Tathmini ya Utayari wa Kuuza Nje

Kigezo mojawapo cha muhimu kinachopaswa kuzingatiwa wakati wa kuanzisha biashara ya kuuza bidhaa nje ya nchi ni kujitathmin ikiwa upo tayari kuwekeza fedha zako, kuzifungasha na kuzisafirisha kwenda nje.

Uchunguzi wa kujitambua utayari

 1. Kujitambua: Jiulize kwa nini unataka kuuza nje
 2. Nguvukazi ya kukusaidia: Je wewe au mfanyakazi wako yeyote anaweza kuzungumza lugha ya kigeni? Je utakuwa na mtu katika ofisi yako atakayejikita muda wote kushughulikia mauzo ya nje?
 3. Uzalishaji na Uendeshaji: Je Kiwango cha uzalishaji wako ni kikubwa kuweza kukidhi mahitaji? Je tayari umeshaanza kuzalisha bidhaa za aina mbalimbali? Unapenda Ubunifu? Je ukotayari kuboresha bidhaa zako ziendane na mahitaji ya mahali fulani?
 4. Kujitangaza: Je uko tayari kutangaza bidhaa zako mwenyewe soko la nje? Je uko tayari kusafiri nje ya nchi kukutana na wateja wapya? Je uko tayari kujifunza mbinu mpya za kufungasha bidhaa, na kuchapisha vipeperushi vya kutangaza bidhaa zako?
 5. Fedha: Kuanzisha biashara ya kuuza bidhaa nje ya nchi kunamaanisha kuwekeza fedha kwa miaka kadhaa kabla ya kuanza kupata matokeo chanya. Je kampuni yako inauwezo wa kutosha kifedha?

Ukishajiuliza maswali hayo na ukapata majibu chanya basi wewe upo tayari kuuza bidhaa nje ya nchi. Hata hivyo kabla hujaanza kupeleka bidhaa zako nje unatakiwa kujua mambo haya hapa chini.

 1. Kujiandaa kupeleka bidhaa nje: Hapa unahitaji kujua vitu vifuatavyo
 • Gharama za usajili wa bidhaa zako
 • Mchakato wa benki, kama unahitaji kukopa
 • Kusajili bima

Hadi kukamilisha mchakato huu unahitaji angalau siku 60

2. Kuelewa vya kutosha soko unalopeleka bidhaa

 • Fanya utafiti wa masoko
 • Tembelea ofisi mbalimbali
 • Kusafiri (Kama itabidi)

Mchakato huu utakuchukua hadi siku 30

3. Kupata hati stahiki

 • TFDA
 • TBS
 • Ukaguzi wa bidhaa za mazao ya mimea n.k

Hii itakuchukua hadi siku 90

4. Kukamilisha vibali na kupata ruhusa stahiki ya kuuza nje

 • Kufungasha
 • Usafirishaji
 • Kuweka lebo
 • Wakala wa kupitisha mizigo

Itakuchukua hadi siku 90

TARATIBU NA NYARAKA ZA KUUZA NJE

Taratibu na Nyaraka za Jumla

Kwa mujibu wa TRA, bidhaa za kuuza nje hazitozwi kodi na ushuru isipokuwa kwa bidhaa mbili:

Ngozi chepe za wanyama ambazo hutozwa ushuru wa Sh600 kwa kilo.

Korosho ghafi ambazo hutozwa dola za marekani 160 kwa tani moja ya mraba.

Mchakato

Muuzaji nje hulazimika kumteua wakala wa kupokea na kusafirisha mizigo (CFA) kushughulikia nyaraka zake za kutoa na kuingiza mzigo.

Utaratibu wa kushughulikia nyaraka hufanyika kwa njia ya mtandao na hukamilika kabla ya ukaguzi wa mizigo na kutoa kibali cha kusafirisha bidhaa nje ya nchi.

Mchakato wa awali huanza kwa msafirishaji mizigo nje kumteua wakala

Msafirishaji mizigo nje anakabidhi nyaraka zote ama kwa mkono au kwa njia ya kielektroniki kwa wakala ambaye naye huzipakia kwenye mtandao wa mfumo wa pamoja wa Forodha Tanzania  (TANCIS) pamoja na viambatanisho vyote ikiwemo vibali kutoka idara nyingine za serikali kwenda TRA. Idara nyingine za serikali zinahakiki kibali kama kipo (System inakataa ama kudhibitisha)

Tathmini ya kodi na ushuru wa kuuza bidhaa nje ya nchi kama upo

Wakala hufanya utaratibu wa kushikilia nafasi ya kontena kwenye meli au kwa wakala wa usafirishaji

Upakiaji wa mzigo wa kusafirishwa nje kwenye kontena hufanyika chini ya uangalizi wa TRA na idara nyingine za serikali

Mwenye meli au wakala wa usafirishaji huwasilisha TRA taarifa za ratiba ya chombo kinachosafirisha bidhaa nje.

Ukaguzi wa TRA (Unadhibitisha au kukataa) tamko la kupakia mzigo. Tamko lililokubaliwa moja kwa moja hupelekwa kwa muongoza mitambo kama orodha ya kupakia Mzigo, na hatimaye mzigo unasubiri kupakiwa kwenye chombo.

Ukaguzi wa kuingia getini kwa kuzingatia taratibu stahiki za ukaguzi wa geti la kituo

Getini wanawasilisha taarifa za kuingiza mzigo TRA kudhibitisha kuwasili kwa mzigo kituoni wa kusafirishwa nje.

Ripoti ya matokeo ya kupakia mzigo (mzigo wa kawaida/pungufu juliopakiwa)

Nyaraka zinazohitajika

 • Nyaraka zifuatazo zitatolewa kwa ajili ya kusafirisha mzigo nje ya nchi
 • Ankara
 • Orodha ya kufungashia
 • Hati ya namba ya mlipakodi (TIN)
 • Barua ya kuidhinisha
 • Hati ya kusafirisha nje bidhaa kutoka mamlaka husika kutegemeana na aina ya mzigo utakaosafirishwa nje. Hati hizo ni pamoja na;
 1. Hati kutoka wizara ya kilimo
 2. Hati kutoka wizara ya nishati na madini
 3. Hati kutoka wizara ya utalii na maliasili

Usafirishaji wa bidhaa za chakula

Utoaji wa hati kwa ajili ya kusafirisha bidhaa nje bidhaa za vyakula kwa kawaida hufanyika pale inapohitajika au pale inapoombwa na msafirishaji bidhaa nje au nchi inayopokea bidhaa hizo. TFDA hutoa hati ya afya kwa ajili ya kuambatanishwa kwenye bidhaa za chakula zinazosafirishwa nje.

Makundi ya usafirishaji bidhaa nje

 1. wazalishaji wa chakula waliosajiliwa
 2. Kampuni/watu binafsi waliopewa kibali cha kusafirisha nje na TFDA

TFDA itatoa hati ya afya ikiwa imejiridhisha kuwa

 1. Chakula kimesajiliwa na kutengenezwa chini ya leseni ya biashara iliyotolewa na TFDA
 2. Kwa kampuni/watu binafsi wenye nia ya kusafirisha bidhaa nje, ukaguzi na uchukuaji wa sampuli ya mzigo utakaosafirishwa nje utafanywa na mkaguzi kabla ya kutolewa kwa hati ya afya ambapo sampuli za bidhaa husika zitafanyiwa vipimo kwa gharama za msafirishaji bidhaa nje
 3. Chakula husika hakikiuki kifungu chochote cha sheria ya chakula, dawa na vipodozi (TFDC Act) ya mwaka 2003, au kanuni za kuingiza chakula nchini au kukisafirisha nje ya nchi.

Vyakula ambavyo haviwezi kusafirishwa nje ya nchi

 1. Mzigo ambao awali uliingizwa kama msaada au kwa matumizi ya mafunzo/utafiti au kwa matumizi binafsi haupaswi kusafirishwa tena kwenda nje ya nchi.

Taratibu za kupata kibali cha kusafirisha nje/hati ya afya;

 1. Mtu yeyote mwenye nia ya kusafirisha chakula kwenda nje anapaswa kuwasilisha maombi yake ya kusafirisha bidhaa hizo kwenda nje kwa mkurugenzi mkuu, TFDA.
 2. Barua ya maombi inapaswa kutamka kituo/bandari ya kutolea bidhaa nchini na aina ya usafiri itakayotumika. Barua hiyo iambatane na ankara kifani inayoonyesha
 • Jina na anwani ya kampuni inayosafirisha bidhaa nje
 • Jina na anwani ya anayeingiza bidhaa hizo kwenye nchi inayokwenda
 • Kiasi na thamani ya bidhaa za chakula zitakazosafirishwa nje
 • Aina ya matini ya kufungashia
 • Jina la mtengenezaji
 • Nchi bidhaa zinapokwenda

Maombi yaambatane na ada ya kuyashughulikia kama ilivyoainishwa kwenye kanuni ya ada na tozo mbalimbali ya mwaka 2011. Baada ya ukaguzi wa nyaraka na kuridhishwa na taarifa zilizowasilishwa, hati ya afya/kibali cha kusafirisha bidhaa nje hutolewa kwa msafirishaji. Kibali hicho kitakuwa na uhalali kwa muda wa miezi mitatu kuanzia tarehe ya siku kilipotolewa na kitatumika mara moja pekee.