Utafutaji wa masoko kwa wajasiliamali

Soko ni mahali au eneo ambapo wanunuzi na wauzaji hukutana ili kubadilishana bidhaa na huduma. Hatahivyo, kwa upande wa maendeleo ya biashara soko huelezewa kama wale watu au wateja ambapo wauzaji / wajasiriamali hutarajia kuuza na kununua bidhaa au huduma zao.

Utafutaji wa masoko kwa Wajasiriamali ni muhimu kwa sababu

• Ni moja ya njia bora za kushikilia wateja wa zamani na kuvutia wateja wapya
Utafutaji wa masoko kwa bidhaa na huduma ni muhimu sana kwa sababu huwa na mchango mkubwa katika kushikilia wateja ulio nao na kuvutia wateja wapya kwenye biashara yoyote. Matumizi ya njia mbali mbali za kutafuta masoko zilizopo yanasaidia kufanya bidhaa/huduma unazaofanya kujulikana zaidi na wateja wa kila siku, na vile vile kuvutia wateja wapya kuanza kutumia bidhaa au huduma husika.

• Ni njia nzuri ya kutangaza bidhaa na huduma zinazopatikana / zinazotolewa katika biashara

Utafutaji wa masoko hutoa fursa ya kuifanya bidhaa au huduma unayotoa ionekane na kutambulika kwa wateja waliokusudiwa na hivyo kuongeza uelewa wao kwa bidhaa husika. Hii ni muhimu kwa sababu kabla wateja hawajaanza kutumia bidhaa au huduma zako wanahitaji kufahamu uwepo wa bidhaa au huduma yenyewe, kwa hiyo ni muhimu kutafuta masoko kwa maendeleo ya biashara husika.

• Huongeza ukuaji wa pato la biashara
Lengo kuu la utafutaji masoko kwa ajili ya biashara ni kuongeza jumla ya wateja wanaotumia huduma au bidhaa za biashara husika. Kama idadi ya watumiaji bidhaa inaongezeka, itasababisha na pato la biashara pia kuongezeka. Kwa mtazamo huo, utafutaji wa masoko ukifanyika sawia husababisha kuongezeka kwa mapato na ukuaji wa biashara kwa ujumla

Njia zinazopendekezwa kuongeza ubora wa huduma/bidhaa zako:

Kuzingatia Ubora wa bidhaa/huduma

Bila shaka njia bora na sahihi ya kupata masoko kwa bidhaa au huduma husika huwa ni ubora wa huduma au bidhaa husika inayotolewa. Kabla ya kufikiria njia za gharama kubwa za kutangaza bidhaa au huduma fulani, ni lazima mjasiriamali ahakikishe bidhaa au huduma yake ipo katika ubora unaokubalika. Hii inafanyika kwa kuhakisha kiwango cha huduma au bidhaa zinazozalishwa ziko katika viwango bora kuliko bidhaa za washindani wanaotoa huduma au bidhaa zinazofanana na anazotoa mjasiriamali husika.

Njia zinazopendekezwa kuongeza ubora wa huduma/bidhaa zako:

i) Tambua aina ya wateja wako na mahitaji yao, jitahidi kuwafahamu wateja wako kwa kadri ya unavyoweza, mfano kufahamu wanatokea wapi, ni akina nani, na wanategemea aina gani ya huduma au bidhaa kutoka kwako? Hili ni muhimu kwa sababu wateja wanatofautiana kulingana na mazingira wanayotokea na uzoefu mbali mbali walio nayo. 

ii) Toa huduma na bidhaa zenye viwango, Hii inajumuisha kujiuliza maswali kama- je unafahamu matarajio ya wateja wako kwa huduma/bidhaa unazotoa? Je unafahamu ni kwa namna gani wanakichukulia kile wanachokifurahia katika huduma/bidhaa unayotoa? Kama hufahamu unadhani ni faida au hasara kama utafanikiwa kuwapatia wanachofurahia. Unachokichukulia kama ubora kinaweza kisionekane ni ubora kwa wateja wako, jaribu kubuni njia ambayo wateja wako wataweza kuelezea hisia zao juu ya bidhaa/huduma zako na uwe mwenye kiu na hamu ya kuwasikiliza wateja wako.

iii) Sahihisha upotoshaji katika mategemeo ya wateja wako, wafanyakazi/ wasaidizi wako katika biashara ni lazima wawajibike katika kutambua matarajio ya wateja kwenye huduma/bidhaa mnazotoa katika biashara yako, pia wawe na uelewa na wenye uwezo wa kufanya maamuzi ili kufikia viwango vya utendaji unaotegemewa na wateja wenu.
Kuwapa wateja wako nafasi ya kuzungumza nao na kutoa maoni yao kwa kadri inavyowezekana, hii itakusaidia kupata maoni na taarifa juu ya huduma/bidhaa unazotoa kabla halijatokea suala la kukukatisha tamaa kuhusu ubora wa bidhaa zako.

iv) Imarisha uaminifu wa wateja kwa bidhaa/huduma zako, hii inahusisha majibu ya haraka endapo tu wateja watakuwa na malalamiko kuhusu huduma/bidhaa unazotoa. Utatuaji wa malalamiko ya wateja kwa haraka ni njia ya haraka zaidi ya kuongeza uaminifu kwa wateja juu ya huduma au bidhaa unazotoa katika biashara yako.

v) Ongeza kuridhisha wateja wako ili uendelee kuwashikilia, Kupata mrejesho juu ya uzoefu wa huduma/bidhaa unazotoa katika biashara yako kwa vipindi tofauti itakupa picha halisi ya biashara yako ilipofikia. Kwa kutumia njia tofauti tofauti kuwafanya wafanyakazi wako watambue wateja wenu wana maoni gani kuhusu bidhaa/huduma mnayotoa.

Matangazo

Matangazo ni njia ya kufanya wateja wapate kuona muonekano, ubora na utumiaji wa bidhaa na huduma husika. Katika kutafuta masoko na kutangaza biashara yako unahitaji kuwa na mpango wa kuhakisha wateja wanatambua huduma au bidhaa yako na kubadilisha mtazamo kutoka bidhaa na huduma walizozizoea na kuhamia katika bidhaa yako. Mpango mzuri wa matangazo huhusisha yafuatayo:

i. Yazingatie vitu nyeti, yaani yasiwe na mitazamo ya kingono au kuonyesha itikadi za kivyama au aina fulani ya kibaguzi
ii. Yawe yanavutia, yaani yana urahisi wa kumshawishi mtu kufuatilia kinachotangazwa
iii. Yaweze kufikia watu wengi ndani ya muda mfupi, mjasiriamali hapa anashauriwa kufahamu aina ya wateja wake anaowakusudia na njia ya matangazo wanayoifuatilia mara kwa mara kwa mfano: Radio au Luninga

Ufungaji wa bidhaa

Hii ni maalum kwa zike bidhaa zinazouzwa zikiwa katika mifuko au vifungio vya aina mbalimbali. Ni lazima mjasiriamali ahakikishe mfuko unaotumika kufungia bidhaa unavutia na kumshawishi mteja kutumia bidhaa kwa kuzingatia muonekano wake mzuri tu.

Makampuni yanayotoa huduma ya Vifungashio

Matangazo ya mara kwa mara (Promotions)

Mwisho, mtu anaweza kutumia matangazo michezoni au sehemu yoyote yenye mikusanyiko ya mara kwa mara kama njia ya kuongeza soko kwa bidhaa zinazotolewa au huduma. Hii hufuatana na aina mbalimbali za kutoa bidhaa za nyongeza au kupunguza bei halisi ya bidhaa.
Mbinu kama ya kuuza bidhaa kwa bei nafuu ili kuvutia wateja wapya waanze kuzitumia. Michezo hii inaweza kujumuisha mambo kama, “Nunua 5 upate moja ya bure” au “Pata bidhaa mbili kwa bei ya mmoja”, haya yote yanaweza kuwa kama njia ya kukuza na kuongeza wateja wanaotumia bidhaa yako.