JINSI YA KUSHUGHULIKIA MATWAKWA YA VIBALI (MAELEKEZO)

sheriaKutokana na mahitaji ya kisekta kwa biashara ndogo ndogo, wajasiriamali wanatakiwa kufuata matwakwa kadha wa kadha wakati wa kupata vibali, leseni au ruhusa ya aina fulani. Ili kuweza kupata vibali hivyo, kuna maelekezo ya kufuata. Maelekezo hayo ni kama yafuatayo:

Hatua ya kwanza: Tambua unachotaka kufanya

Hapa unatakiwa kujua ni kitu gani ambacho unakihitaji. Kwa mfano, kama unatakiwa kujua kama unataka kulipia leseni, kuomba kibali au kulipia tozo fulani. Hii itakurahisishia kufuatilia hatua zinazoendelea.

Hatua ya pili: Tambua taasisi zinazohusika na kitu unachotaka kufanya

Baada ya kujua unachotaka kufanya, kinachofuata ni kujua ni taasisi gani inahusika katika kutoa huduma hiyo. Hili ni la muhimu hasa katika kuondoa usumbufu wa kuzunguka maofisini bila kujua ni ofisi ipi hasa itatatua tatizo lako. (Kwa maelezo zaidi, angalia mahitaji kwa kila sekta)

Hatua ya Tatu: Andaa nyaraka zote zinzohitajika

Baada ya kujua ni taasisi gani inayohusika na unachotaka kufanya, kinachofuata ni kuandaa nyaraka zote zinazohitajika kwa ajili ya maombi yako. Mara nyingi ili uweze kupata leseni au kibali, kuna nyaraka zinazohitajika, kwa mfano, namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN) au nyaraka za usajili wa biashara. Hivyo basi kabla ya kwenda kwenye ofisi, ni lazima uhakikishe una nyaraka zote zinazohitajika kwa ajili ya kibali au leseni husika.

Hatua ya nne: Tambua tozo zinazoambatana na maombi yako

Mara nyingi ili uweze kupata vibali husika, kuna tozo ambazo huambatana na maombi yako. Ili uweze kufanikisha hili ni lazima uhakikishe kuwa unajua tozo zinazohitajika na kuhakikisha kuwa fedha kwa ajili ya malipo hayo zipo tayari.

Hatua ya tano: Anza mchakato wa maombi

Baada ya kuhakikisha kuwa hatua zote zimekamilika, kinachofuata ni kuanza mchakato wa maombi.