Taarifa Kuhusu Ushauri wa Utaalamu wa Kisheria

sheria

Kujua ujuzi wa kisheria ni muhimu katika uendeshaji wa biashara yoyote

Ujuzi na utaalam wa kisheria kwa mjasiliamali ni njia mojawapo inayosaidia biashara kujiendesha kwa ufanisi.

Inashauriwa kuwa asasi ya kibiashara ikodishe mtaalamu mahsusi katika masuala ya sheria ili kusaidia biashara yake kujiendesha kwa mujibu wa sheria. Masuala ya kisheria katika uendeshaji wa biashara yanayoweza kushughulikiwa na wataalamu wa sheria ni haya yafuatayo:

Kutetea jina la biashara, mawazo, uvumbuzi na usajili wake. Kuandaa, kutathmini na kusimamia mikataba ya biashara. Kuwa katika mstari wa mbele katika mijadala ya mikataba ya kiabiashara na Kusaidia mchakato wa kupata mali za biashara kwa ujumla.

Taratibu za kupata msaada wa kisheria katika biashara

 • Ili kubaini shughuli za kisheria na huduma zitolewazo si budi mjasiliamali akafanya utafiti kujua wanasheria waliopo/na utaalamu wao

Masuala ya kuzingatia ili kubaini wataalamu wa sheria

  1. Lazima awe muhitimu katika taaluma ya sheria na amesajiliwa katika chombo cha wataalaam wa sheria;

  2. Lazima abainishe majukumu atakayotaka kutekeleza; na

  3. Shurti akubaliane na mpango wa malipo ambao hautaharibu fedha za kuendeshea biashara.

  • Ni budi kujadili masuala muhimu na gharama zinazohusika

  • Ni budi kusaini mkataba baada ya pande zote kuridhika na majadiliano kuhusu masuala na hali ya kazi husika

   

Kwa nini ni muhimu kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati kufuata Sheria?

Sheria ni mkusanyiko wa amri za kudhibiti mahusiano kati ya watu na makundi ya watu katika jamii. Kwa hiyo, kwa ujumla kufuata sheria ni muhimu katika jamii yoyote. Katika biashara, pengine ni muhimu zaidi kuzingatia sheria. Uzingatiaji kama huo unahakikisha kwamba biashara ipo kisheria, na inaingia katika mahusiano yanayotambulika kisheria, yanayotekelezeka na kuendeshwa kulingana na sheria za nchi.

Zifuatazo ni baadhi ya sheria za Tanzania zinazoongoza Wajasiriamali Wadogo na wa Kati:

 1. Sheria ya Makampuni ya mwaka 2002

Baada ya kusajili, kampuni inapata uwepo huru wa kisheria unaodhibitiwa na sheria unaolazimisha matakwa kadhaa ambayo ni lazima yazingatiwe na maofisa wa kampuni. Yafuatayo ni baadhi ya matakwa ya kuzingatiwa na kampuni iliyosajiliwa na maofisa wake:

  1. Kuwasilisha mapato ya kila mwaka yanayohusu maelezo yote muhimu ya kampuni hiyo, ikiwa ni pamoja na maelezo juu ya hisa, uongozi, amana na gharama zingine;

  2. Kuwasilisha mahesabu yaliyokaguliwa;

  3. Kuwasilisha mabadiliko yoyote ya taarifa za kampuni kama vile jina la kampuni, malengo na madhumuni ya kampuni, Bodi ya Wakurugenzi, mtaji wa kampuni, madaraja ya hisa, anwani ya ofisi iliyosajiliwa, uteuzi wa wapokeaji, mameneja, maafisa utawala pamoja na taratibu za kufunga shughuli; na

  4. Malipo ya kodi mbali mbali za serikali kuu na serikali za mitaa.

Kampuni na maafisa wake wasipozingatia matakwa ya sheria na kanuni zilizotajwa hapo juu wataadhibiwa kwa njia ya faini ya fedha na wakati mwingine wanaweza kupata mashitaka ya jinai. Uzingatiaji utaipa kampuni uaminifu, utaipa sifa ya kukopesheka kama hali hiyo itajitokeza na kwa ujumla utaipa kampuni msimamo mzuri katika nyanja za kibiashara na kijamii.

 1. Sheria ya Mikataba

Makampuni yanatakiwa kuzingatia masuala na matakwa ya mikataba iliyofungamana nayo. Endapo matakwa ya kisheria hayatazingatiwa mkataba waweza kuwa batili au kubatilishwa kutegemeana na matokeo ya kisheria mahsusi kwa kosa litakalohusika. Kwa hiyo, ni muhimu kuhakikisha kwamba mikataba ya kisheria inayoingiwa na kampuni inatekelezeka kwa kuzingatia matakwa yote ya kisheria. Kunaweza kuwa na haja ya kupata ushauri wa kisheria kabla ili kuhakikisha kwamba biashara itaendeshwa kulingana na sheria ya mikataba.

 1. Sheria ya kazi

Biashara yoyote inatekelezwa kwa msaada wa watu ambao si wamiliki wa biashara lakini ambao ni wafanyakazi wa kulipwa mishahara kwa huduma zao. Sheri za kazi zinaongoza mahusiano kati ya biashara (kama mwajiri) na wafanyakazi wake (kama waajiriwa). Kampuni pia hutengeneza taratibu za kushughulika na mizozo na usuluhishi wake na masuala ya kustaafu pamoja na mafao ya wafanyakazi. Uhusiano chanya wa kikazi ni suala muhimu katika asasi ya aina yoyote.

 1. Sheria ya Leseni

Kufanya biashara kunahusisha uzingatiaji wa sheria. Kutegemea na aina ya biashara, sheria imeweka mahitaji mahsusi chini ya Sheria ya Leseni za Biashara Sura ya 208. Sheria hiyo inazuia kufanya biashara bila leseni ya biashara. Kila leseni ya biashara inatolewa kwa ajili ya biashara husika na katika eneo husika, labda kama kuna eneo maalumu la biashara ambapo leseni ya biashara tanzu hutolewa au kama hakuna ada ya biashara inayoelezwa kulingana na biashara husika. Mamlaka za leseni zina uwezo wa kufunga maeneo ya biashara zinazoendeshwa bila leseni. Kwa kufanya hivyo, mamlaka yaweza kuomba msaada wa polisi au mamlaka nyingine iliyoidhinishwa.

 1. Sheria ya Ardhi

Sheria kuu ya ardhi nchini Tanzania ni Sheria ya Ardhi Sura 113. Hii ni sheria ya msingi kulingana na aina za ardhi nchini Tanzania, licha ya kusimamia moja kwa moja ardhi ya kijiji pia inaongoza uendeshaji wa ardhi na usuluhishi unaoendana na matatizo ya ardhi. Biashara yoyote lazima iwe na eneo. Kwa sababu hiyo, biashara yaweza miliki ardhi yake au mali au kukodisha sehemu toka kwa mmiliki. Ardhi yaweza tumika kutunisha mtaji kwa njia ya amana, na ardhi hiyo kuwa kama dhamana ya mkopo. Sheria inaruhusu uanzishwaji, usajili na utekelezaji wa mipango hiyo.

 1. Sheria ya Hakimiliki

Sheria hii imependekezwa kwa malengo ya kulinda/kutetea haki mbali mbali na matumizi ya uvumbuzi wa kiteknolojia, bidhaa au huduma. Uvumbuzi unatakiwa kusajiliwa katika Ofisi ya Msajili wa Leseni. Sheria pia inatoa haki ya umiliki na matumizi kwa mvumbuzi halisi na inatoa maelekezo kwa mtu yeyote atakayependa kutumia uvumbuzi huo kulingana na makubaliano yatakayofanyika na mvumbuzi halisi wa ujuzi au huduma husika.

 1. Sheria ya Bima

Sheria hii inaelekeza taratibu za bima kwenye biashara na kuweka miongozo na taratibu zinazoongoza makubaliano ya bima kati ya wafanyabiashara ya bima na wafanyabiashara wanaotaka kuwekea bima biashara zao. Kuna aina tofauti tofauti za bima kama vile Bima ya moto, bima ya wizi, bima ya magari na bima ya fidia kwa kazi ni baadhi ya madhara yanayohusiana na biashara.

 1. Sheria ya Mirathi

Lengo kuu la sheria hii ni kutoa utaratibu wa kusimamia mali za marehemu baada ya kifo chake ikiwamo kuhamisha umiliki wa mali hizo kutoka kwa marehemu kwenda kwa watu wenye haki ya kuzipata mali hizo.Nia hasa ni kwamba mali alizoacha marehemu zisibaki zikiharibika na kupotea bure,au warithi halali au watu wenye maslahi na mali za marehemu,kwa mfano wale wanaomdai hawapotezi haki hiyo, bali awepo mtu ambaye atazisimamia na kuzigawa kwa wahusika wakiwamo wadai na kuepusha mgongano katika jamii husika.Hivyo sheria inamuweka msimamizi wa kugawa mirathi husika na mamlaka yake.

 

ULINZI WA KISHERIA NA MIONGOZO KWA WAJASIRIAMALI WADOGO NA WA KATI:

Zifuatazo ni Sheria na Miongozo inayowalinda Wajasiriamali Wadogo na wa Kati:

Sera
 • Sera ya Kuzuia Rushwa
 • Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Ushirika
 • Sera ya Taifa ya Ukimwi
 • Sera ya Taifa ya Teknohama
 • Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Uwekezaji
 • Sera ya Taifa ya Umwagiliaji
 • Sera ya Taifa ya Uhifadhi Nyuki
 • Sera ya Taifa ya Uhifadhi Mazingira
 • Sera ya Taifa ya Misitu
 • Sera ya Taifa ya Ardhi
 • Sera ya Taifa ya Fedha (Micro-Finance)
 • Sera ya Taifa ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati
 • Sera ya Taifa ya Nishati
 • Sera ya Taifa ya Chakula na Lishe
 • Sera ya Taifa ya Madini
 • Sera ya Taifa ya Utalii
 • Sera ya Taifa ya Biashara
 • Sera ya Taifa ya Maliasili
 • Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Wanawake
 • Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii
 • Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Jamii
 • Sera ya Endelevu ya Maendeleo ya Viwanda
Sheria na Kanuni
 • Sheria ya Kuzuia Kutupa Taka Ovyo ya 2004
 • Sheria ya Benki Kuu ya 2004
 • Sheria ya Benki ya 2004
 • Sheria ya Usajili wa Biashara ya 2007
 • Sheria ya Mikataba
 • Sheria ya Maziwa ya 2004
 • Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya 2004
 • Sheria ya Uwezeshaji ya 2004
 • Sheria ya Mchakato wa Kusafirisha Bidhaa Nje ya 2006
 • Sheria ya Fedha ya 2003
 • Sheria ya Kodi ya Mapato ya 2004
 • Sheria ya Bima
 • Sheria ya Hakimiliki
 • Sheria ya Uwekezaji ya 1997
 • Mabadiliko ya Sheria ya Ardhi ya 2004
 • Sheria ya Kazi
 • Sheria ya Mirathi
 • Sheria ya Leseni
 • Sheria ya Dhamana ya Mikopo ya 2003
 • Sheria ya Bandari ya 2004
 • Sheria ya Ushindani wa Haki ya 2003
 • Sheria ya Fedha ya 2006