Zijue mbinu za kuanzisha biashara

Uchumi wa Tanzania umekuwa ukizalisha ajira chache kila siku. Hii imekuwa ikifanya vijana wengi wanaohitimu vyuoni kubaki wakizunguka na bahasha kila kona kusaka ajira.

Takwimu kutoka ofisi ya takwimu ya taifa zinaonyesha kuwa mwaka 2014 taifa lilizalisha nafasi za ajira 282,382 tu ukilinganisha na mahitaji ya zaidi ya wahitimu 400,000 wanaomaliza vyuo kila mwaka.

Hii inaonyesha dhahiri kuwa Tanzania kama nchi inahitaji kuweka nguvu za ziada katika kuhakikisha kuwa nafasi zaidi za ajira zinatengenezwa.

Pengine njia pekee inayoweza kutumiwa kupunguza tatizo hili au hata kulimaliza kabisa ni kupitia ajira binafsi (Ujasiriamali).

Pamoja na kuwa ujasiriamali unaweza kuwa suluhisho la ajira nchini, vijana wengi wameshindwa kabisa kufanya ujasiriamali kutokana na kukosa elimu sahihi. Kwa bahati mbaya sana mfumo wetu wa elimu haumsaidii sana muhitimu kupata stadi za ujasiriamali.

Katika vipaumbele vyake, Rais John Magufuli anasisitiza sana Tanzania ya viwanda, lakini hili litatokea tu kama vijana wa kitanzania watapatiwa elimu ya ujasiriamali.

Sehemu hii itakuwa ikiwapatia makala mbalimbali za ujasiriamali… tutajifunza jinsi ya kuanzisha biashara, jinsi ya kuendeleza biashara yako na namna ya kupata fedha.

Leo tutaanza kujifunza mambo ya msingi katika kuanzisha biashara.

Mambo ya Msingi katika kuanzisha biashara

Biashara yoyote huanza na wazo, ila wazo pekee halitoshi, linahitaji kufanyiwa kazi. Hapo ndipo watu wengi huweza kuanza kujisikia kuzidiwa. Si ajabu kuona mtu anakatishwa tamaa kwa kutizama msururu wa mambo yanayohitajika ili kuanzisha biashara, lakini pia kuanzisha biashara ni rahisi kuliko unavyodhani. Kama ilivyo katika lengo lolote kubwa, ukianza kwa kutengeneza malengo madogo madogo ya kutekeleza utaweza kufanya mambo yote muhimu katika kuanzisha biashara.

Jinsi ya Kuanzisha Biashara Ndogo

Kuanzisha na kuendesha biashara inahitaji msukumo, nia na kipaji. Inahitaji pia utafiti na mipango. Kama ilivyo kwenye mchezo wa drafti, mafanikio kwenye biashara ndogo huanza na maamuzi sahihi katika hatua za mwanzoni. Ikumbukwe pia hapa kuwa pamoja na kwamba makosa madogomadogo ya mwanzoni yanaweza yasiue biashara yako, inahitaji ujuzi, nidhamu, na bidii kuyasahihisha.

Ili kuboresha uwezekano wa kufanikiwa, unapaswa kutenga muda wa kujichunguza na kutathmini malengo yako kibiashara na malengo binafsi. Tumia taarifa hiyo kutengeneza kwa umakini mkubwa mpango wa biashara ambao utakuwezesha kufikia malengo yako.

Mchakato wa kuandaa mchanganuo wa biashara utakuchochea kufikiria hata baadhi ya mambo ambayo usingekumbuka kuyafikiria katika hali ya kawaida. Mchanganuo wako utakuwa zana muhimu sana unapopambana kutafuta fedha kwa ajili ya biashara yako. Mchanganuo huo pia unaweza kutumika kama kigezo cha kila mara kufuatilia/ kupima mafanikio ya biashara yako.

Yako mambo kadhaa yanayohitajika katika biashara yoyote.

Jambo la kwanza kabla ya kuanzisha biashara ni kuwa unatakiwa ujiulize sababu za wewe kutaka kuingia kwenye biashara. Sababu zilizozoeleka za kuanza biashara ni:

 • Unataka kujiongoza mwenyewe.
 • Unataka uhuru wa kifedha.
 • Unataka uhuru wa kutumia ubunifu wako.
 • Unataka kutumia kikamilifu ujuzi na ufahamu wako

Jambo la pili ni kuamua biashara ipi inakufaa? Ili kufahamu ni biashara ipi inakufaa, jiulize maswali yafuatayo:

 • Ninapenda kutumiaje muda wangu?
 • Nimejifunza au kusomea ujuzi gani?
 • Watu wengine wanazungumzia ubora wangu kwenye mambo gani?
 • Nina muda kiasi gani kuendesha biashara kwa ufanisi?
 • Katika mambo ninayopendelea yapo ambayo yanaweza yakawa fursa ya biashara?
 • Biashara yangu itahudumia sehemu/ kundi gani katika soko?
 • Je? Wazo langu linatekelezeka na litakidhi hitaji katika soko?
 • Ushindani nilionao ni upi? Nami nina uwezo gani katika ushindani?
 • Biashara yangu ina manufaa gani kuzidi zingine zilizopo?
 • Je? Naweza kutoa huduma zenye ubora zaidi?
 • Je? Naweza kutafuta soko kwa ajili ya bidhaa/ huduma zangu?

Ukishapata majibu ya maswali hayo hapo juu ni wazi kuwa utakuwa ulishaanza kujua ni biashara gani unaweza kuianzisha. Lakini pia unatakiwa ujiulize maswali haya hapa ili kuwa na uhakika na biashara ambayo utaifanya.

 • Ninakusudia kuanzisha Biashara gani?
 • Nitauza bidhaa gani au nitatoa huduma gani? Biashara nitafanyia eneo gani?
 • Nitatumia ujuzi na uzoefu gani kwenye biashara?
 • Biashara yangu itakuwa na muundo gani kisheria?
 • Niiite biashara yangu jina gani?
 • Nitatumua vifaa gani, na nitakuwa na mahitaji gani?
 • Nahitaji bima ya aina gani?
 • Nahitaji fedha kiasi gani?
 • Nina rasilimali zipi?
 • Nitajilipaje?

Majibu yako yatasaidia kutengeneza mpango makini, uliofanyiwa utafiti wa kutosha, ambao utautumia kama ramani ya kuelekeza kila hatua katika utekelezaji wa biashara na hata kupata mtaji.

Chagua muundo sahihi wa biashara yako.

Unapoanzisha biashara yoyote, mojawapo ya maamuzi muhimu sana ya kufanya ni uchaguzi wa muundo wa hiyo biashara. Mambo yanayozingatiwa katika kuchagua muundo wa biashara ni pamoja na:

 • Masharti ya kisheria
 • Uwajibikaji wa wamiliki kwa madeni ya biashara
 • Aina ya shughuli za biashara
 • Mgawanyo wa mapato
 • Mahitaji ya mtaji
 • Idadi ya wafanyakazi na utawala
 • Manufaa na hasara za kihasibu/ kikodi
 • Urefu wa mzunguko wa biashara

Tuishie hapa kwa leo, wiki ijayo tutajifunza aina za biashara.

Ukitaka kupata habari zaidi za ujasiriamali tembelea tovuti www.wajasiriamalitz.or.tz

Imeandaliwa na Veneranda Sumila

Taasisi ya sekta binafsi Tanzania

Aina za muundo wa biashara

Utangulizi

Wiki iliyopita tulijifunza mambo mbalimbali unayotakiwa kufanya kabla ya kuanzisha biashara. Baada ya kujua mambo hayo sasa tujifunze aina mbalimbali za biashara.

Mojawapo ya maamuzi ya mwanzoni kabisa unayohitaji kufanya kwa ajili ya biashara yako mpya ni kuchagua aina ya muundo wa biashara unaoona unakufaa. Uchaguzi unaofanya ni muhimu kwa kuwa utaathiri uwezo na mamlaka ya biashara yako kufanya au kutofanya jambo fulani. Kuwa na aina na muundo sahihi wa biashara kutakusaidia kukuongoza wakati biashara yako iko kwenye mafanikio au wakati wa taabu.

Muundo sahihi wa biashara ndio utakuongoza nini cha kufanya ikiwa utashtakiwa, na kwa namna gani wewe na biashara yako mtatozwa kodi. Kimsingi ziko namna kuu tatu za kuunda biashara, zimeelezewa hapa chini

 • Biashara inayoendeshwa na mtu binafsi peke yake
 • Biashara inayomilikiwa na kuendeshwa kwa Ubia
 • Kampuni yenye ukomo wa madeni

Biashara inayomilikiwa/ kuendeshwa na mtu mmoja

Biashara inayoendeshwa na mtu binafsi peke yake, au Mfanyabiashara pekee ni aina ya biashara ambayo imeenea sana miongoni mwa wajasiriamali nchini. Hii ni biashara ambayo ni rahisi sana kuanzisha kwani mmiliki hufanya usajili wa jina la biashara na kutimiza masharti mengine machache kabla ya kufungua bishara.

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) imetoa mwongozo wa kusajili jina la biashara ambapo mjasiriamali atatakiwa kulipia wastani wa Shilingi 20,000. Mwongozo huu unapatikana kwenye tovuti ya Brela. Mada zijazo pia tutajadili namna ya kusajili biashara.

Biashara inayomilikiwa na mtu mmoja inaweza kuendeshwa kwa jina la mmiliki au jina jingine lisilo lake. Biashara ya aina hii imejipatia umaarufu mkubwa sana kutokana na urahisi wake, haswa katika uanzishaji, pamoja na gharama ndogo. Mfanyabiashara anahitaji tu kujisajili au kusajili jina lake na kupata leseni na hivi hutosha kuanza kufanya biashara.

Hasara kubwa ya kipekee ya muundo huu wa biashara ni kuwa mmiliki anabeba majukumu kwa madeni yote ya biashara yake. Hivyo ikiwa atapata matatizo ya kifedha, wadeni wanaweza kufungua kesi/ madai dhidi yake na yakifanikiwa yeye binafsi atawajibika kulipa madeni hayo kutoka kwenye vyanzo binafsi vya fedha.

Ubia

Hii ni biashara inayotambulika kisheria inayofanywa na watu wawili au zaidi wanaoshiriki katika umiliki, utendaji na faida au hasara za biashara hiyo. Ziko aina kuu mbili za ubia, ubia wa jumla (usio na ukomo wa madeni) na ubia wenye ukomo wa madeni.

Katika ubia usio na ukomo wa madeni (ubia wa jumla), wabia wanaendesha biashara na wanawajibika kwa madeni ya biashara na mali zao binafsi zinaweza kulipia madeni hayo. Kwenye ubia wenye ukomo wa madeni, baadhi ya wabia huwa na ukomo wa kuwajibika kwa madeni ya biashara na baadhi huwa hawana. Wale wasio na ukomo wa kuwajibika kwa madeni ya biashara wanamiliki biashara na wanawajibika binafsi kwa madeni ya biashara, na wale wenye ukomo huwekeza tu, hawana nguvu ya moja kwa moja katika maamuzi ya biashara na hawawajibiki kuchangia fedha binafsi kulipa madeni ya biashara.

Uwajibikaji binafsi wa wabia kwa madeni ya biashara ni suala kubwa la kufikiria iwapo unatazamia kuendesha biashara kwa mfumo wa ubia. Kama ilivyo kwa wafanyabiashara wanaomiliki biashara peke yao, wabia wanawajibika kwa fedha zao binafsi kulipia madeni ya biashara. Kila mbia wa jumla (asiye na ukomo wa madeni) anaweza kufanya maamuzi na kuingia katika makubaliano ambayo wabia wenzake wote watayaheshimu na yatawaathiri (kutegemeana na makubaliano/ mkataba wa ubia wao) kwa niaba ya biashara.

Kumbuka kuwa biashara ya ubia ina gharama kubwa zaidi kuianzisha na kuiendesha kuliko biashara ya mtu binafsi, hii inatokana na ukweli kuwa kuna taratibu mbalimbali inabidi zifuatwe kabla ya biashara kuanza. Taratibu hizo ni pamoja na kuweka makubaliano ya namna ya kuendesha biashara, mgawanyo wa mapato na mengine mengi.

Ikiwa utaamua kuendesha biashara kwa mfumo wa ubia, hakikisha kuwa umeweka kimaandishi makubaliano au mkataba kuonesha namna maamuzi yatakavyofanyika, namna ya kumaIiza tofauti zinazotokea katika kufanya maamuzi, na hata namna ya kufikia makubaliano ya kubadilisha umiliki wa biashara itakapohitajika kufanya hivyo. Makubaliano hayo yanasaidia sana pale itakapotokea kwa sababu moja au nyingine biashara imeingia katika matatizo ya kifedha au ya kiuendeshaji, au ikitokea mbia mmojawapo anataka kuondoka kwenye biashara.

Mkataba wa ubia unapaswa kukazia kuhusu kusudi la biashara na mamlaka na wajibu wa kila mbia. Ni vema kupata msaada wa kisheria kutoka kwa mwanasheria mwenye uzoefu na mambo ya biashara ndogo na za kati katika kuandika mkataba wa ubia. Mambo mengine ambayo ni muhimu yazungumziwe katika makubaliano ya ubia ni:

 • Umiliki utachangiwa kwa viwango gani? Si lazima viwango vya umiliki na na mgawanyo wa majukumu vilingane kati ya wabia wote. La msingi ni kuhakikisha kiwango cha kila mmoja kiko katika makubaliano.
 • Maamuzi yatafanyika kwa mtindo gani? Ni vema kuweka makubaliano juu ya haki za kupiga kura baina ya wabia ikiwa wameshindwa kufikia muafaka kwenye suala fulani. Ikiwa wabia ni wawili tu na umiliki wao ni nusu kwa nusu, uko uwezekano wa kushindwa kufikia muafaka katika kuamua jambo. Kuepusha hili, biashara zingine huamua kuweka mbia wa tatu, mtu anayeaminika na kummilikisha asilimia ndogo tu ya biashara, ili kusaidia kuiondoa biashara kwenye mkwamo wa aina hiyo.
 • Ikiwa mbia mmoja atajiondoa, kiasi cha kumlipa kitaamuliwaje? Namna mojawapo ya kuamua kuhusu hili ni kuwa na mhusika aliye nje ya ubia, mfano benki, au mhasibu kutafuta mtathmini atakayethaminisha kiasi cha kumlipa mbia anayejitoa katika ubia.
 • Ikiwa mbia atajitoa katika biashara, ni lini anapaswa kulipwa fedha yake? Hii inaweza kuwekwa katika makubaliano ili ijulikane bayana. Ikiwa itachukua muda mrefu, inaweza kuwa busara kuweka makubaliano kuwa ilipwe pamoja na riba. Bila makubaliano haya uendeshaji biashara unaweza kuathirika ikiwa mtu atajitoa na kiasi chote kulazimika kulipwa kwa mkupuo kwa haraka mara anapojitoa.

2.4 Kampuni yenye ukomo wa madeni

Kampuni yenye ukomo wa madeni ni muundo wa shirika ambamo uwajibikaji wa wamiliki (wanahisa) kwa madeni ya biashara unakomea kwenye kiasi walichowekeza katika kampuni, au ambacho wamekubaliana kukiweka dhamana kwa ajili ya kampuni. Hivyo kampuni yenye ukomo wa madeni inaweza kuwa na ukomo kwa njia ya hisa au ukomo kwa njia ya dhamana waliyoweka wanahisa. Suala la nani anaweza kuwa mwanahisa wa kampuni binafsi linatawaliwa na sheria na kanuni za kampuni.

Kama ilivyo kwa biashara zingine zinazoendeshwa hapa nchini, Kampuni yenye ukomo wa madeni inapaswa kusajiliwa na Mamlaka ya Usajili na Leseni za Biashara, ambayo iko chini ya wizara inayohusika na Biashara. Katika usajili, hatua ya kwanza ni kupata kibali cha kutumia jina la biashara kinachotolewa na mamlaka hiyo. Nyaraka/ taarifa zifuatazo zinahitajika katika mchakato wa kuanzisha kampuni:

 • Jina la kampuni (ambalo lazima lipitishwe na msajili wa makampuni);
 • Anuani rasmi ya ofisi ya kampuni Tanzania;
 • Majina, anuani, na utaifa wa wanahisa wa kwanza na wakurugenzi wa kampuni (angalau wawili kwa kampuni binafsi au saba kwa kampuni ya umma).
 • Mkataba wa kuanzisha kampuni (unaotaja madhumuni ya kampuni) na sheria/ makubaliano yanayosimamia utendaji na maamuzi ya kampuni (inayotaja muundo wa uongozi na michakato ya maamuzi mbalimbali). Angalau nakala mbili za kila waraka zinapaswa kuwasilishwa.;
 • Kujaza fomu maalumu zenye tamko kuwa kampuni imezingatia matakwa ya sheria ya makampuni Tanzania; na
 • Kulipa tozo/ ada za kuwasilisha nyaraka, usajili, na ushuru wa stempu.

Tuishie hapa kwa leo….. wiki ijayo tutaongelea masuala ya kodi na leseni kwa biashara yako.

Kwa taarifa zaidi tembelea www.wajasiriamalitz.org

Imeandaliwa na Veneranda Sumila

Taasisi ya sekta binafsi

Masuala ya Kodi na Leseni kwa Biashara Yako

Kuwa mmiliki wa biashara ndogo kunaambatana na changamoto mbalimbali ambazo zinaendana na ukubwa na shughuli za biashara yenyewe. Mmiliki analazimika kukabili changamoto hizo, zikiwemo za uuzaji, usambazaji, usimamizi wa fedha na kuhakikisha biashara inakua. Haya yote anayafanya huku akiwa na wafanyakazi wachache, au pengine bila kuwa na hata mmoja. Katika kujaribu kufanikisha, anakabiliwa pia na changamoto muhimu ya kufanya shughuli za kiutawala. Utawala wenye ufanisi katika biashara unaleta matokeo mazuri kwa mfanyabiashara binafsi na ustawi wa biashara yake pia. Ni muhimu kufanya yafuatayo kuhakikisha unafanya baishara yako kwa mujibu wa kanuni na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sajili jina la biashara yako

Kabla ya kufanya taratibu nyingine zozote, mjasiriamali atatakiwa kusajili jina la biashara. Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) ndio inajukumu la kusajiri majina yote ya biashara nchini.

Utatakiwa kuwasilisha kwa Brela mapendekezo ya majina matatu ya biashara yako. Lengo la kupeleka majina matatu ni kuhakikisha kuwa angalau jina moja kati ya hayo matatu haliingiliani na majina mengine ambayo tayari yalishasajiliwa. Kwa hiyo ikiwa jina la kwanza ulilopendekeza litaingiliana na lililosajiliwa tayari mamlaka itasajili jina la pili na kama nalo litapatikana lipo tayari pendekezo la tatu ndio litasajiliwa.

Gharama za kusajili jina la biashara kwa mujibu wa Brela ni Shilingi 20,000 na usajili unaweza ukafanyika pia kwa njia ya mtandao.

Maelezo zaidi ya namna ya kusajili jina la biashara yanapatikana katika tovuti ya Brela, kwa kufika katika ofisi zao zilizopo Dar es salaam na Mwanza au kupitia mawakala wao.

 Jisajili na Mamlaka ya Mapato

Mara biashara au kampuni inapokamilishwa kusajiliwa na msajili wa makampuni, inalazimika kusajiliwa na ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliyo karibu. Hati ya kwanza unayopaswa kupewa na Mamlaka ya Mapato ni namba ya utambulisho ya mlipakodi (TIN). Kwa kawaida namba hii inapatikana ndani ya siku tatu.

TIN inapotolewa, jalada la kodi linafunguliwa. Namba ya jalada inapotolewa, kampuni inategemewa kujaza fomu ya muda (ya makadirio) ya taarifa za kodi ya mapato. Fomu hizi za muda zinapaswa kuwasilishwa ndani ya miezi mitatu tangu kuanza kwa biashara. Kampuni inatakiwa kukadiria faida yake kwa mwaka wa kwanza na kulipa kodi kwa makadirio hayo mara nne kwa mwaka. Kingine kinachotolewa TRA baada ya namba ya jalada kupatikana ni cheti cha kukamilisha hatua za awali za kodi, ambacho kinaweza kutumika kupata leseni ya biashara.

Ikiwa mauzo ya biashara kwa mwaka ni kuanzia shilingi milioni mia moja, biashara hiyo inalazimika pia kujisajili kwa ajili ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT). VAT inatozwa katika kiwango cha asilimia 18 ya mauzo. Ili kujisajili kwa ajili ya VAT, mwombaji anapaswa kujaza fomu ya maombi inayopatikana katika idara ya VAT ya TRA. Fomu inapaswa kukamilishwa na kurejeshwa pamoja na nakala ya nyaraka zifuatazo;

 • Cheti cha usajili cha kampuni (kwa kampuni) au cheti cha usajili (kwa biashara zinazomilikiwa kwa muundo wa ubia au kumilikiwa na mtu mmoja pekee);
 • Mkataba wa kuanzisha kampuni na sheria za ndani za kampuni, ambavyo vinaonesha, pamoja na mambo mengine, iwapo malengo ya kampuni yaliyotajwa katika mkataba wa kuanzisha kampuni yanairuhusu kampuni kufanya shughuli ambazo zinaombewa leseni.;
 • Ushahidi wa uraia wa Tanzania, kwa mfano nakala ya hati ya kusafiria, cheti cha kuzaliwa, au kwa ambaye sio raia, kibali cha kuishi nchini cha daraja A (kinachoonesha kuwa mwenye kibali ni mwekezaji kwenye kampuni/ biashara hiyo);
 • Ikiwa wanahisa wa kampuni sio raia na hawana vibali vya kuishi nchini, hati ya kiapo ya raia/ mkazi inapaswa kuwasilishwa;
 • Ushahidi kuwa mwombaji ana eneo linalofaa kwa ajili ya biashara anayoiombea leseni. Ushahidi ambao unaweza kuwasilishwa ni hati ya ardhi, mkataba wa pango, stakabadhi ya kulipa pango, au stakabadhi ya kulipa kodi ya ardhi au pango;
 • Namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) iliyotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania;
 • Cheti cha kukamilisha hatua za awali za kodi kilichotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (idara ya kodi ya mapato);
 • Leseni ya biashara iliyotolewa na wizara ya viwanda na biashara au mamlaka ya serikali za mitaa, chini ya sheria ya leseni za biashara; na
 • Picha tatu za mwombaji, au mmoja wa wakurugenzi wakazi wa kampuni au mwakilishi ambaye yupo nchini.

 

Pata vibali/ leseni za biashara

Aina na idadi ya vibali/ leseni zinazohitajika hutofautiana kati ya sekta moja na nyingine, kutegemeana na kiwango cha udhibiti katika sekta husika. Kiujumla inashauriwa kutafuta ushauri wa kisheria kuhusu vibali vinavyohitajika katika sekta unayokusudia kuingia. Pamoja na kukidhi matakwa ya sekta husika, kila biashara inapaswa kupata leseni ya ‘jumla’, inayotolewa kwa mujibu wa Sheria ya Leseni za Biashara ya mwaka 1972. Ili kupata leseni ya jumla ya biashara, mwombaji analazimika kuwasilisha nyaraka zifuatazo:

 • Kivuli cha cheti cha usajili wa kampuni, cheti cha kufuata sheria (kwa makampuni) au cheti cha usajili (kwa biashara zinazomilikiwa na mtu binafsi au kwa ubia).
 • Mkataba wa kuanzisha kampuni na sheria za ndani za kampuni, ambavyo vinaonesha, pamoja na mambo mengine, iwapo malengo ya kampuni yaliyotajwa katika mkataba wa kuanzisha kampuni yanairuhusu kampuni kufanya shughuli ambazo zinaombewa leseni.;
 • Ushahidi wa uraia wa Tanzania, kwa mfano nakala ya hati ya kusafiria, cheti cha kuzaliwa, au kwa ambaye sio raia, kibali cha kuishi nchini cha daraja A (kinachoonesha kuwa mwenye kibali ni mwekezaji kwenye kampuni/ biashara hiyo);
 • Ikiwa wanahisa wa kampuni sio raia na hawana vibali vya kuishi nchini, hati ya kiapo ya raia/ mkazi inapaswa kuwasilishwa;
 • Ushahidi kuwa mwombaji ana eneo linalofaa kwa ajili ya biashara anayoiombea leseni. Ushahidi ambao unaweza kuwasilishwa ni hati ya ardhi, mkataba wa pango, stakabadhi ya kulipa pango, au stakabadhi ya kulipa kodi ya ardhi au pango
 • Namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) iliyotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania;

Kama ilivyodokezwa awali hapo juu,  mjasiriamali atatakiwa kutimiza masharti mengine kama ilivyoainishwa kisheria ili kupata vibali kutoka taasisi za udhibiti kisekta.

Ifuatayo ni mifano ya matakwa mahsusi ya sekta:

 • Leseni ya uwakala wa forodha (inayotolewa na TRA) kwa wanaotaka leseni ya kuendesha biashara ya uwakala wa forodha (kusafirisha mizigo nje ya nchi na kutoa mizigo inayoingia nchini.
 • Leseni ya wakala wa utalii (inayotolewa na wizara ya maliasili na utalii) kwa waombaji wa kibali cha kufanya biashara za utalii kama vile hoteli ya kitalii, wakala wa usafirishaji, uwindaji, uongozaji wa watalii, n.k.
 • Kibali cha utafutaji/ uchimbaji madini (kinachotolewa na wizara ya nishati na madini) kwa waombaji wa leseni za kufanya bishara zinazohusisha uchimbaji madini.
 • Kibali cha mawasiliano/utangazaji/ usambazaji habari (kinachotolewa na mamlaka ya mawasiliano) kwa wale waombaji wa leseni ya kufanya biashara ya utangazaji (redio, TV), mawasiliano ya simu, intaneti, n.k.
 • Leseni ya bima (Inayotolewa na wakala wa usimamizi wa bima) kwa wale wanaoomba kibali cha kuendesha biashara ya bima.
 • Kibali/leseni maalum (kinachotolewa na mamlaka ya chakula na dawa Tanzania) kwa waombaji wa leseni ya biashara inayojihusisha na chakula, dawa, na vipodozi.
 • Leseni ya uvuvi (inayotolewa na wizara ya maliasili na utalii) kwa waombaji wa kibali cha kuendesha biashara ya uvuvi.
 • Vyeti/ vibali vya kitaaluma, kwa biashara zinazotegemea taaluma kama vile madaktari, wanasheria, marubani, wahasibu, manahodha wa meli, n.k. (hivi hutolewa na taassisi/ bodi za taaluma hizo).
 • Leseni za viwanda (inayotolewa na wizara ya viwanda na biashara), kwa waombaji wa leseni za kuanzisha viwanda.
 • Kwa bishara zinazohusisha kutoa huduma za ulinzi, lazima kibali kitolewe na Mkuu wa jeshi la polisi, chini ya wizara ya mambo ya ndani.

Tuishie hapa kwa leo, wiki ijayo mambo mengine zaidi kuhusiana na biashara. Ukitaka kupata habari zaidi za ujasiriamali tembelea tovuti www.wajasiriamalitz.or.tz

Imeandaliwa na Veneranda Sumila

Taasisi ya sekta binafsi Tanzania

Namna ya kupata fedha kwa ajili ya biashara yako

Namna ya kupata fedha ni jambo la msingi kuliko yote katika shughuli za biashara, japo linaweza lisiwe jambo rahisi sana, kimsingi linaweza kuwa jambo gumu na la kukatisha tamaa wakati mwingine. Hata hivyo, ukiwa unafahamu na umejipanga vizuri, kupata fedha kwa ajili ya biashara yako linaweza lisiwe suala linaloambatana na maumivu makali.

Vifuatavyo ni baadhi ya vyanzo vya fedha (Mtaji)

 • Mtaji kutoka kwa Mmiliki: Hapa mjasiriamali huanza kujitunzia kiasi kidogo kidogo cha pesa kama akiba. Pesa hii yaweza kutunzwa benki au kuhifadhiwa vizuri ndani. Wengi huweka kisanduku maalumu ambacho si rahisi kukivunja na humo hutumbukiza kiasi cha pesa alichojipangia, baada ya mwaka mmoja hukivunja kisanduku na kupata pesa ya kuanzia biashara yake. Mara nyingi hiki huwa chanzo pekee cha fedha kwa biashara ndogo ambayo ni mpya. Kwa biashara kubwa, au zenye ubora na zinazokuwa kwa kasi, aina nyingine za kupata mtaji hutumika.
 • Mtaji kutokana na mikopo: Hapa mjasiriamali huamua kukopa fedha kutoka katika vyanzo mbalimbali vya fedha kama vile benki, saccoss au hata vikoba. Kabla hujaamua kukopa fedha hakikisha umefanya utafiti wa kutosha kuhusiana na taasisi unayoenda kukopa. Tutajadili kwa kina kuhusiana na mikopo
 • Ubia: Njia nyingine nzuri ya kupata fedha kwa ajili ya biashara ni kuanzisha ubia. Hapa mtu huangalia watu au biashara ambazo anahisi kama atashirikiana nazo zitamsaidia kupata mtaji wa biashara yake. Hata hivyo, ili hii iwezekane, unatakiwa mkataba mzuri na makubaliano ya ubia huo yaonyeshe mtaji ambao kila mtu atakayehusika na biashara hiyo atachangia na namna ambavyo atanufaika.
 • Familia na marafiki: Kutumia wanafamilia na marafiki ni njia nzuri mbadala ya kukuza mtaji wa biashara. Hapa mtu anayependa kuanzisha biashara anaweza kutafuta msaada wa fedha kutoka kwa wanafamilia au marafiki ambao wanaweza kusaidia jitihada zake. Anaweza kuomba akopeshwe na kuahidi kurejesha au anaweza kuomba asaidiwe kwa kuchangiwa na wanandugu.

Kabla ya kuamua kuhusu vyanzo vipi vya fedha vitakuletea mtaji, ni muhimu kujiuliza  maswali yafuatayo:

 • Hitaji lako ni la haraka kiasi gani? Unaweza kupata mkopo wenye masharti rafiki ikiwa ulijipanga mapema na kuomba mkopo kwa wakati, kuliko ukitafuta mkopo kwa haraka.
 • Biashara yako ina hatari zipi? Kila biashara ina hatari zake, na kiwango cha hatari kitaathiri gharama za vyanzo mbalimbali vya fedha na namna ya kupata fedha.
 • Fedha itatumika kwa ajili gani? Wakopeshaji wengi hutaka fedha ziombwe kwa ajili ya matumizi mahsusi.
 • Soko liko katika hali gani? liko katika hali ya kuporomoka, liko imara, au linakua? kila hatua katika soko inahitaji namna tofauti ya kutazama uhitaji wa fedha na vyanzo vya fedha. Biashara zinazofanikiwa wakati zingine zikiporomoka zitapata fedha kwa urahisi na masharti nafuu kuliko zingine..
 • Biashara yako ni ya msimu? Mahitaji ya fedha kwa biashara ya msimu mara nyingi huhitaji vyanzo vya fedha za muda mfupi.
 • Safu yako ya uongozi ina ubora gani? Uongozi ni jambo linalotizamwa sana na vyanzo vingi vya fedha.
 • Pengine la muhimu kuliko yote, hitaji lako linaendana vipi na mpango/ mchanganuo wako wa biashara? Ikiwa huna mchanganuo wa biashara, lipe kipaumbele suala la kuandika mpango huo. Vyanzo vyote vya mitaji vitapenda kuona mpango wako wa kuanzisha au kupanua biashara.

Kupata fedha kupitia mikopo

Imesemwa mara nyingi kuwa biashara ndogo hupata changamoto kukopa fedha. Sio mara zote kauli hii ina ukweli. Ikumbukwe kuwa biashara kubwa ya mabenki ni kukopesha. Unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha kuwa unajiandaa vyema kabla ya kuomba mkopo. Unapoomba mkopo huku ukiwa hujajiandaa vya kutosha kunapeleka kiashiria kibaya kwa mkopeshaji wako kuhusu uwezo wako wa kulipa. Ili kufanikiwa kupata mkopo, ni lazima uwe umejiandaa na kujipanga. Ni lazima ujue kiasi sahihi unachohitaji, kwa nini unakihitaji, na utakirejesha namna gani. Unatakiwa kuweza kuwashawishi wakopeshaji kuwa wewe sio mkopaji atakayewatia hasara.

Aina za mikopo kwa biashara ndogo

Ziko aina kuu mbili za mikopo, mkopo wa muda mfupi na mkopo wa muda mrefu. Kwa kawaida, mkopo wa muda mfupi unatakiwa kulipwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja wakati mikopo ya muda mrefu ni ile inayopaswa kulipwa baada ya muda unaozidi mwaka mmoja, ingawa mara nyingi si zaidi ya miaka saba. Mikopo kwa ajili ya mali za muda mrefu kama ardhi, nyumba au mitambo inaweza kuwa na kipindi kirefu cha kulipa, kinachoweza kufikia hata miaka 25.

Kukubaliwa kwa maombi yako ya mkopo kunategemea na jinsi unavyojieleza na jinsi unavyoelezea biashara yako. Kumbuka, wakopeshaji wanapenda sana kutoa mkopo lakini watatoa mkopo pale tu watakapopata uhakika kuwa utarejeshwa.

Namna bora ya kuboresha uwezekano wa kupata mkopo ni kuandaa maombi ya mkopo kwa maandishi, na kuhakikisha maombi hayo yana uhalisia na yana ushawishi kwa mkopeshaji kukukopesha fedha.

Maombi ya mkopo yaliyoandikwa vizuri yanajumuisha vipengele vifuatavyo:

 • Taarifa za jumla
 • Maelezo ya biashara
 • Sifa za viongozi
 • Taarifa kuhusu soko
 • Taarifa za kifedha

Yafuatayo ni maelezo zaidi kuhusu vipengele vilivyotajwa hapo juu

Taarifa za jumla

Kiujumla, maombi ya mkopo yanajumuisha taarifa zifuatazo:

 • Jina la biashara, majina ya maafisa wakuu, namba ya hifadhi ya jamii ya kila afisa mkuu, na anwani ya biashara.
 • Lengo la mkopo (mkopo unaoomba utatumikaje na ni kwa nini unahitajika)
 • Kiasi cha pesa unachohitaji kukopa ili kutimiza lengo lako.

 

Maelezeo ya Biashara

Maelezo ya biashara yatajumuisha taarifa zifuatazo

 • Historia na aina ya biashara (maelezo ya kina kuhusu aina ya biashara, umri wake, idadi ya waajiriwa, mali zake)
 • Muundo wa umiliki (maelezo ya muundo wa kisheria wa umiliki wa biashara yako)

Sifa za Viongozi

Tengeneza taarifa fupi kuhusu kila afisa mkuu katika biashara yako inayoelezea:

 • Historia
 • Elimu
 • Uzoefu
 • Ujuzi
 • Mafanikio

Taarifa kuhusu soko

Ni muhimu taarifa kuhusu soko ;

 • kuelezea bayana bidhaa za kampuni yako pamoja na soko.
 • kubainisha washindani wako na elezea namna biashara yako itakavyoshindana katika soko.
 • kuelezea wateja wako na namna ambavyo biashara yako itatosheleza mahitaji yao.

Taarifa za kifedha

Taarifa hizi huhitajika sehemu nyingi wanazotoa mikopo. Unapotengeneza taarifa hizi ni muhimu kuonesha;

 • Taarifa za kifedha kama taarifa za hali ya kifedha, taarifa za mapato na matumizi kwa miaka mitatu iliyopita. Ikiwa ni biashara mpya, tengeneza makadirio ya taarifa hizo kwa miaka ijayo.
 • Pia zinahitajika taarifa binafsi za fedha za kwako na wamiliki wakuu wa biashara.
 • Dhamana ambayo unakusudia kuweka kwa ajili ya mkopo unaoomba.

Namna maombi yako ya mkopo yanayotathminiwa

Anapopitia maombi ya mkopo, mkopeshaji huwa kimsingi anatizama kuhusu ulipaji wa deni lake. Kwa nchi zilizoendelea maafisa mikopo huomba ripoti ya mikopo ya mwombaji kutoka kwa wakala wa kuthaminisha hali za wakopaji Ili kupima uwezo wa mlipaji kurejesha deni. Kwa Tanzania wakala wa kudhamanisha  hali za wakopaji imeanzishwa miaka miwili iliyopita hivyo huenda ikawa haina taarifa za kutosha za wakopaji hivyo kupelekea wakopeshaji kutegemea zaidi maelezo yaliyoambatanishwa ili kujiridhisha kama unakopesheka ama la. Hivyo unapaswa kuandika maombi yako kwa lugha inayoeleweka na kwa ufasaha ili kuwashawishi wakopeshaji.

Mambo yanayozingatiwa na Maafisa mikopo

Ingawa uchambuzi na vigezo hutofautiana baina ya wakopeshaji, kwa kutumia ripoti ya mkopo na taarifa ulizowasilisha, afisa mikopo atazingatia yafuatayo:

 • Kama umewekeza akiba zako binafsi kwa kiwango cha angalau asilimia 25 hadi asilimia 50 ya mkopo unaoomba. (kumbuka kuwa mkopeshaji au mwekezaji hatakuwa tayari kuwekeza katika biashara yako kwa asilimia 100)
 • Kama una rekodi nzuri ya kuaminika katika madeni yako. Kama inavyooneshwa na historia za madeni yako ya nyuma ya mikopo, umeme, maji, historia ya kazi/ ajira, na barua za wadhamini. Hili ni la muhimu sana.
 • Kama una uzoefu na ujuzi wa kutosha kuendesha biashara kwa ufanisi.
 • Kama umeandaa maombi ya mkopo na mchanganuo wa biashara ambao unadhihirisha uelewa wako na nia ya mafanikio ya biashara yako.
 • Kama biashara ina mtiririko/ mzunguko wa kutosha wa fedha kuiwezesha kulipa mkopo kwa awamu zilizowekwa.

Pia Maafisa mikopo wanakutathmini kwa vigezo vifuatavyo;

 • Tabia: Hapa wakopeshaji hutathmini ni kwa kiasi gani mkopaji anaonekana kuwajibika kulipa madeni yake, hupima uwezo huu kwa kupitia historia ya mikopo na ulipaji wa mkopaji.
 • Uwezo wa kulipa: Tathmini isiyo na kanuni maalum ya uwezo wa kulipa hufanywa na mkopeshaji kwa kuzingatia uchambuzi wa taarifa za fedha na taarifa zingine.
 • Dhamana: Hii ni mali ya mkopaji ambayo huwekwa kama kinga kwa mkopeshaji iwapo mkopaji atashindwa kulipa. Kiwango cha dhamana kinatofautiana baina ya wakopeshaji mbalimbali. Kadri thamani ya dhamana inavyozidi kukaribiana na thamani ya mkopo unaoombwa, ndivyo ambavyo utayari wa mkopeshaji unazidi kuwa mkubwa, na kuamini kuwa kiasi kinachokopwa kitarejeshwa.
 • Hali ya soko: Hali za kiuchumi, kijiografia, na za uzalishaji katika soko.
 • Kujiamini: Mkopaji mzuri anashawishi wakopeshaji kumuamini kwa kuandaa maombi yake ya mikopo kwa ufanisi na ufasaha. Maombi yake ya mkopo yanabeba taswira kuwa mwombaji ni mweledi, mwenye kuheshimika, mwenye historia nzuri karika mambo ya mikopo, mwenye taarifa za fedha zinazokubalika, mwenye mtaji mzuri na mwenye dhamana inayokidhi vigezo.

Haya ni baadhi tu ya mambo ya msingi ya kuzingatia unapotafuta mtaji kwa ajili ya biashara yako na namna wakopeshaji wanavyochambua hitaji lako. Ukitaka kupata habari zaidi za ujasiriamali tembelea tovuti www.wajasiriamalitz.or.tz

Imeandaliwa na Veneranda Sumila

Taasisi ya sekta binafsi Tanzania

Utunzaji wa kumbukumbu

Wiki iliyopita tulijifunza kuwa Utunzaji na udhibiti wa fedha ni muhimu sana kwa ustawi wa biashara yoyote, biashara ambayo inafanya vizuri lakini haina usimamizi vema wa fedha inaweza kufa. Ni lazima mjasiriamali adhibiti matumizi ya fedha zinazopatikana ili asitumie kupita kiasi (overspend), pia kufanya hivyo kutasaidia kujua vyema mapato na matumizi yako.

Pia tulijifunza namna ya kukadiria mtiririko wa fedha, tuliona kuwa makadirio ya mtiririko wa fedha hutumika kupima iwapo fedha inayokadiriwa kukusanywa ndani ya kipindi husika itatosha kukidhi kiasi kinachokadiriwa kulipwa ndani ya kipindi hicho Leo tutajifunza zaidi kuhusu utunzaji wa kumbukumbu za kifedha.

Kutunza Kumbukumbu za kifedha

Utunzaji wa kumbukumbu za kifedha ni muhimu sana kwa ustawi wa biashara yako. Ukiamua kutunza kumbukumbu zako za kifedha kwa usahihi kutakusaidia kupanga mipango ya baadae ya biashara yako.  Ukiwa na kumbukumbu za fedha utaweza kufanya maamuzi bora ya biashara yako hususani kuhusu vyanzo vya mapato, kodi, matumizi binafsi ya mmiliki wa biashara na hata kustaafu katika biashara.

Kama mjasiriamali ni vyema sana uweke utaratibu wa kutunza taarifa sahihi za miamala ya kifedha inayofanyika na kuonesha namna fedha zilivyotumika. Utunzaji wa kumbukumbu za kifedha utakusaidia kutoa taarifa kuhusu namna taasisi inavyoendeshwa na ikiwa inafanikiwa kutimiza malengo yake ama la.

Umuhimu wa kumbukumbu

 1. i) Taarifa: Kila biashara inahitaji kutunza kumbukumbu za miamala yake ya kifedha ili waweze kupata taarifa kuhusu hali yao kifedha, ikiwa ni pamoja na:

Taarifa fupi ya mapato na matumizi na mgawanyiko wake katika vipengele mbalimbali.

Matokeo ya shughuli za biashara – ziada (faida) au upungufu (hasara).

Mali na madeni – au vitu vinavyomilikiwa na biashara na vile ambavyo biashara inadaiwa.

 1. ii) Uaminifu: Kutunza kumbukumbu sahihi za kifedha kunachochea uadilifu, uwajibikaji na uwazi, na kuepuka hisia za kukosa uaminifu hasa kwa wakopeshaji au wawekezaji ambao wangependa kushirikiana nawe katika biashara.

iii) Mipango ya baadaye: Pamoja na kuwa taarifa za kifesha zinaripoti mambo yaliyokwishatendeka, zinasaidia utawala kuweka mipango ya mbeleni na kuelewa zaidi kuhusu uendeshaji wa biashara. Ukiwa na taarifa za miaka miwili mitatu ni rahisi kupata taswira ya mwenendo wa biashara.

Namna za kutunza kumbukumbu za kifedha

Kumbukumbu za kifedha zinaweza kutunzwa katika mfumo wa kuandika kwa mikono katika vitabu vya fedha, au kutumia mfumo wa kompyuta ambapo unaweza kutumia mojawapo ya programu za kihasibu za kompyuta.

Namba mbili kuu za utunzaji wa kumbukumbu za fedha ni:

 • Kurekodi kwa kuzingatia miamala ya fedha taslimu tu
 • Kurekodi kwa kuzingatia msingi wa muamala, hata ikiwa ni deni

Mfumo wa kurekodi fedha taslimu tu

Hii ni namna rahisi sana ya kutunza kumbukumbu za kifedha na haihitaji ujuzi wa juu katika utunzaji wa mahesabu. Sifa zake ni:

 1. i) Malipo yanaandikwa kwenye jedwali la fedha taslimu mara yanapofanyika, kadhalika makusanyo pia yanaandikwa katika jedwali hilo mara yanapotokea.
 2. ii) Mfumo huu haujishughulishi na malipo yaliyofanyika kwakati uliopita, au kiasi cha malipo ambayo bado yanadaiwa.

iii) Mfumo huu hauweki moja kwa moja kumbukumbu za madeni au mali za biashara

 1. iv) Mfumo huu hautunzi kumbukumbu za miamala isiyohusisha fedha taslimu moja kwa moja, mfano Uchakavu wa mitambo. .

Mfumo wa kutambua madeni katika kuweka kumbukumbu

Huu ni mfumo rasmi wa kihasibu unaoweka kumbukumbu kwa kutambua na kuandika pande mbili za kila muamala unaofanyika, ambazo zinahusisha kutoa na kupokea.

Pande mbili za jedwali hutumika, yaani upande wa kushoto na upande wa kulia. Mfumo huu ni wa kisasa na unahitaji ujuzi wa kanuni za kihasibu.

 1. i) Matumizi/ gharama huandikwa kwenye kitabu kikuu cha mahesabu pale biashara inapoingia gharama hizo, na sio kusubiria hadi zitakapolipwa. Hali kadhalika, mapato hutambulika na kuingizwa kwenye vitabu pale biashara inapoyapata, na sio kusubiria hadi fedha hizo zikusanywe.
 2. ii) Mfumi huu unajishughulisha na aina zote za miamala.

iii) Mfumo huu hupelekea kuwa na taarifa sahihi ya mali na madeni ya biashara.

Kumbukumbu katika mfumo huu huwa na jedwali la mapato na matumizi, ambalo hujumuisha mapato na matumizi yote yaliyofanyika kwa kipindi fulani, pamoja na taarifa ya hali ya kifedha ambayo huonesha, licha ya mambo mengine, madeni inayodai na kudaiwa biashara katika siku ya mwisho ya kipindi hicho.

Mifano ya nyaraka muhimu zinazotunzwa ni:

 • Jedwali la fedha taslimu/ zilizoko benki
 • Vocha (Makusanyo, Malipo na kitabu cha kumbukumbu)
 • Rajisi ya malipo ya awali
 • Taarifa ya benki/ uoanisho wa taarifa ya benki na taarifa ya fedha taslimu

Jedwali la fedha taslimu

Hili ni jedwali linalotunza taarifa za miamala ya kifedha (malipo na makusanyo) yanayotokea katika biashara. Katika jedwali hili, makusanyo na malipo yanayofanyika na biashara huandikwa.

Jedwali hili hutumika kurekodi, kuainisha na kutoa muhtasari wa miamala ya fedha taslimu katika namna ambayo itamuwezesha yeyote anayehitaji taarifa za yaliyomo katika jedwali hilo kufanya maamuzi yenye kuzingatia taarifa. Jedwali hili likitunzwa vema, mtu anayelisoma atapata taarifa kuhusu salio la fedha taslimu lililokuwepo mwanzo wa kipindi, kiasi gani cha fedha taslimu kimeingia (makusanyo), kiasi gani cha fedha taslimu kimetoka (malipo) na salio la fedha taslimu mwishoni mwa kipindi husika

Kielelezo: Mfano wa ukurasa katika jedwali la fedha taslimu

Mapato ya fedha taslimu Matumizi ya fedha taslimu
Tarehe Kiasi kilichopokelewa Mteja Bidhaa alizouziwa Tarehe Kiasi kilicholipwa Muuzaji Bidhaa alizotuuzia
2.6.05 30,000 JC Stores Juisi ya nanasi
3.6.03 2,500 Mohammed stationery Karatasi
6.6.05 12,000 Star shop Mchanganyiko wa nyanya 6.6.03 5,000 Market Mifuko ya plastiki

Itaendelea wiki ijayo

Imeandaliwa na Veneranda Sumila

Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania

Mpango na Mchanganuo wa Biashara

Maana ya na umuhimu wa mchanganuo

Mchanganuo wa biashara ni andiko ambalo linaweka bayana malengo na madhumuni ya biashara na namna yatakavyofikiwa. Ni mpangilio maalum wa kuongoza utekelezaji wa kufanikisha lengo la biashara.

Kuandaa mpango wa biashara ni muhimu kwa mafanikio ya biashara yoyote. Mchanganuo wa biashara hutoa dira na kusaidia kuongoza uendeshaji wa biashara. Mara nyingi ni sharti mojawapo katika kuomba mkopo.

Mpango wa biashara ulioandaliwa vizuri utatoa majibu ya maswali mbali mbali kama vile nini madhumuni ya biashara yako, Utamwuzia nani/akina nani? Ni yapi malengo yako ya mwisho? Utagharimia vipi biashara yako? na mengine mengi

Mpango wako wa biashara utakusaidia kutafakari mwelekeo wa kampuni yako na namna ambavyo itakabiliana na changamoto mbalimbali ili iwe endelevu.

Vipengele muhimu vya Mchanganuo wa Biashara

Vipengele muhimu vya Mchanganuo wa Biashara ni kama vifuatavyo:-

 1. Ufupisho

Kipengele hiki huandikwa mwishoni. Andika katika kipengele hiki mambo ambayo ungeandika kama ungeambiwa uelezee biashara yako kwa dakika tano katika usaili. Iandike kitaalamu, kiukamilifu, kwa usahihi, na kuonesha hali ya juu ya kujiamini.

Elezea mambo ya msingi kuhusu biashara: Bidhaa yako ni nini? Wateja wako ni kina nani? Wamiliki ni kina nani? Unafikiri nini kuhusu mustakabali wa biashara yako na tasnia yake kwa ujumla?

Ikiwa unaomba mkopo, eleza ni kiasi gani unahitaji, fafanua kiasi hicho kitatumikaje, na namna kitakavyosaidia katika kuboresha biashara yako.

Muhtasari ni lazima uwe ni jumuisho la vitu vifwatavyo:

 • Mpango wa biashara unahusu nini
 • Bidhaa au huduma inayoletwa na umuhimu wake
 • Upatikanaji wa masoko
 • Mpangilio wa uongozi
 • Matarajio ya kifedha
 • Fedha zina hozohitajika na mapato yake
 1. Maelezo ya Biashara

Unaingia kwenye biashara gani? Utafanya nini? Kwa kifupi, wateja wako ni akina nani? Taja ni wapi eneo lako la biashara na saa za kazi ni zipi.

Biashara itakuwa katika muundo upi wa umiliki kisheria: Mfanyabiashara pekee, ubia, shirika, kampuni yenye ukomo wa madeni? Kwa nini umechagua muundo huo?

Wamiliki wakubwa wa biashara ni kina nani? Elezea sifa zao kwa kifupi.

Malengo ya kampuni: Unatarajia kampuni yako iwe katika hatua gani ndani ya mwaka wa kwanza? Na baada ya miaka 3-5. 

Falsafa ya Biashara: Ni jambo gani muhimu kwako katika biashara? Mambo gani yatasaidia kampuni kufanikiwa?

Una uwezo mzuri katika Nyanja zipi za kiushindani? Kundi gani katika soko unalenga kulitumia kufanikisha kuingia sokoni.

Maelezo juu ya uzalishaji (kama upo) na mahitaji

 1. Utawala na uendeshaji (kurasa 1-2)

Taja jina la biashara, muundo wa kisheria na umiliki:  Mfano “ ABC ni ni biashara inayoendeshwa na mmiliki mmoja pekee na inamilikiwa na Jane Success.” 

Elezea kwa kifupi kuhusu mmiliki na sifa zinazomuwezesha kuendesha biashara hiyo. Ambatanisha wasifu wa kila mmiliki.

Nani atafanya kazi ipi? Kama utafanya mwenyewe kila kitu, elezea namna utakavyofanya shughuli za ununuzi, masoko, utunzaji wa mahesabu, wateja, mali, ukarabati, n.k.

Utakuwa na waajiriwa? Watafanya kazi gani? Watahitaji kuwa na sifa gani? Utawalipa kiasi gani? Kuna mpango wowote wa mafunzo?

Utatumia wataalamu kutoka nje au wanafamilia kusaidia uendeshaji? Onesha iwapo watakuwepo wahasibu, watunza kumbukumbu za fedha, wanasheria, n.k. Elezea wanafamilia watachukua majukumu gani katika biashara.

Biashara yako inahitaji leseni maalum, au inabanwa na sheria/ kanuni/ makubaliano maalum? Eneo ilipo biashara ni sahihi kisheria kwa ajili ya uuzaji au uzalishaji unaofanyika? Una bima ipi katika biashara yako?

Bainisha wauzaji wako wakuu. Una wauzaji wengine wa kutegemea ikiwa ulionao watashindwa kukuuzia?

Utauza kwa mkopo? Utaweka vigezo na masharti gani kwa wateja wanaokopa bidhaa/ huduma? Utapimaje uaminifu wa mteja mpya?

 1. Masoko

Katika kipengele cha masoko unatakiwa uelezee mambo kadha wa kadha kama ilivyobainishwa hapa chini.

 1. Picha ya jumla ya sekta

Unafahamu kiasi gani kuhusu sekta ya biashara yako? Biashara inakua kwenye hiyo sekta? Kuna mabadiliko gani yanayoendelea? Soko likoje katika eneo unapopanga kuendesha biashara yako?

 1. Soko unalolenga

Elezea soko la msingi unalolenga katika biashara yako. Hawa ndio wateja wako muhimu kuliko wote. Chambua wateja wako kwa vigezo kama umri, jinsia, kipato. Wateja wako wako maeneo gani? Wateja wengine unaowalenga ni wapi?

 1. Ushindani

Orodhesha washindani watatu wakubwa ambao unashindana nao moja kwa moja (wanaofanya biashara inayofanana na ya kwako).

Watashindana nawe katika kila kitu au katika baadhi tu ya bidhaa, wateja au maeneo?

Wana nguvu gani ya ziada kukuzidi? Na utakabiliana vipi na hali hizo?

Wana madhaifu gani? Na utatumiaje madhaifu yao kwa faida yako?

Unalenga kundi gani katika soko? (Usijaribu kutaka kufanya kila kitu kwa kila mteja)

 1. Bidhaa/Huduma

Elezea kwa kirefu huduma unayotoa au bidhaa unazouza.

 1. Kuvutia wateja/Kutangaza biashara

Utawafikishia vipi wateja ujumbe? (elezea iwapo utatumia matangazo ya maandishi/ picha, maonesho ya biashara, wavuti, vipeperushi, kadikazi, mawasiliano ya barua, mitandao mbalimbali, ya kijamii, n.k). Kadiria gharama na tarehe, idadi ya matangazo, n.k.

 1. Kupanga bei

Umefanyaje maamuzi kuhusu bei? Bei zako zinaendana na soko? Bei zako zikoje ukilinganisha na za washindani wako?

 1. Eneo la biashara

Unafanyia wapi biashara yako? Nyumbani? Ofisini, au dukani? Eleze sababu za uchaguzi wake. Ikiwa bado hujafikiria au hujafanya maamuzi, elezea unatafuta eneo la namna gani.

 1. Mipango ya kifedha

Katika kipengele hiki, elezea masuala mbali mbali ya kifendha ikijumuisha

 1. Taswira yako binafsi ya kifedha, Makadirio/ matarajio ya kifedha         , kwa ajili ya mashine, vifaa, ofisi, n.k.
 2. Gharama za kuanzia na vyanzo vya fedha: mfano wa vyanzo vya fedha ni akiba yako mwenyewe, marafiki, wawekezaji, mikopo, n.k.
 3. Matumizi ya fedha na dhamana
 4. Taarifa ya mapato, na taarifa ya hali ya kifedha (faida na hasara).
 5. Mtiririko wa fedha taslimu (kiasi kinachoingia na kutoka katika biashara kwa kipindi fulani – mwezi)),

Viambatanisho:

 • Matarajio ya kifedha ya kina kwa mwezi
 • Wasifu wa wafanyakazi wa muhimu
 • Taarifa za utafiti wa masoko
 • Mpangilio wa uongozi

Kwa maelezo zaidi:

Imeandaliwa na Veneranda Sumila

Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania