Maonyesho ya biashara

Maonesho ya biashara ni maonesho yanayoandaliwa kwa ajili ya kampuni maalum au kutoka sekta mbalimbali ili kuonesha bidhaa au huduma zao. Kwa kiasi kikubwa, maonesho ya biashara ni ya muhimu kwa sababu hutoa fursa kwa wajasiriamali kuonesha bidhaa zao kwa watu mbalimbali katika muda mfupi

Umuhimu wa Maonesho ya biashara

Maonesho ya biashara kwa wajasiriamali yana faida zifuatazo:

• Kupata jukwaa la kuonesha bidhaa na huduma zao
Kwenye maonesho ya biashara, wajasiriamali hupata sehemu ya kuweka huduma au biashara zao kwa watu ili wapate kuziona. Hii hufanya maonesho ya biashara kuwa sehemu ya msingi ambapo wajasiriamali wanaweza kuweka biashara zao ziweze kuonekana.

• Kufanya uchambuzi wa washindani
Umuhimu mwingine ni kwamba wajasiriamali wanaweza kupata fursa ya kufanya uchambuzi wa soko. Kutokana na uwepo wa watu wengi wenye biashara sawa au zinazofanana, mjasiriamali anaweza kutumia muda huo kufanya uchambuzi wa watu wake kubaini mapungufu na uwezo wao ili ajue jinsi ya kupambana nao na kuboresha biashara yake kwa ujumla.

• Kupata fursa ya kulielewa soko
Licha ya kuwatambua washindani, mjasiriamali anapata fursa ya kulielewa soko pia. Kwenye hili, wakati wa maonesho ya biashara, mjasiriamali anaweza kulielewa soko kwa kujua mahitaji ya watu na mapendeleo yao ambao kwa pamoja husaidia katika kuboresha viwango vya huduma na bidhaa ambazo mjasiriamali anazitoa.

• Kupata nafasi ya kutambua/kuchambua fursa za kuwekeza
Kuhudhuria au kushiriki katika maonesho ya biashara kwa mjasiriamali humsaidia mjasiriamali nafasi mbalimbali zilizopo ili kuwekeza. Kwenye hili, mjasiriamali anaweza kupata fursa ya kukutana na wajasiriamali wengine ambao kwa pamoja huweza kujadili kuhusu upatikanaji wa fursa mbalimbali za uwekezaji.

Mambo ya kuzingatia wakati wa kutaka kuhudhuria/kushiriki katika maonesho ya biashara

• Aina ya maonesho
Kabla ya kushiriki kwenye maonesho ni lazima mjasiriamali ajue lengo zima la maonesho hayo. Kujua lengo la maonesho hayo kunasaidia katika kujua ni bidhaa gani au huduma zipi mjasiriamali anatakiwa kuzipeleka kwenye maonesho.

• Gharama za ushiriki
Kujua gharama za ushiriki ni jambo la msingi kwani humsaidia mjasiriamali katika kuchanganua faida zinazoweza kupatikana kutokana na ushiriki wake katika maonesho hayo. Pia husaidia kuepuka hasara inayoweza kupatikana kutokana na kushiriki katika maonesho hayo. Hivyo basi ni lazima kabla ya kushiriki katika maonesho, mtu ahakikishe kuwa ushiriki wake utakuwa na faida kwa biashara na siyo hasara.

• Sehemu ambayo maonesho hayo yatafanyika
Mwisho, ni lazima mjasiriamali ajue mapema sehemu maonesho hayo yatakapofanyika. Hili ni la msingi kwani mtu anahitaji kupanga miundombinu inayohitajika katika kuhakikisha kuwa bidhaa na huduma zinafika katika sehemu husika. Kujua eneo maonesho yatakapofanyikia hurahisisha zoezi zima la uandaaji mchakato wa kufikisha bidhaa zako katika eneo husika.

Orodha ya maonesho ambayo wajasiriamali wanaweza kushiriki:

• SIMA-SIPSA ALGÉRIE 2016 – Maonesho ya kimataifa ya biashara ya kilimo. Maonesho haya huonesha vitu kama vile mashine za kilimo, vyakula, afya, ufugaji wa wanyama na vifaa vya kufugia ng’ombe. Pia wanaonesha namna mbalimbali za uzalishaji wa mifugo. Maonesho haya yatafanyika kuanzia Oktoba 04 hadi 07, 2016 Algiers (Algeria – Africa – Mashariki ya Kati)

• SIPSA-AGRISIME & SIPSA-AGROFOOD: Maonesho ya kimataifa ya mifugo na mashine za kilimo. Maonesho haya hufanyika kila mwaka mara moja mjini Algiers, Algeria na kwa mwaka huu ni kuanzia tarehe 04 Oktoba hadi 07 Oktoba 2016

• MAGHREB PHARMA EXPO: Maonesho ya kimataifa ya wasambazaji wa vifaa vya famasia. Maonesho hufanyika nchini Algeria kila mwaka katika hoteli ya Hilton, Algiers ambapo kwa mwaka huu ni kuanzia tarehe 08 Novemba hadi 10 Novemba 2016

• ALGERIA FOODEXPO: Maonesho ya kimataifa ya vyakula, hoteli na bidhaa za kilimo, vifaa na mashine mbali mbali. Maonesho haya hufanyika mara moja kila mwaka katika mji wa Algiers, Algeria na mwaka huu ni kuanzia 23 Novemba hadi tarehe 26 Novemba 2016

• Maonesho ya Kilimanjaro ya utalii na viwanda yatakayofanyika tarehe 02 hadi 04. Juni 2017. Maonesho haya ni kwa ajili ya wataalamu wa fani hizi na jumuiya kwa ujumla. Yatafanyika katika viwanja vya gofu vya Moshi, Kilimanjaro

• Maonesho ya kilimo yanatarajiwa kufanyika mwezi Juni 2016 katika ukumbi wa Diamond Jubilee Dar es Salaam

• Maonesho ya kimataifa ya plastiki, uchapishaji na ufungashaji yatakayofanyika tarehe kuanzia tarehe 01 hadi 03 Desember 2016 katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City Dar es Salaam

• Maonesho ya kimataifa ya chakula na kilimo kwa ajili ya vyakula, hoteli, bidhaa za kilimo na mashine za aina mbalimbali yatakayofanyika kuanzia tarehe 25 hadi 27 Novemba 2016 katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City Dar es Salaam

• KILIFAIR- Maonesho ya viwanda na utalii ya Kilimanjaro yatakayofanyika kuanzia tarehe 03 hadi 05 Juni 2016 katika viwanja vya klabu ya gofu Moshi

• Agro & Poultry East Africa: Manonesho ya kimataifa ya kilimo, ufugaji na ufugaji wa kuku kuanzia tarehe 16 hadi 18 Mei 2016 katika ukumbi wa Diamond Jubilee Dar es Salaam

• Plast Print Pack Paper East Africa: Maonesho ya kimataifa ya plastiki, vifungashio na mashine za aina mbalimbali yatakayofanyika tarehe 16 hadi 18 Mei 2016 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee Dar es Salaam

• Food Hotel Kitchen East Africa: Maonesho ya kimataifa ya usindikaji vyakula na bidhaa za jikoni katika hoteli yatakayofanyika tarehe 16 hadi 18 Mei 2016 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee Dar es Salaam