Kupanga bei na kukadiria gharama

Kupanga bei na kukadiria gharama

Katika hili hakuna kanuni imara sana, wala hakuna namna moja tu bora ya kupanga bei, ila viko viashiria mbalimbali ambavyo vinaweza kusaidia. Ni suala tu la kugundua bei ipi inayofaa kwa kuzingatia kwa uangalifu vigezo mbalimbali.

Kupanga bei ni suala muhimu sana katika maamuzi ya masuala ya masoko. Bei unayotoza kwa bidhaa/ huduma yako inaathiri moja kwa moja faida (au hasara) utakayopata.

Pamoja na umuhimu wote huo wa kupanga bei kwa umakini, uko ushahidi kuwa wajasiriamali wengi hawatilii mkazo suala la upangaji wa bei. Matatizo yanayotokana na kutokuwa makini katika kupanga bei ni kuwa na faida ndogo katika baadhi ya bidhaa, hasara katika uuzaji wa bidhaa hizo kutokana na kuongezeka kwa gharama, na kushindwa kupanga bei upya. Mbaya zaidi, upangaji bei usio makini unaweza kutofautisha kati ya kupata faida au kupata hasara.

Mambo ambayo yanaathiri bei zako yanaweza kugawanywa katika makundi manne yafuatayo:

  • Gharama zako
  • Mkakati wako wa masoko
  • Udhibiti wa bei
  • Hali ya soko

Ni dhahiri kuwa bei utakayopanga itapaswa kufidia gharama zote za kuendesha biashara yako.

Kufahamu gharama zako

Gharama za kuendesha biashara zinaathiri kwa kiwango kikubwa bei utakayotoza kwa hiyo bidhaa. Ikiwa utaweza kufahamu gharama zote zilizotumika katika kuzalisha bidhaa hiyo, utakuwa kwenye nafasi nzuri sana ya kutoza bei yenye uhalisia. Hata hivyo, si jambo rahisi sana kukokotoa kwa usahihi kiasi cha gharama za bidhaa iliyozalishwa.

Ni rahisi kufahamu kiasi cha malighafi iliyotumika na gharama yake, au gharama uliyonunulia bidhaa unayouza, lakini bado linabaki suala la gharama nyinginezo. Gharama kama vile za mishahara ya wafanyakazi, Kodi ya jengo, Umeme, maji na nyinhgine nyingi lazima kuzingatia wakati wa kupanga bei.

Aina za gharama

Ili kuweza kuweka makadirio ya gharama katika hatua mbalimbali za uzalishaji tunahitaji kuelewa tabia za gharama mbalimbali kuendana na kiwango/ kiasi cha uendeshaji biashara. Kuwa iwapo biashara itakuwa kubwa gharama hizo zitaongezeka, zitapungua, au hazitabadilika. Kwa kuzingatia tabia ya gharama kuendana na kiwango cha biashara, tuna gharama zisizobadilika na gharama zinazobadilika,

Gharama zisizobadilika: hizi ni zile ambazo hazibadiliki hata kama mjasiriamali atazalisha bidhaa nyingi kwa pamoja. Gharama hizi ni lazima zilipwe kwa kiwango kile kile bila kuzingatia mabadiliko yoyote katika kiwango/idadi cha uzalishaji, yaani hamna tofauti ya gharama hizi katika kuzalisha bidhaa moja au kuzalisha bidhaa 1000.

Mifano ni kama Kodi (pango), uchakavu, riba, na bima

Gharama zinazobadilika kutegemeana na kiwango cha uzalishaji/mauzo. Hizi ni zile ambazo ukiongeza uzalishaji kufikia idadi ya vitu 1000 na gharama za uzalishaji zitaongezeka kuwa mara mbili ya ulizotumia wakati ukitengeneza vitu 500.

Mifano  ni kama bei ya manunuzi, gharama za malighafi na ujira wa wafanyakazi walioko katika uzalishaji.

Kuzitambua gharama

Hatua ya kwanza katika kukokotoa gharama ni kutambua aina za gharama mbalimbali zilizochangia katika uzalishaji wa bidhaa , au bidhaa iliyouzwa, au huduma iliyotolewa. Ili ufanye hivyo, ni vema kuainisha gharama katika gharama za moja kwa moja na gharama zisizo za moja kwa moja

Gharama za moja kwa moja ni gharama ambazo ni rahisi kufuatiliwa kuona mchango wake katika bidhaa au shughuli fulani. Mifano ni kama bei ya kununulia bidhaa, gharama za vibarua, gharama za malighafi. Mara nyingi gharama hizi hubadilika kadri ya kiwango/kiasi cha uzalishaji, mauzo, au huduma zinazotolewa. Gharama za moja kwa moja zimegawanyika katika gharama moja kwa moja za malighafi na gharama moja kwa moja za ujira.

Gharama zisizo za moja kwa moja Hizi ni gharama ambazo haiwezekani kufuatilia na kujua mchango wake moja kwa moja katika uzalishaji wa bidhaa fulani.

Mifano ni pamoja na gharama za kifedha, matangazo, utawala.

Gharama zisizo za moja kwa moja haziwezi kuonekana/ kuhusishwa moja kwa moja na bidhaa inayozalishwa au kuuzwa, au huduma inayotolewa. Mara nyingi hazibadiliki kuendana na kiwango cha uzalishaji/ mauzo. Badala yake, kiasi cha gharama hizi huwa kile kile kwa kila kipindi husika. Gharama hizi zimegawanyika katika gharama za mauzo, za kifedha, na za kiutawala.

Baadhi ya mifano ya gharama zisizo za moja kwa moja kwa biashara ndogo ni kama:

  • Kodi (pango)
  • Mishahara
  • Riba
  • Gharama za matumizi mbalimbali ya ofisi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *