MWONGOZO WA KUANZISHA BIASHARA

Baada ya kupata cheti cha namba ya utambulisho wa mlipakodi mwombaji atatakiwa kuomba leseni ya biashara kutoka ofisi za Biashara katika Wilaya, Manispaa, Jiji na Wizara ya Biashara na Viwanda kwa kutegemea aina ya biashara anayotaka kuanzisha.

Uchumi wa Tanzania umekuwa ukizalisha ajira chache kila siku. Hii imekuwa ikifanya vijana wengi wanaohitimu vyuoni kubaki wakizunguka na bahasha kila kona kusaka ajira.

Takwimu kutoka ofisi ya takwimu ya taifa zinaonyesha kuwa mwaka 2014 taifa lilizalisha nafasi za ajira 282,382 tu ukilinganisha na mahitaji ya zaidi ya wahitimu 400,000 wanaomaliza vyuo kila mwaka.

Hii inaonyesha dhahiri kuwa Tanzania kama nchi inahitaji kuweka nguvu za ziada katika kuhakikisha kuwa nafasi zaidi za ajira zinatengenezwa.

Pengine njia pekee inayoweza kutumiwa kupunguza tatizo hili au hata kulimaliza kabisa ni kupitia ajira binafsi (Ujasiriamali).

Pamoja na kuwa ujasiriamali unaweza kuwa suluhisho la ajira nchini, vijana wengi wameshindwa kabisa kufanya ujasiriamali kutokana na kukosa elimu sahihi. Kwa bahati mbaya sana mfumo wetu wa elimu haumsaidii sana muhitimu kupata stadi za ujasiriamali.

Katika vipaumbele vyake, Rais John Magufuli anasisitiza sana Tanzania ya viwanda, lakini hili litatokea tu kama vijana wa kitanzania watapatiwa elimu ya ujasiriamali.

Sehemu hii itakuwa ikiwapatia makala mbalimbali za ujasiriamali… tutajifunza jinsi ya kuanzisha biashara, jinsi ya kuendeleza biashara yako na namna ya kupata fedha.

Kabla ya kuanzisha biashara yako hakikisha una sifa zifuatazo:

Nidhamu binafsi – Hakuna mjasiriamali anayependa kuona biashara yake inakufa, kila mmoja analenga kuhakikisha biashara inafanikiwa na huondosha kila jambo linaloweza kuhatarisha ustawi wa biashara husika. Wajasiriamali waliofanikiwa wana nidhamu ya kuchukua hatua kila siku kuelekea kwenye kufanikisha malengo yao. Hakikisha unanidhamu ya kutunza mda na nidhamu ya kutumia pesa zinazopatikana kutokana na biashara yako.

Kujiamini – Mjasiriamali hupaswi kuwa na wasiwasi kuwa unaweza kufanikiwa au la, unapaswa kujiamini mda wote kuwa utafanikisha biashara yako. Jitahidi kudhihirisha kujiamini huko kwa kufanya kazi kwa bidii ili kifikia malengo uliyojiwekea.

Muwazi wa fikra – Mjasiriamali anatambua kuwa kila tukio au hali ni fursa ya kibiashara. Mawazo mapya yanaibuliwa kila mara kuhusu mtiririko wa kazi na ufanisi, ujuzi, na biashara mpya. Mjasiriamali ana uwezo wa kutizama kila jambo [hali/ tukio] linalomzunguka na kulitumia kufanikisha lengo lake.

Muanzilishi – Mjasiriamali anafahamu kuwa kama kuna jambo linalopaswa kufanyika basi yeye mwenyewe ndiye anayepaswa kulianzisha. Hujiwekea vigezo na kuhakikisha biashara inafuata kuelekea kutekeleza/ kukidhi vigezo hivyo. Wako makini katika kutwaa fursa bila kuhitaji kusubiri mtu mwingine awape fursa

Mshindani – Chanzo cha biashara nyingi ni mjasiriamali mmoja kutambua kuwa anaweza kufanya biashara hiyo kwa ubora kuliko mwingine/ wengine. Wajasiriamali wanahitaji kufanikiwa katika biashara wanazoanzisha mithili ya mchezaji anavyohitaji kushinda katika mchezo anaocheza. Mjasiriamali ni mwepesi kuonesha namna taasisi yake ilivyofanikiwa katika hatua mbalimbali.

Mbunifu – mojawapo ya mambo muhimu katika ubunifu ni kumudu kuunganisha mambo ambayo hayaonekani kuwa na uhusiano katika kutengeneza fursa. Wajasiriamali huja na suluhisho baada ya kuchambua na kutengeneza uhusiano wa hali/ matukio mbalimbali. Huweza hata kubadili malengo ya bidhaa fulani na kuiuza katika soko tofauti.

Kutokata tamaa – Wajasiriamali hawakatishwi tamaa na kushindwa. Kila anaposhidwa huichukulia kama fursa ya kujifunza na kufanikiwa. Wanatamani kila wanalofanya lifanikiwe, hivyo hujaribu tena na tena hadi wafanikiwe. Hawaamini kuwa kuna jambo lisilowezekana

Ujuzi binafsi – Mjasiriamali ana ujuzi mzuri wa kuwasiliana katika kuuza na kuwapa motisha waajiriwa wao. Wajasiriamali wengi waliofanikiwa hufahamu namna ya kuwapa motisha waajiriwa wao hivyo kukuza biashara zao. Ni wazuri katika kuelezea faida za hali mbalimbali na kuwafundisha wengine katika kufanikiwa.

Mwenye kuheshimu maadili ya kazi yake – Mjasiriamali hufanikiwa kwa kufuata/ kutii kanuni na taratibu zilizowekwa na mamlaka husika. Mifano ya wajasiriamali wasio na maadili ni: Muuzaji wa matunda anayeokota matunda kutoka kwenye shimo la taka kwa ajili ya kuwatengenezea wateja wake sharubati (juisi), au mjasiriamali anayeuza nyama isiyokaguliwa au iliyokatazwa kwa matumizi ya binadamu.

Mwenye kupenda kazi yake – Kupenda na kuthamini kazi yake ni sifa muhimu kuliko zote anayohitaji mjasiriamali ili kufanikiwa. Mjasiriamali ana mapenzi ya dhati kwa kazi yake. Yuko tayari kufanya kazi saa za ziadakuhakikisha biashara yake inafanikiwa, maana hupata furaha kuona biashara inafanikiwa. Mjasiriamali anayefanikiwa ni yule ambaye hujifunza bila kuchoka na kutafiti namna mbalimbali za kufanya biashara yake iwe bora zaidi.

Wajasiriamali wanaofanikiwa hutizama biashara zao kama mtu aliye juu ya kilima na kuona biashara yake ilivyo. Akishaiona, anataka kwenda mbali zaidi. Wanafahamu namna ya kuzungumza na waajiriwa wao, na biashara zao hutanuka kwa sababu hiyo.

Jinsi ya Kuanzisha Biashara Ndogo

Biashara yoyote huanza na wazo, ila wazo pekee halitoshi, linahitaji kufanyiwa kazi. Hapo ndipo watu wengi huweza kuanza kujisikia kuzidiwa. Si ajabu kuona mtu anakatishwa tamaa kwa kutizama msururu wa mambo yanayohitajika ili kuanzisha biashara, lakini pia kuanzisha biashara ni rahisi kuliko unavyodhani. Kama ilivyo katika lengo lolote kubwa, ukianza kwa kutengeneza malengo madogo madogo ya kutekeleza utaweza kufanya mambo yote muhimu katika kuanzisha biashara.

Jinsi ya Kuanzisha Biashara Ndogo

Kuanzisha na kuendesha biashara inahitaji msukumo, nia na kipaji. Inahitaji pia utafiti na mipango. Kama ilivyo kwenye mchezo wa drafti, mafanikio kwenye biashara ndogo huanza na maamuzi sahihi katika hatua za mwanzoni. Ikumbukwe pia hapa kuwa pamoja na kwamba makosa madogomadogo ya mwanzoni yanaweza yasiue biashara yako, inahitaji ujuzi, nidhamu, na bidii kuyasahihisha.

Ili kuboresha uwezekano wa kufanikiwa, unapaswa kutenga muda wa kujichunguza na kutathmini malengo yako kibiashara na malengo binafsi. Tumia taarifa hiyo kutengeneza kwa umakini mkubwa mpango wa biashara ambao utakuwezesha kufikia malengo yako.

Mchakato wa kuandaa mchanganuo wa biashara utakuchochea kufikiria hata baadhi ya mambo ambayo usingekumbuka kuyafikiria katika hali ya kawaida. Mchanganuo wako utakuwa zana muhimu sana unapopambana kutafuta fedha kwa ajili ya biashara yako. Mchanganuo huo pia unaweza kutumika kama kigezo cha kila mara kufuatilia/ kupima mafanikio ya biashara yako.

Yako mambo kadhaa yanayohitajika katika biashara yoyote.

Jambo la kwanza kabla ya kuanzisha biashara ni kuwa unatakiwa ujiulize sababu za wewe kutaka kuingia kwenye biashara. Sababu zilizozoeleka za kuanza biashara ni:

 • Unataka kujiongoza mwenyewe.
 • Unataka uhuru wa kifedha.
 • Unataka uhuru wa kutumia ubunifu wako.
 • Unataka kutumia kikamilifu ujuzi na ufahamu wako

Jambo la pili ni kuamua biashara ipi inakufaa? Ili kufahamu ni biashara ipi inakufaa, jiulize maswali yafuatayo:

 • Ninapenda kutumiaje muda wangu?
 • Nimejifunza au kusomea ujuzi gani?
 • Watu wengine wanazungumzia ubora wangu kwenye mambo gani?
 • Nina muda kiasi gani kuendesha biashara kwa ufanisi?
 • Katika mambo ninayopendelea yapo ambayo yanaweza yakawa fursa ya biashara?
 • Biashara yangu itahudumia sehemu/ kundi gani katika soko?
 • Je? Wazo langu linatekelezeka na litakidhi hitaji katika soko?
 • Ushindani nilionao ni upi? Nami nina uwezo gani katika ushindani?
 • Biashara yangu ina manufaa gani kuzidi zingine zilizopo?
 • Je? Naweza kutoa huduma zenye ubora zaidi?
 • Je? Naweza kutafuta soko kwa ajili ya bidhaa/ huduma zangu?

Ukishapata majibu ya maswali hayo hapo juu ni wazi kuwa utakuwa ulishaanza kujua ni biashara gani unaweza kuianzisha. Lakini pia unatakiwa ujiulize maswali haya hapa ili kuwa na uhakika na biashara ambayo utaifanya.

 • Ninakusudia kuanzisha Biashara gani?
 • Nitauza bidhaa gani au nitatoa huduma gani? Biashara nitafanyia eneo gani?
 • Nitatumia ujuzi na uzoefu gani kwenye biashara?
 • Biashara yangu itakuwa na muundo gani kisheria?
 • Niiite biashara yangu jina gani?
 • Nitatumua vifaa gani, na nitakuwa na mahitaji gani?
 • Nahitaji bima ya aina gani?
 • Nahitaji fedha kiasi gani?
 • Nina rasilimali zipi?
 • Nitajilipaje?

Majibu yako yatasaidia kutengeneza mpango makini, uliofanyiwa utafiti wa kutosha, ambao utautumia kama ramani ya kuelekeza kila hatua katika utekelezaji wa biashara na hata kupata mtaji.

Chagua muundo sahihi wa biashara yako.

Unapoanzisha biashara yoyote, mojawapo ya maamuzi muhimu sana ya kufanya ni uchaguzi wa muundo wa hiyo biashara. Mambo yanayozingatiwa katika kuchagua muundo wa biashara ni pamoja na:

 • Masharti ya kisheria
 • Uwajibikaji wa wamiliki kwa madeni ya biashara
 • Aina ya shughuli za biashara
 • Mgawanyo wa mapato
 • Mahitaji ya mtaji
 • Idadi ya wafanyakazi na utawala
 • Manufaa na hasara za kihasibu/ kikodi
 • Urefu wa mzunguko wa biashara

Masuala ya Kuzingatia katika kuanzisha Biashara

Masuala ya Kuzingatia katika kuanzisha Biashara
Sehemu hii imetayarishwa kwa lengo la kuonesha masuala muhimu unayotakiwa kuzingatia kabla ya kuanza biashara yako. Unaweza kuiangalia sehemu hii na kujaribu kuhusisha yaliyoandikwa hapa na mahitaji ya biashara yako, aina ya wateja wako na huduma/bidhaa unayotegemea kuuza au kutoa.
Jiandae kuanza biashara yako kwa kuamua ni aina gani ya biashara unayotaka kufanya pia ni vyema kuyajua masuala ya kisheria yanayohusiana na aina hiyo ya biashara.

Tayarisha mpango wa biashara yako na ujifunze kutokana na makosa ya watu wengine. Bonyeza katika kila sehemu iliyo hapo chini ili upate taarifa zaidi:-

 

Masuala ya Kodi na Lesesni kwa biashara yako

Kuchagua Biashara Sahihi

kuku

Jaribu kutafuta biashara ambayo ina faida kubwa na ya muda mrefu kiuchumi

Katika kuchagua na kufanya uamuzi juu ya biashara unayotaka kuifanya ni vema kuchukua muda katika kufanya uamuzi sahihi. Hutapungukiwa kitu chochote kwa kuchelewa au kupitwa na baadhi ya fursa. Mchakato wa kuchagua unahusisha kujipanga kwa kina na uzoefu wako na ujuzi kamili wa masuala ya biashara ni muhimu ili ufanikiwe katika biashara yako.

• Usifanye biashara ambayo changamoto zake ni kubwa sana kwa anayeanza biashara. Ni vizuri kutambua na kutatua changamoto iliyo ndogo kuliko kubwa
• Jaribu kutafuta biashara ambayo ina faida kubwa na ya muda mrefu kiuchumi
• Anzisha biashara ambayo itakuwa inakua katika soko kila siku
• Fuata ushauri wa wajasiriamali waliofanikiwa kama vile Reginald Mengi, Mohamed Dewji/Enterprises ambao wanashauri juu ya biashara ambayo iliyojikita zaidi kwa watumiaji/wateja katika kupanga bei na ukuaji wa masoko wa muda mrefu
• Biashara za kukwepa kufanya mara nyingi ni zile za bidhaa za kuuza na kununua kwa sababu zitakulazimu kufuata bei ya soko na ili kuendelea kufanya biashara husika itakulazimu kuwa na bei ya chini ya bidhaa yako
• Kama unadhamiria kufanya biashara ya kutegeneza bidhaa hakikisha umeshafanya tathmini ya faida na hasara ya kutafuta mtu wa kukuzalishia kwa bei ya chini
Masuala ya kufanya na kuepuka ukiwa unaanza Biashara
Mambo ya kufanya
• Anza kwa kuweka akiba ya kuendeshea biashara yako
• Jifunze aina ya biashara yako kwa kufanya kazi kwa mtu mwenye biashara kama hiyo
• Fikiria kuanzisha biashara ya kwako tofauti na ulipoajiriwa
• Fikiria juu ya uwezekano wa kuanzisha biashara ya familia
• Kwa malengo kabisa pima ujuzi wako na mafunzo uliyo nayo dhidi ya ushindani unaotazamiwa kuwepo
• Fikiria kumtafuta mzalishaji kwa niaba yako kama unafikiria kufanya biashara ya uzalishaji bidhaa
• Fanya majaribio ya soko la biashara yako kabla hujaamua kuianzisha au kuikuza
• Ongea na watu mbali mbali wenye utaalamu kuhusu biashara yako kwa ajili ya ushauri
• Tengeneza orodha ya vitu vitakavyokuwa ni rafiki na ambavyo sio rafiki kwa biashara yako

Mambo ya Kuepuka
Kuacha kazi kabla hujamaliza mipango ya kuanza biashara yako
Kuamua kufanya biashara ya kitu ambacho hufurahii kufanya
Kuhatarisha rasilimali zote za familia na kwa hiyo, jitahidi kufanya hasara zako kuwa za kiwango kinachotambulika
Kushindana na mwajiri wako katika biashara yako ya pembeni uliyoianzisha
Kufanya haraka katika kuamua biashara ya kufanya ambapo hakuna gharama zozote ukichelewa kuzitumia fursa
Kuchagua biashara ambayo changamoto zake ni kubwa sana kwa muanzaji biashara
Kufanya biashara itakayokulazimu kuuza bidhaaa kwa bei ya chini ili kufanikiwa
Kuacha kujifunza upande hasi wa biashara unayokusudia kufanya
Kuruhusu kujiamini kwa kijasiriamali kwa kupuuza taarifa zilizo za uhakika
Kuruhusu matamanio ya mafanikio yazidi uhalisia wa majaribu ya kibiashara

Aina za muundo wa biashara

Utangulizi

Wiki iliyopita tulijifunza mambo mbalimbali unayotakiwa kufanya kabla ya kuanzisha biashara. Baada ya kujua mambo hayo sasa tujifunze aina mbalimbali za biashara.

Mojawapo ya maamuzi ya mwanzoni kabisa unayohitaji kufanya kwa ajili ya biashara yako mpya ni kuchagua aina ya muundo wa biashara unaoona unakufaa. Uchaguzi unaofanya ni muhimu kwa kuwa utaathiri uwezo na mamlaka ya biashara yako kufanya au kutofanya jambo fulani. Kuwa na aina na muundo sahihi wa biashara kutakusaidia kukuongoza wakati biashara yako iko kwenye mafanikio au wakati wa taabu.

Muundo sahihi wa biashara ndio utakuongoza nini cha kufanya ikiwa utashtakiwa, na kwa namna gani wewe na biashara yako mtatozwa kodi. Kimsingi ziko namna kuu tatu za kuunda biashara, zimeelezewa hapa chini

 • Biashara inayoendeshwa na mtu binafsi peke yake
 • Biashara inayomilikiwa na kuendeshwa kwa Ubia
 • Kampuni yenye ukomo wa madeni

Biashara inayomilikiwa/ kuendeshwa na mtu mmoja

Biashara inayoendeshwa na mtu binafsi peke yake, au Mfanyabiashara pekee ni aina ya biashara ambayo imeenea sana miongoni mwa wajasiriamali nchini. Hii ni biashara ambayo ni rahisi sana kuanzisha kwani mmiliki hufanya usajili wa jina la biashara na kutimiza masharti mengine machache kabla ya kufungua bishara.

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) imetoa mwongozo wa kusajili jina la biashara ambapo mjasiriamali atatakiwa kulipia wastani wa Shilingi 20,000. Mwongozo huu unapatikana kwenye tovuti ya Brela. Mada zijazo pia tutajadili namna ya kusajili biashara.

Biashara inayomilikiwa na mtu mmoja inaweza kuendeshwa kwa jina la mmiliki au jina jingine lisilo lake. Biashara ya aina hii imejipatia umaarufu mkubwa sana kutokana na urahisi wake, haswa katika uanzishaji, pamoja na gharama ndogo. Mfanyabiashara anahitaji tu kujisajili au kusajili jina lake na kupata leseni na hivi hutosha kuanza kufanya biashara.

Hasara kubwa ya kipekee ya muundo huu wa biashara ni kuwa mmiliki anabeba majukumu kwa madeni yote ya biashara yake. Hivyo ikiwa atapata matatizo ya kifedha, wadeni wanaweza kufungua kesi/ madai dhidi yake na yakifanikiwa yeye binafsi atawajibika kulipa madeni hayo kutoka kwenye vyanzo binafsi vya fedha.

 

Ubia

Hii ni biashara inayotambulika kisheria inayofanywa na watu wawili au zaidi wanaoshiriki katika umiliki, utendaji na faida au hasara za biashara hiyo. Ziko aina kuu mbili za ubia, ubia wa jumla (usio na ukomo wa madeni) na ubia wenye ukomo wa madeni.

Katika ubia usio na ukomo wa madeni (ubia wa jumla), wabia wanaendesha biashara na wanawajibika kwa madeni ya biashara na mali zao binafsi zinaweza kulipia madeni hayo. Kwenye ubia wenye ukomo wa madeni, baadhi ya wabia huwa na ukomo wa kuwajibika kwa madeni ya biashara na baadhi huwa hawana. Wale wasio na ukomo wa kuwajibika kwa madeni ya biashara wanamiliki biashara na wanawajibika binafsi kwa madeni ya biashara, na wale wenye ukomo huwekeza tu, hawana nguvu ya moja kwa moja katika maamuzi ya biashara na hawawajibiki kuchangia fedha binafsi kulipa madeni ya biashara.

Uwajibikaji binafsi wa wabia kwa madeni ya biashara ni suala kubwa la kufikiria iwapo unatazamia kuendesha biashara kwa mfumo wa ubia. Kama ilivyo kwa wafanyabiashara wanaomiliki biashara peke yao, wabia wanawajibika kwa fedha zao binafsi kulipia madeni ya biashara. Kila mbia wa jumla (asiye na ukomo wa madeni) anaweza kufanya maamuzi na kuingia katika makubaliano ambayo wabia wenzake wote watayaheshimu na yatawaathiri (kutegemeana na makubaliano/ mkataba wa ubia wao) kwa niaba ya biashara.

Kumbuka kuwa biashara ya ubia ina gharama kubwa zaidi kuianzisha na kuiendesha kuliko biashara ya mtu binafsi, hii inatokana na ukweli kuwa kuna taratibu mbalimbali inabidi zifuatwe kabla ya biashara kuanza. Taratibu hizo ni pamoja na kuweka makubaliano ya namna ya kuendesha biashara, mgawanyo wa mapato na mengine mengi.

 

Ikiwa utaamua kuendesha biashara kwa mfumo wa ubia, hakikisha kuwa umeweka kimaandishi makubaliano au mkataba kuonesha namna maamuzi yatakavyofanyika, namna ya kumaIiza tofauti zinazotokea katika kufanya maamuzi, na hata namna ya kufikia makubaliano ya kubadilisha umiliki wa biashara itakapohitajika kufanya hivyo. Makubaliano hayo yanasaidia sana pale itakapotokea kwa sababu moja au nyingine biashara imeingia katika matatizo ya kifedha au ya kiuendeshaji, au ikitokea mbia mmojawapo anataka kuondoka kwenye biashara.

Mkataba wa ubia unapaswa kukazia kuhusu kusudi la biashara na mamlaka na wajibu wa kila mbia. Ni vema kupata msaada wa kisheria kutoka kwa mwanasheria mwenye uzoefu na mambo ya biashara ndogo na za kati katika kuandika mkataba wa ubia. Mambo mengine ambayo ni muhimu yazungumziwe katika makubaliano ya ubia ni:

 • Umiliki utachangiwa kwa viwango gani? Si lazima viwango vya umiliki na na mgawanyo wa majukumu vilingane kati ya wabia wote. La msingi ni kuhakikisha kiwango cha kila mmoja kiko katika makubaliano.
 • Maamuzi yatafanyika kwa mtindo gani? Ni vema kuweka makubaliano juu ya haki za kupiga kura baina ya wabia ikiwa wameshindwa kufikia muafaka kwenye suala fulani. Ikiwa wabia ni wawili tu na umiliki wao ni nusu kwa nusu, uko uwezekano wa kushindwa kufikia muafaka katika kuamua jambo. Kuepusha hili, biashara zingine huamua kuweka mbia wa tatu, mtu anayeaminika na kummilikisha asilimia ndogo tu ya biashara, ili kusaidia kuiondoa biashara kwenye mkwamo wa aina hiyo.
 • Ikiwa mbia mmoja atajiondoa, kiasi cha kumlipa kitaamuliwaje? Namna mojawapo ya kuamua kuhusu hili ni kuwa na mhusika aliye nje ya ubia, mfano benki, au mhasibu kutafuta mtathmini atakayethaminisha kiasi cha kumlipa mbia anayejitoa katika ubia.
 • Ikiwa mbia atajitoa katika biashara, ni lini anapaswa kulipwa fedha yake? Hii inaweza kuwekwa katika makubaliano ili ijulikane bayana. Ikiwa itachukua muda mrefu, inaweza kuwa busara kuweka makubaliano kuwa ilipwe pamoja na riba. Bila makubaliano haya uendeshaji biashara unaweza kuathirika ikiwa mtu atajitoa na kiasi chote kulazimika kulipwa kwa mkupuo kwa haraka mara anapojitoa.

 

 

 

2.4 Kampuni yenye ukomo wa madeni

Kampuni yenye ukomo wa madeni ni muundo wa shirika ambamo uwajibikaji wa wamiliki (wanahisa) kwa madeni ya biashara unakomea kwenye kiasi walichowekeza katika kampuni, au ambacho wamekubaliana kukiweka dhamana kwa ajili ya kampuni. Hivyo kampuni yenye ukomo wa madeni inaweza kuwa na ukomo kwa njia ya hisa au ukomo kwa njia ya dhamana waliyoweka wanahisa. Suala la nani anaweza kuwa mwanahisa wa kampuni binafsi linatawaliwa na sheria na kanuni za kampuni.

Kama ilivyo kwa biashara zingine zinazoendeshwa hapa nchini, Kampuni yenye ukomo wa madeni inapaswa kusajiliwa na Mamlaka ya Usajili na Leseni za Biashara, ambayo iko chini ya wizara inayohusika na Biashara. Katika usajili, hatua ya kwanza ni kupata kibali cha kutumia jina la biashara kinachotolewa na mamlaka hiyo. Nyaraka/ taarifa zifuatazo zinahitajika katika mchakato wa kuanzisha kampuni:

 • Jina la kampuni (ambalo lazima lipitishwe na msajili wa makampuni);
 • Anuani rasmi ya ofisi ya kampuni Tanzania;
 • Majina, anuani, na utaifa wa wanahisa wa kwanza na wakurugenzi wa kampuni (angalau wawili kwa kampuni binafsi au saba kwa kampuni ya umma).
 • Mkataba wa kuanzisha kampuni (unaotaja madhumuni ya kampuni) na sheria/ makubaliano yanayosimamia utendaji na maamuzi ya kampuni (inayotaja muundo wa uongozi na michakato ya maamuzi mbalimbali). Angalau nakala mbili za kila waraka zinapaswa kuwasilishwa.;
 • Kujaza fomu maalumu zenye tamko kuwa kampuni imezingatia matakwa ya sheria ya makampuni Tanzania; na
 • Kulipa tozo/ ada za kuwasilisha nyaraka, usajili, na ushuru wa stempu.

Hatua kwa hatua katika kuanzisha na kusajiri biashara

Sheria zinazohusu Ujasiriamali Mdogo, wa Kawaida na wa Kati

Sheria ni mkusanyiko wa amri zinazodhibiti mahusiano kati ya watu na makundi ya watu katika jamii. Kwa hiyo, kufuata sheria ni sharti la lazima kwa ajili ya kupata mpangilio unaoeleweka katika jamii. Katika biashara ni lazima kufuata sheria zilizowekwa kuongoza biashara husika. Ufuataji wa sheria unapelekea namna bora ya mpangilio wa ufanyaji biashara husika katika misingi na amri zilizowekwa. Hii husaidia kuepusha ufanyaji wa vitendo visivyokubalika katika biashara husika hivyo kupelekea mfanyabiashara kutoingia katika matatizo na mamlaka zenye majukumu ya kusimamia biashara husika kisheria. Ifuatayo ni orodha ya sheria husika zilizochaguliwa kuongoza Wajasiriamali Wadogo, wa Kawaida na wa Kati:

(i) Sheria ya Makampuni (2002)

Hii ni sharia inayosimamia usimamizi biashara za aidha makampuni au mtu mmoja mmoja. Sheria imetoa maelekezo muhimu katika uendeshaji wa kampuni na biashara kwa ujumla. Sheria inaelezea uhuru wa kampuni na michakato mbali inayohusisha usimamizi wa biashara na kampuni. Sheria hii imeainisha matakwa yafuatayo uanpotaka kufungua na kusajili shughuli za kampuni/biashara yako:

  1. Kuwasilisha kumbukumbu za mwaka zinazojumuisha taarifa zote muhimu za kampuni pamoja na taarifa kuhusu hisa, ukurugenzi na gharama zingine;

  2. Kuwasilisha mahesabu yaliyokaguliwa;

  3. Kuwasilisha mabadiliko yoyote ya taarifa za kampuni kama vile mabadiliko ya jina la kampuni, malengo, madhumuni, Bodi ya Wakurugenzi, majina ya mtaji, viwango vya hisa, uteuzi wa wapokeaji, mameneja, watawala na utaratibu wa ufilisi; na

  4. Malipo mbali mbali ya kodi serikali kuu na serikali za mitaa.

Kampuni (na ofisi zake) ambayo haitazingatia yaliyoainishwa pamoja na mahitaji mengine yaweza adhibiwa kwa kutozwa faini kulingana na ukubwa wakosa, na wakati mwingine kushitakiwa. Kuzingatia hayo kutafanya watu waiamini kampuni na kuifanya iweze kukopesheka na hatimae kuaminiwa na wadau mbalimbali.

(ii) Sheria ya Mkataba

Sheria hii inayataka makampuni/biashara kufuata kanuni,maelekezo na mahitaji yahusuyo mikataba baina ya muajiri na muajiriwa. Kama mahitaji ya kisheria hayatazingatiwa, mkataba unakuwa batili, hili linatokana na kushindwa utekelezaji wa sheria husika. Kwa hiyo, ni muhimu kuhakikisha kwamba mikataba iliyoridhiwa inafanyika kisheria kwa kuzingatia mahitaji ya sheria. Pia inashauriwa kwa waajiri kutafuta ushauri kwa mwanasheria au mtaalamu yeyote wa masuala ya sheria kabla ya kuingia mkataba na mwajiriwa wake ili kuhakikisha kwamba biashara inaendeshwa kulingana na matakwa ya sheria husika.

(iii) Sheria ya Kazi

Sheria hii ya kazi inaongoza mahusiano kati ya biashara (kama mwajiri) na wafanyakazi wake (kama waajiriwa). Pia inatengeneza taratibu za kushughulika na masuala ya ajira na usuluhishi wa migongano ya kimaslahi kuhusiana na haki na stahiki za muajiri na muajiriwa, namna ya kuingia mkataba wa kazi pamoja na masuala ya malipo ya pensheni, na mafao mengine ya wafanyakazi. Uhusiano chanya ni suala muhimu katika kazi au ujasiriamali wa aina yoyote ili kuhakikisha utendaji uliokusudiwa unafikiwa, na katika hili sharia haibagui kikundi chochote cha ajira iliyo rasmi kama wajasiriamali.

(iv) Sheria ya Leseni

Kimsingi hii iko chini ya Sheria ya Leseni za Biashara, (Cap. 208). Sheria hii inazuia kufanya biashara bila leseni. Leseni hutolewa kwa ajili ya biashara mahsusi na katika eneo husika. Mamlaka za leseni zina nguvu ya kufunga eneo la biashara inayofanyika bila leseni na kwa kufanya hivyo, mamlaka yaweza omba msaada wa afisa polisi au mhusika yeyote aliyeidhinishwa.

(v) Sheria ya Ardhi

Sheria kuu ya ardhi nchini Tanzania ni Sheria ya Ardhi Sura 113. Hii ni sheria ya msingi kulingana na aina za ardhi nchini Tanzania, licha ya kusimamia moja kwa moja ardhi ya kijiji pia inaongoza uendeshaji wa ardhi na usuluhishi unaoendana na matatizo ya ardhi. Biashara yoyote lazima iwe na eneo. Kwa sababu hiyo, biashara yaweza miliki ardhi yake au mali au kukodisha sehemu toka kwa mmiliki. Ardhi yaweza tumika kutunisha mtaji kwa njia ya amana, na ardhi hiyo kuwa kama dhamana ya mkopo. Sheria inaruhusu uanzishwaji, usajili na utekelezaji wa mipango hiyo.

(vi) Sheria ya Haki Miliki

Sheria hii imependekezwa kwa malengo ya kulinda/kutetea haki mbali mbali na matumizi ya uvumbuzi wa kiteknolojia, bidhaa au huduma. Uvumbuzi unatakiwa kusajiliwa katika Ofisi ya Msajili wa Leseni. Sheria pia inatoa haki ya umiliki na matumizi kwa mvumbuzi halisi na inatoa maelekezo kwa mtu yeyote atakayependa kutumia uvumbuzi huo kulingana na makubaliano yatakayofanyika na mvumbuzi halisi wa ujuzi au huduma husika.

(vi) Sheria ya Bima

Sheria hii inaelekeza taratibu za bima kwenye biashara na kuweka miongozo na taratibu zinazoongoza makubaliano ya bima kati ya wafanyabiashara ya bima na wafanyabiashara wanaotaka kuwekea bima biashara zao. Kuna aina tofauti tofauti za bima kama vile Bima ya moto, bima ya wizi, bima ya magari na bima ya fidia kwa kazi ni baadhi ya madhara yanayohusiana na biashara.

(vii) Sheria ya Mirathi

Lengo kuu la sheria hii ni kutoa utaratibu wa kusimamia mali za marehemu baada ya kifo chake ikiwamo kuhamisha umiliki wa mali hizo kutoka kwa marehemu kwenda kwa watu wenye haki ya kuzipata mali hizo.Nia hasa ni kwamba mali alizoacha marehemu zisibaki zikiharibika na kupotea bure,au warithi halali au watu wenye maslahi na mali za marehemu,kwa mfano wale wanaomdai hawapotezi haki hiyo, bali awepo mtu ambaye atazisimamia na kuzigawa kwa wahusika wakiwamo wadai na kuepusha mgongano katika jamii husika.Hivyo sheria inamuweka msimamizi wa kugawa mirathi husika na mamlaka yake.

Usajili wa Biashara

Baada ya kuwa na mpango wa biashara unaobainisha namna biashara yako itakavyokuwa, hatua inayofuata ni usajili wa leseni ya biashara. Kisheria, usajili wa biashara na leseni vinafanyika kwa vyombo kama BRELA na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Ili kusajili biashara, hatua/taratibu zifuatazo zinatakiwa kuzingatiwa.

HATU YA 1: Ombi la kibali cha kupata jina la biashara

Katika hili, mtu anahitajika kuomba kuidhinishiwa jina la biashara alilopendekeza kwa kuwasilisha majina matatu (3) ili kuhakikisha kuwa biashara haitakuwa na jina linalofanana na biashara iliyopo tayari. Kazi hii inafanywa na BRELA na hii yaweza fanyika kwa kuandika barua ya maombi ya jina na kibali cha biashara husika.

Baada ya kupewa taarifa kuwa jina limeidhinishwa, mwombaji ataandaa kanuni na katiba ya biashara na kuviwasilisha BRELA. Kama kanuni na katiba ya biashara vilikwisha andaliwa na kuwasilishwa kwa usajili kabla ya kupata idhini ya kutumia jina fulani la biashara, utafutaji wa jina utafanyika wakati wa usajili.

Angalizo: Mchakato huu ni bure, hautozwi malipo. Taarifa zaidi kuhusu usajili wa biashara na jina la biashara inaweza kupatikana kupitia anwani ya tovuti ifuatayo, www.brela.go.tz

HATUA YA 2: Kupata Tamko la Uthibitisho wa Kisheria kuhusu Uzingatiaji (Compliance)

Katika hatua hii, mjasiriamali/mmiliki wa biashara lazima aende kwa mwanasheria kwa ajili ya kuwekewa tamko na sahihi ya uthibitisho kisheria kuhusu uhalali wa nyaraka husika. Wanasheria wenye jukumu la kuthibitisha nyaraka kisheria wanatoza kati ya shillingi 10,000 hadi 50,000 kwa huduma za kuthibisha uhalali wa nyaraka mbali mbali.

HATUA YA 3: Maombi ya kuthibitisha ushirika wa kampuni na kupata hati ya uthibitishwaji wa kampuni

Hii inafanyka kwa kujaza fomu namba 14A ambayo itaeleza mahali ofisi ilipo, maelezo muhimu ya wakurugenzi na katibu wa kampuni hiyo. Lengo hapa ni kutambua utaifa wa kampuni na maelezo binafsi ya waendesha kampuni, kujua kama wamiliki (Directors) wanasifa kuwa wamiliki wa kampuni kifedha pamoja na umri uwe zaidi ya miaka 21.

Kujaza fomu namba 14b ambayo ni ya kiapo kuwa kampuni husika imefuata taratibu zote za kisheria. Kanuni na katiba ya kampuni inaambatanishwa na fomu hizi.

Baada ya kuwasilisha fomu za maombi, hati ya usajili wa kampuni, maombi haya hushughulikiwa kwa kawaida ndani ya siku 2 hadi 3. Fomu za Usajili ni bure na maombi ya ada za usajili (kulingana na Sheria Mpya ya Makampuni ya mwaka 2002) zinaoneshwa katika jedwali lifuatalo:

Fomu namba 14 A

Fomu 14 b

Jedwali 1: Ada ya usajili wa kampuni (kulingana na hisa za mitaji)

[embeddoc url=”https://entrepreneurs.or.tz/wp-content/uploads/2016/01/Ada-ya-usajili-wa-kampuni.pdf”]

Ghrama zingine: Ada ya jalada, shillingi 45,000: 15,000 kwa kila waraka

Ada ya Stampu:

– Mkataba halisi na Makala ya Chama, shillingi 6,200

– Kila nakala ya ziada, shillingi 5,000

HATUA YA 4: Maombi ya Utambulisho wa Namba ya Mlipa Kodi (TIN) Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)

Usajili wa Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN) ni bure. Inachukuwa kati ya siku 1 hadi 2 kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN), hii inategemea idadi ya maombi yaliyowasilishwa TRA kwa wakati husika. Cheti cha ushirika wa Kampuni sharti kiambatanishwe na maombi ya TIN pamoja na Mkataba na makala ya chama kwa mwombaji wa nambari ya utambulisho kutoka TRA.

Kampuni (komo, limited) itaomba hati ya TIN kwa kujaza fomu za maombi kama ifuatavyo:

 1. Maombi ya kampuni

 2. Maombi kwa kila mwana hisa/mkurugenzi, kama mkurugenzi ana hati ya TIN tayari kwa sababu nyingine yoyote hawezi kupewa hati nyingine ya TIN. Hati ya TIN hiyo hiyo itatumika.

Walau mmoja kati ya wanahisa/wakurugenzi lazima awepo katika ofisi za kodi ili kuchukua kumbukumbu za alama za vidole. Mwombaji lazima afike katika ofisi za TRA ili kuchukua hati ya TIN mwenyewe. Kampuni itatakiwa kuwasilisha makadirio ya mapato kwa ajili ya tathmini ya makisio ya kodi katika mwaka husika. Katika ofisi za TRA, Afisa Kodi anaweza kuwasaili waanzilishi/wakurugenzi wa kampuni na kuweka kumbukumbu za biashara yao pamoja na taarifa zao binafsi.

HATUA YA 5: Maombi ya leseni ya biashara Wizara ya Viwanda na Biashara, na Mamlaka za Serikali za Mitaa i.e. Afisa Biashara Mkoa/Wilaya

Leseni ya biashara hutolewa na Wizara ya Biashara na Viawanda au Mamlaka kutoka Serikali za Mitaa, kutegemea na aina ya biashara. Maombi ya leseni huambatana na nyaraka zifuatazo lazima ziwasilishwe:

 1. Hati ya kuingizwa kampuni

 2. Mkataba na Makala za Chama

 3. Uthibitisho wa Uraia wa Tanzania

 4. Uthibitisho wa maeneo mwafaka ya kampuni

 5. Hati ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN)

Wizara ya Viwanda

HATUA YA 6: Moambi kwa ajili ya Hati ya Kodi ya Ongezeko la Thamanai (VAT) katika ofisi za TRA

Kodi hii inahusu biashara zote zenye usajili wa mtaji wa kuanzia shilingi millioni 50 kwa miezi sita ya awali katika biashara au shilingi millioni 100 katika mwaka wanatakiwa kusajili kodi ya ongezeko la thamani (VAT). Hata hivyo, gharama hizo hulipwa na wateja. Ili kusajili VAT, mtu anatakiwa kwenda katika ofisi ya TRA iliyo karibu kupata fomu za usajili. Usajili unahusu wote isipokuwa biashara zinazotoa huduma ya kitaalamu kama udaktari au uanasheria. Njia nyingine ya usajili ni kupitia anwani ya tovuti ya TRA.

Tembelea tovuti ya TRA

HATUA YA 7: Sajili biashara yako kwa ajili ya fidia kwa wafanyakazi katika Shirika la Bima la Taifa au mtoa huduma ya bima mbadala

Kusajili bima ya fidia kwa wafanyakazi, waajiri lazima wajaze fomu maalumu kwa ajili hiyo (Workmen’s Compensation Tarriff Proposal Form). Hii inafanyika katika Mfuko wa Fidia ya Wafanyakazi (WFC) na Mamlamka ya Udhibiti wa Bima Tanzania (TIRA). Fomu hiyo lazima ikamilishwe pindi kampuni inapoanza kuajiri wafanyakazi na kabla ya kampuni haijaanza shughuli. Hata hivyo, kwa vile sekta ya bima imebinafsishwa Tanzania, waajiri wana uhuru wa kujisajili kwenye bima badala ya ile ya madai ya fidia kwa wafanyakazi.

HATUA YA 8: Pata nambari ya usajili kwa kampuni yako kutoka mifuko ya hifadhi ya jamii ya lazima

Maombi ya nambari hii huchukua muda usiozidi wiki moja katika mifuko ya hifadhi ya jamii Kila mwajiri katika sekta iliyo rasmi anatakiwa kusajili wafanyakazi wake katika mifuko ya lazima ya hifadhi ya jamii, hii inatokana na uhalisia kwamba ni haki ya kila mfanyakazi kuchagua mfuko wowote wa hifadhi ya jamii. Mifuko ya hifadhi ya jamii ya lazima imeanzishwa kwa sheria za nchi na imedhaminiwa na serikali kutoa huduma za hifadhi ya kijamii kwa manufaa ya wafanyakazi.

Utafutaji wa Masoko

Kufanya utafiti wa masoko ni muhimu sana ili kujua kama watu watanunua bidhaa ama huduma zako. Utafiti unaweza kufanyika kwa kuanzia kwa watu wanao kuzunguka kwa kuwauliza kama wataweza kununua bidhaa zako kwa bei ambayo umeipanga.

Ni muhimu kuhakikisha unauliza watu sahihi ili upate picha kamili, usiulize rafiki zako au ndugu zako wa karibu maana watakubali ili kukuridhisha na kukupa moyo.

Utafiti wa Masoko

Mpango wako wa masoko ni muhimu kwa ajili ya mpango mzima wa biashara yako. Mabenki na wakopeshaji wengine watataka kufahamu ni namna gani umejipanga kuzalisha fedha. Ukianzisha, mpango wa shughuli za masoko utakusaidia sana ku:

 • Kutathmini mahitaji ya wateja na kubuni bidhaa zinazowafaa
 • Kufikisha ujumbe kuhusu sifa za bidhaa au huduma zako kwa wateja wako
 • Kuandaa mfumo wa usambazaji wa bidhaa kuwafikishia wateja
 • Kuchagua namna bora ya kuvutia wateja
 • Kuchagua njia zinazofaa za kutangaza biashara

Kabla ya kutengeneza mpango wa masoko kwa bidhaa au huduma yako unapaswa kutafiti soko la bidhaa/ huduma yako. Tumia matokeo ya utafiti wa masoko kama ushahidi wa kauli unazotoa katika mpango wako wa masoko.

Utafiti wa masoko

Utafiti wa masoko ni mchakato wa kukusanya taarifa ambao zitakuwezesha kufahamu namna ambavyo wateja unaotarajia kuwauzia bidhaa/ huduma watachukulia biashara au huduma yako.

Mfanyabiashara yeyote hufanya utafiti huu, kwa kujua (kupanga) au kutokujua. Kwa mfano, unapozungumza na wateja kuhusu biashara yako, au unapotizama bei za washindani wako tayari unafanya utafiti wa masoko. Kuufanya utafiti huu kuwa rasmi kunaweza kukupa taarifa zenye thamani kubwa kuhusu bidhaa na huduma zako, pamoja na wateja na soko unalohudumia.

 

Namna ya kufanya utafiti wa masoko

Ni muhimu kwanza kuweka malengo yaliyo bayana kwa ajili ya shughuli ya utafiti unayoiendea. Unapaswa kuwa na uhakika kuhusu jambo gani unahitaji kufahamu na kwa nini.

Ukishajiwekea malengo, ni muhimu kutengeneza mkakati na kuchagua mbinu za kukusanya takwimu. Aina kuu mbili za utafiti unazoweza kutumia ni utafiti wa awali na utafiti unaotegemea tafiti zingine

Utafiti wa awali

Katika utafiti wa awali unakusanya taarifa za awali ama kwa ajili yako au kwa kwa niaba ya taasisi ya kitafiti) ili kujibu maswali ya kitafiti au kufikia malengo ya kitafiti. Taarifa hizi hukusanywa kwa njia ya madodoso, kufanya uchunguzi kwa kuona, ama kufanya majaribio.

Utafiti wa awali unaweza kujibu maswali yafuatayo kwa mfano:

 • Wateja wetu ni kina nani na tutawafikiaje?
 • Sehemu zinazofaa kuweka biashara
 • Mikakati ya kimasoko
 • Wateja wanahitaji bidhaa na huduma zipi?
 • Mambo gani yanaathiri maamuzi ya wateja wangu kununua? Je ni bei, huduma, urahisi, au jina/ chapa/ utambulisho n.k.?.
 • Niweke bei gani kwa ajili ya bidhaa/ huduma zangu? Matarajio ya wateja?
 • Washindani wangu ni kina nani? Wanafanyaje biashara zao? Wana nguvu gani na madhaifu gani?

Baadhi ya hasara za utafiti wa awali ni kuwa unaweza kugharimu muda mresu na fedha nyingi, hasa pale inapobidi kutumia watu wengine kuufanya, na matokeo yake hayapatikani haraka.

Faida za utafiti wa aina hii ni kuwa unaweza kuufanya kwa kulenga makundi mahsusi (kwa mfano wateja wako, au eneo linaloizunguka biashara yako) na unaweza kutengeneza dodoso lako kujibu maswali mahsusi. Pamoja na kupunguza gharama (fedha), kufanya utafiti kwa kushiriki mwenyewe moja kwa moja kutakuwezesha kupata ufahamu mzuri wa soko la biashara yako..

Madodoso ndio namna maarufu kuliko zote za kukusanya taarifa za awali. Yanaweza yakafanyiwa kazi kupitia:

 • Barua za moja kwa moja kwa walengwa, ambapo walengwa wanapatiwa madodoso na kuyajibu kasha kurudisha kwa njia hiyo hiyo. Ufanisi wa njia hii una shaka, na unahitaji ufuatiliaji na kukumbushia
 • Utafiti kwa njia ya simu – huu una gharama ndogo ila wakati mwingine inaweza kuwa ngumu kuwafikia wateja. Pia watu wengine hawapendi usumbufu wa simu
 • Utafiti kwa njia ya wavuti. Huu unawezesha washiriki kujaza dodoso kwa wakati wao kupitia wavuti. Gharama yake ni ndogo
 • Kutumia usaili wa mtu mmoja mmoja au vikundi. Huu unawezesha kuuliza maswali ya ziada au kubadilisha uelekeo wa utafiti kwa urahisi pale inapohitajika

Unapotengeneza dodoso kwa ajili ya utafiti, hakikisha:

 • Linakuwa fupi na rahisi kwa kadri iwezekanavyo
 • Linavutia na linasomeka kirahisi
 • Anza na maswali ya jumla kuelekea kwenye maswali mahsusi
 • Maswali yawe mafupi na yanayoeleweka kirahisi
 • Usiweke maswali yanayotoa muelekeo wa jibu, au yenye maneno tata, au magumu sana kujibu
 • Iwapo utatumia majibu yanayopimwa kwa namba au viwango vingine, viwe vipimo vinavyoeleweka bila utata
 • Lijaribu dodoso lako kung’amua ikiwa lina matatizo yoyote kabla ya kulitumia

Vyanzo vya kimtandao/ wavuti mbalimbali vinaweza kukupatia mfano wa dodoso na kubadilisha maswali kuendana na matakwa yako, ziko pia kampuni zinazowezesha kutengeneza na kufanya utafiti kwa njia ya mtandao.

Taarifa nzuri kuhusu wateja wako inaweza kupatikana bila kuwahusisha wateja wenyewe moja kwa moja. Kuwahoji wafanyakazi wako kunaweza kukupa majibu mazuri maana wao wanakutana na wateja kila siku na wanaweza kukupatia taarifa kuhusu:

 • Sifa za wateja (umri, jinsia, n.k.)
 • Bidhaa na huduma zinazohitajika na wateja
 • Kuridhika kwao na kiwango cha bei na ubora wa bidhaa
 • Maoni yao kuhusu washindani wako

Utafiti unaotegemea tafiti zingine

Utafiti huu unatumia taarifa zilizopo tayari kama rekodi za kampuni, tafiti zilizofanyika awali na hata vitabu na machapisho mengine na kutumia taarifa hizo kujibu maswali yanayolengwa. Utafiti huu unachukua muda mfupi kuliko utafiti wa awali na unaweza pia kuwa na gharama nafuu.

Pamoja na kuwa utafiti huu haulengi makundi mahsusi, unaweza kuleta taarifa yenye thamani kubwa na kujibu baadhi ya maswali ambayo yasingejibika kirahisi na utafiti wa awali (kwa mfano kuthanimisha kwa icha kubwa hali ya kiuchumi ya soko), au kmaswali ambayo wateja wasingeyajibu kwa uhuru (mfano umri au kiwango cha kipato).

Yafuatayo ni baadhi ya maswali ambayo utafiti huu unaweza ukayakabili:

 • Biashara yangu inajiendesha katika hali gani za kiuchumi kwa sasa? Je hali hizo zinabadilika? (hali za kikanda, kitaifa, kimataifa)
 • Mabadiliko gani yanaathiri sekta ninayofanyia biashara yangu? Wateja wanataka nini?
 • Mabadiliko ya kiteknolojia
 • Bei za bidhaa na huduma
 • Yapo mahitaji ya bidhaa / huduma zangu Katina soko la kimataifa ambayo yataniwezesha kukuza biashara yangu?
 • Zipi zifa za kitakwimu za wateja wangu na wanaishi wapi? Idadi yao, umri, viwango vya mapato, n.k.
 • Hali ya soko la ajira ikoje?
 • Watu wangapi wana ujuzi ninaounitaji?
 • Nitarajie kuwalipa kiwango gani waajiriwa wangu?

Kumbukumbu zilizopo za kampuni kama ankara, risiti, malalamiko rasmi ya wateja ni vyanzo muhimu vinavyoweza kutumika katika utafiti huu. Mara nyingi kumbukumbu hizi hutoa mwanga katika mambo ambayo hata utafiti wa awali huwa unayatafuta, na hivyo kuzichambua kumbukumbu za kampuni unapaswa kufanyika kabla ya kufikiri kukusanya taarifa za awali kwa wateja. Mifano ya kutumia takwimu zilizopo za kampuni kwa ajili ya utafiti wa masoko ni kama::

 • Kutizama risiti za mauzo kuona mwenendo wa mauzo/ mahitaji ya bidhaa au huduma fulani
 • Kulinganisha risiti za mauzo na anwani za wateja ili kutathmini namna ambavyo matangazo ya biashara yamefanikiwa
 • Kuchambua malalamiko ili kufahamu maeneo ya kuboresha katika huduma kwa wateja, bei au bidhaa/ huduma zenyewe

Chanzo kingine cha taarifa nim taarifa za kitakwimu kutoka taasisi rasmi za takwimu na taasisi zingine. Takwimu hizi zinaweza kuingia katika taarifa za kichambuzi na kutoa picha za hali ya soko.

Kufahamu ni taarifa zipi za kitafiti zinaweza kusaidia biashara yako inaweza kuwa kazi ngumu, na baadhi ya takwimu zinauzwa kwa gharama kubwa. Hata hivyo, ziko pia takwimu zenye ubora na taarifa za kichambuzi ambazo zinapatikana, pamoja na mwongozo ambao unaweza kukusaidia kuchambua taarif zilizopo.

Taarifa za idadi ya watu

Pata taarifa kuhusu idadi ya watu na tabia zake kama maeneo, umri, kipato, kiwango cha elimu, n.k.

Taarifa za kazi na ajira

Pata takwimu na uchambuzi kuhusu nguvukazi, ajira na vipato kutoka chanzo rasmi serikalini na vyanzo vya kimataifa

Hali ya uchumi

Pata taarifa za viashiria vya kiuchumi ambavyo vinaathiri utendaji wa sekta mbalimbali kiuchumi

Taarifa za kisekta

Pata taarifa ambazo zitakuwezesha kuelewa sekta yako na soma mwenendo wa kisekta ambao unaweza kuathiri biashara yako.

Tafuta
Kuanzisha biashara
Habari mpya
Maoni
Opinion

Maoni

Je, ni habari au taarifa zipi ungependa ziwekwe zaidi kwenye tovuti hii?

View Results

Loading ... Loading ...
Video

Jinsi ya kujenga wazo la biashara

Kutathmini wazo la biashara