaa ambayo lazima yazingatiwe na mwombaji. Yafuatayo yafikiriwe kabla ya kutafuta mkopo:

 1. Aina ya biashara

Kabla ya kutafuta mkopo, mtu lazima ajue aina ya biashara anayojihusisha. Hii ni muhimu kwa sababu itasaidia kusaidia tathmini ya mapato ya biashara kwa jumla na uwezekano wa kulipa mkopo.

 1. Kiasi halisi kinachohitajika

Katika hili, mtu anahitaji kujua kiasi halisi anachohitaji kuanzishia biashara. Ili kujua kiwango kinachotakiwa, mtu anahitaji kujua matakwa yote ya kuanzisha biashara husika. Kwa mfano, mahitaji yanayohitajika ni kama yafuatayo:

 1. Sehemu – nyumba/chumba ambapo mtu anahitaji kuwekeza biashara yake

 2. Vifaa/mitambo inayohitajika

 3. Kazi inayohitajika na gharama zinazoambatana nayo

 4. Gharama za usajili na leseni kwa ujumla

 5. Bima

 1. Riba iliyopangwa na mpango wa marejesho

Kujua riba inayotakiwa ni lazima kwa sababu inasaidia kuandaa marejesho ya mkopo. Kwa kujua riba inayotakiwa kulipa itasaidia kujua jumla ya fedha itakayotakiwa kulipwa na hivyo kuwezesha mpango rahisi wa marejesho.

 1. Mapato ya biashara

Haya nayo yanasaidia kuandaa mpango wa marejesho ya mkopo. Kujua mapato ya biashara kunatoa fursa ya kujua kiwango ambacho mtu anaweza kulipa kwa mpango wa wiki au kwa mwezi. Kuwa na wazo ambalo biashara yako itazalisha kutasaidia kujua kama kutakuwa na mapato/faida inayotosha kuweza kulipa mkopo au mtu atatafuta chanzo cha fedha cha ziada ili kulipa mkopo utakaochukuliwa.

 1. Dhamana inayotakiwa katika mkopo

Mwisho mtu anahitaji kujua dhamana inayotakiwa katika mkopo husika. Hii ni lazima kwa sababu kushindwa kulipa mkopo kutapelekea kuuzwa au kutaifisha/kufilisi mali iliyowekwa kama dhamana. Kulingana na hilo, mtu anahitaji kujua mali halisi zitakazohesabiwa kama dhamana pia anatakiwa kujua madhara atakayoyapata endapo dhamana hiyo itauzwa.

Zifuatazo ni changamoto zinazowakabili wajasiriamlai tajwa katika kupata mikopo:

 • Wajasiriamali hao kuwasilisha nyaraka za uongo na taarifa za uongo

 • Matumizi mabaya ya mikopo iliyotolewa

 • Uchelewaji kulipa mkopo

 • Viwango vikubwa vya riba

 • Kushindwa kutoa dhamana

 • Benki nyingi haziendeshi dirisha kuwakopesha wajasriamali tajwa

 • Mgawanyo usio sawa kwa taasisi za kifedha, yaani, nyingi ziko mijini na kando kando mwa miji

Mambo ya kufanya na yasiyofaa wakati wa kutafuta mkopo

Mambo ya kufanya wakati wa kutafuta mkopo

 • Lazima uwe na wazo la biashara

 • Mpango mzuri ulioandaliwa mahsusi kwa kuonesha jinsi mkopo utakavyotumika

 • Kuwe na mpango sahihi wa marejesho ya huo mkopo

 • Wekeza mkopo utakaopata kwa biashara iliyolengwa

 • Ongeza muda wa kulipa mkopo, kwa mfano, kama waweza lipa ndani ya miezi sita omba kulipa ndani ya miezi 12 ili kuwa katika upande salama.

Mambo yasiyofaa wakati wa kutafuta mkopo

 • Usitumie kwa matumizi yako binafsi nje ya biashara iliyodhamiriwa

 • Wekeza mkopo katika biashara tofauti na iliyokusudiwa

 • Kutokuwa na mpango wa kulipa marejesho

 • Panga kutorosha bila kulipa mkopo

 • Kutoa taarifa za uongo

Zifuatazo ni huduma zingine zinazoweza kutolewa na taasisi za kibenki na fedha:

 • Kufungua akaunti (mabenki)

 • Kuweka na kutoa fedha (mabenki)

 • Huduma ya Intaneti an Benki kwa simu (Mabenki)

 • Mafunzo (wote)

 • Nyingizeo

 • Kadi za ATM

Mambo ya kuzingatia kabla ya kupata mkopo mdogo

1. Tambua unachohitaji

Kama huna uhakika ni kiasi gani kampuni yako inahitaji ili kuanzisha au kupanua biashara, kutana na mshauri au mhasibu kabla ya kwenda kwa wakopeshaji. Jiandae kuwasilisha nyaraka dhidi ya maombi yako na jibu maswali kuhusu uwezo wako kifedha, aina ya biashara na mipango ya baadaye. Pia uwe tayari kuongea haswa kuhusu utakavyotumia mkopo. Kwa mfano, unaweza onesha jinsi fedha zitakavyotumika kununa vifaa, kuanzisha eneo jipya la biashara au kulipa wafanyakazi wa ziada.

2. Tafuta Mtaalamu

Kama wahitaji msaada wa kupata mkopo sahihi kwa biashara yako au mwongozo wa kukusaidia katika mchakato wa maombi waweza tafuta msaada toka vituo vidogo vya Uendelezaji Biashara mfano wa vituo hivyo ni vituo vya Biashara vya wanawake na taasisi za ushauri wa biashara ndogo vyaweza saidia katika mchakato.

3. Boresha mpango wako wa biashara

Biashara yoyote lazima iwe na mpango wake. Kabla ya kuomba mkopo kwa ajili ya biashara hakikisha una mpamgo wa biashara unaojieleza kuhusu kampuni yako kwa ukweli na usahihi. Hakikisha umeandikwa kwa ufasaha kiasi cha kuwavutia wawekezaji. Kagua masuala yafuatayo:

 • Jinsi gani umeonesha kwamba unaelewa namna ya kuuza bidhaa au huduma yako na kuweza kufaidika kwa kufanya hivyo?

 • Dibaji yako ina nguvu/uwezo kiasi gani?

 • Umejiamini vipi katika tathmini ya soko na ushindani?

4. Weka karatasi zako vizuri

Maombi ya viwango yanahitaji nyaraka mahsusi na idadi mahsusi. Tenga mda wa kutosha kupitia na kuweka taarifa zako sawasawa kabla ya kuendelea na mchakato wa kukopa. Ni vizuri kuandaa mkutano na mshauri wa fedha ili kufanikisha azma hiyo.

Zifuatazo ni baadhi ya nyaraka utakazohitaji:

Nyaraka za kampuni kama vile nyaraka za kuingizwa kampuni (Article of incoporation), kufanya biashara, leseni ya biashara na kadhalika

Orodha ya mali za biashara na mali binafsi inayoweza kutumika kama dhamana

Majina na anwani za walau wadhamini waaminifu watatu

Taarifa ya fedha kwa miaka mitatu ya fedha (kama ipo)

Nyaraka za marejesho ya kodi kwa miaka mitatu iliyopita

5. Jiandae kuonesha jinsi utakavyotumia fedha za mkopo

Waweza ambatanisha ripoti ya taarifa ya fedha (Financial statement) inayoonyesha matarajio ya mzunguko wa fedha kwa miaka mitatu hadi mitano ijayo. Katika Ankara hiyo, onesha jinsi utakavyotekeleza manunuzi na jinsi unavyotarajia kulipa mkopo.

Kuwa sahihi (be specific). Onesha jinsi utakavyotumia fedha kufungua masoko mapya au matumizi ya biashara mahsusi yatakayotoa majibu chanya.

Kama unatafuta fedha kwa ajili ya mkopo, utahitaji kusisitiza namna utakavyolipa mkopo. Kwa upande mwingine, wawekezaji wa usawa (Equity investors) wanataka kuona uwezo wa nguvu ya kulipa mkopo.

6. Kagua mkopo

Benki nyingi zinatumia vipimo vya mikopo (credit scoring) ili kuamua kama unahitimu kwa mkopo au la. Kwa kawaida, kwa mikopo ya kibiashara, vipimo hivyo hutumia vigezo vya historia ya ukopaji ili kuamua kama uko katika hatari au la. Hata kama benki yako haiegemei katika njia hii,itakagua katika historia ya kumbukumbu zako ili kuamua ukopaji wako wa baadaye. Kuna uwezekano mzuri waweza ulizwa udhamini wako binafsi katika mkopo. Kwa hiyo, historia yako ya mkopo ni ya maana.

7. Weka maombi yako nadhifu

Taarifa za fedha zako zaweza kuwa vigezo vya maana kukusaidia kupata mkopo lakini unadhifu unahesabu pia. Usisahau vitu vidogo vyaweza wapendezesha watoa fedha na kuimarisha taswira ya kitaalamu. Weka fomu zako nadhifu na rahisi kusomeka. Vaa kinadhifu, mavazi yanayofaa katika mikutano ya kibiashara. Onesha kadri unavyoweza kuonesha uaminifu na onesha una uwezo mkubwa.

8. Uwe Mtulivu/mvumilivu

Kupata fedha, haijalishi kiwango cha biashara yako, ni mchakato una gharimu muda na kuchosha. Wamiliki wengi wa biashara ndogo ndogo hawajali itachukua muda gani kupata fedha wanazohitaji na si ajabu kuishiwa fedha ya uendeshaji biashara katika mchakato huo. Hakikisha unazingatia muda katika majukumu yote utakayotekeleza, kuanzia kwenye urekebishaji wa mpango wa biashara hadi kutohoa orodha ya mabenki, taasisi za kukopesha fedha au wawekezaji wa nje.

Bima kwa Wajasiriamali Wadogo na Wa kati

Bima ni mabadilishano kama fidia kati ya mmiliki wa biashara na kampuni ya bima katika kiwango maalumu kwa muhula/kipindi maalumu. Mara baada ya kusajili biashara, hasa kabla ya kuanza biashara, shurti mmiliki afikirie masuala ya bima. Kulipia bima kwa biashara yako ni kuzuia biashara yako kuingia hasara endapo tatizo lolote lisilotarajiwa kama vile moto, wizi au majanga ya asili yatatokea. Biashara inapokatiwa bima, wakala wa bima atafidia hasara itakayotokea.

1. Faida

 • Usalama dhidi ya matukio yasiyotarajiwa kama vile wizi na moto

Mfanyabiashara anaweza lipia bima biashara yake ili asidhurike na madhara kama vile wizi na moto. Kwa maana hiyo, mhusika hupata fidia yote baada ya kutokea tukio.

 • Njia rahisi za fidia ya hasara endapo bahati mbaya yaweza kutokea

Mtu anaweza lipia bima ya biashara yake ili asidhurike hasara ikitokea. Kama biashara imelipiwa bima, baadhi ya hasara zaweza kulipwa/kufidiwa na hivyo kuwezesha uwepo wa biashara.

 • Bima yatoa fursa katika huduma bila kulipia fedha halisi kwa wakati husika, kwa mfano, bima ya afya

Hii ni kwa ajili ya aina zingine za bima kama vile bima ya afya. Mtu hupata fursa kamili kwa ajili ya huduma za afya bila kulipa hata senti. Hapa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wanaweza kuwa na uhakika wa usalama kwa afya za familia zao wanapougua.

 • Huruhusu ukuaji wa biashara kwa urahisi bila kudhurika na changamoto

Katika hili, biashara inaweza kushamiri bila kuwa na wasi wasi kuhusu changamoto zisizotarajiwa zikitokea wakati biashara imelipiwa bima

2. Mambo ya kuzingatia wakati wa mahitaji ya bima kwa ajli ya biashara

 1. Aina ya bima ambazo mtu anaweza kujiunga

Kuna aina nyingi za bima, kwa mfano, bima ya moto, bima ya wizi na bima ya magari. Si budi mtu akajua mpango mahsusi kwa kujiunga na bima

 1. Uhalisi wa kampuni ya bima

Katika maeneo mengi, kuna mawakala wa bima bandia. Kwa hiyo, kabla mtu hajalipia huduma ya bima, si budi awe na ufahamu wa uhalisi wa kampuni ya bima. Mambo/masula ya mtu kuzingatia ni kukagua katika maeneno/masula yafuatayo:

 1. Nyaraka zilizothibitishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wakala wa Usajili wa Leseni(BRELA)

 2. Ofisi na maeneo halisi ya kampuni

 3. Nakala za risiti (hata hivyo, hizi zisiwe uthibitisho pekee kwani wakati mwingine zinaweza kuwa za kughushi)

 4. Orodha ya makampuni nchini au orodha ya makampuni ya biashara nchini ili kuhakikisha kama kampuni inatambulika kisheria

 1. Kulinganisha makampuni kadhaa ya bima ili kubaini kampuni inayotoa huduma zinazofaa katika gharma ambazo waweza kuzimudu

Kutokana na kuwepo makampuni mengi yanayotia huduma za bima kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati, kabla ya kujiunga na mpango wa kampuni yo yote ya bima, mtu anapaswa kukagua gharama kwa kulinganisha na makampuni kadhaa ili kupata huduma itakayofaa

 1. Hakikisha kuwa una nyaraka muhumi

Kimsingi, nyaraka muhimu hutegemea namna ya mali/huduma ya bima mtu atakayojiunga nayo, kwa mfano,

 1. Nyaraka za usajili na leseni

 2. Hati ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN)

 3. Nyaraka halisi/zilizothibitishwa zinazoonesha umiliki na thamani ya mali/biashara

Angalizo: Nyaraka zinazotakiwa hutofautiana kutegemea na makampuni (Tafadhali angalia orodha ya makampuni iliyoambatanishwa)

 1. Lipia bima kwa vitu muhimu sana katika biashara

Ingawa si wazo jema kuacha kusajili baadhi ya vitu/mali, lakini mara nyingi mtu aanze kusajili vitu/mali muhimu zaidi katika biashara. Kwa mfano, kwa biashara ya vyakula, vitu vya kwanza kulipia bima ni jiko.

 1. Lipia bima dhidi ya majanga yanayoweza kutokea

Japokuwa si rahisi kutabiri kutokea kwa janga, lakini kutegmea na aina ya biashara na eneo biashara itakapofanyika, kuna majanga muhimu ambayo mtu anatakiwa kuambatana nayo. Kwa mfano katika biashara ya hoteli, moto, wizi na mali ni vitu vya lazima kujiunga katika mipango yake wakati mipango ya biashara ya usafirishaji inaweza kuhuisha mali, ajali na wizi.

3. Aina za msingi za bima kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati

 1. Wizi

Aina hii ya bima inaweza kuhusisha madhara dhidi ya kutokea kwa wizi wa mali za biashara

 1. Moto

Hii mtu anaweza kulipia bima ya nyumba na vifaa vyake dhidi ya moto

 1. Majanga ya asili

Hii inahusu kulipia biashara kutokana na madhara yanayotokana na majanga ya asili kama vile mafuriko dhidi ya biashara

 1. Mpango wa Bima ya Afya/Matibabu

Aina hii ya bima inaweza kuwa katika aina mbili zifuatazo:

 1. Aina ya kwanza ya bima ya afya ni kutoa huduma ya afya kwa watu. Katika aina hii ya bima, watu wanaweza kupata huduma za afya baada ya kujiunga na mpango wa bima ya afya.

 2. Aina ya pili ya bima ya afya ni kulipia madhara ya aina zote yanayoweza kutokana na ajali au kifo wakati wa kazi au katika mazingira ya kazi

 1. Bima ya mali

Katika aina hii ya bima mtu alipie bima ya mali. Kuna aina nyingi zinazoweza kulipiwa bima kama zifuatazo:

 • Mizigo ya bandari: Sera hii inahusisha kinga dhidi ya upotevu wa mizigo wakati inasafirishwa baharini (kwa meli), angani (kwa ndege) au ardhini (kwa barabara au reli).

 • Magari:Sheria inataka magari yote katika barabara za umma kuwa na bima au kinga dhidi ya dhima kwa kuumia kwa mwili na kwa abiria.

ANGALIZO: Biashara yo yote inayoendeshwa nchini kisheria yaweza lipiwa bima

 

4. Orodha ya Sheria Zinazoongoza Huduma za Bima

 1. Sheria ya Bima ya mwaka 2009

Sheria iliyoanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Bima Nchini (Tanzania Insurance Regulatory Authority). Chini ya Sheria hii, mamlaka imepewa nguvu ya kuongoza na kusimamia biashara ya bima na masuala yote yanayohusiana na bima Tanzania Bara na Zanzibar.Sheria inaipa mamlaka nguvu ya kusimamia na kuratibu shughuli zote za bima. Sheria inaainisha kanuni za maadili kwa ajili ya bima na taarifa zote muhimu za kuendesha biashara ya bima wakati ambapo mamlaka ya usajili wa biashara za bima amepewa Kamishna wa Bima au Naibu Kamishna wa Bima. Sheria inaelekeza kwamba yeyote atakayeanzisha biashara ya bimalazima awe mkazi wa Tanzania lakini kama ni kundi angalau theluthi moja ya wajumbe wa bodi wawe ni wakazi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sheria inaelekeza taratibu na nyaraka muhimu za kuanzisha biashara ya bima. Pia sheria inaelekeza haki ya bima ya tatu kama vile kuwa na bima dhidi ya dhima kama kufilisika pamoja na haki ya kupata taarifa kwa mwendesha biashara ya bima.

 1. Kanuni za Bima Ndogo za 2003

Kanuni hizi zinahusu wakala wa bima ndogo na mwekeza bima anayehusika na bima kwa ujumla kuhusu bima ndogo au bima ndogo ya maisha. Huduma chini ya kanuni hizi zinahusu banda, mifugo, vifaa vya uvuvi, mazao ya kilimo, zana za biashara ndogo au vifaa au ajali ya mtu binafsi au kundi, elimu, muda wa mkopo, maisha ya familia na bima ya mkataba wa mazishi.