TPSF Kuanzisha Mabaraza ya Ujuzi ya Kisekta

Katika kutimiza azma ya kuboresha biashara nchini, TPSF kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia tunatekeleza Mkakati wa Taifa wa Kuendeleza ujuzi (National Skills Development Strategy) kupitia Mradi wa Kukuza Stadi za Kazi na Ujuzi (Education and Skills for Productive Jobs).

 

Katika mradi huu TPSF tumepewa jukumu la kuanzisha Mabaraza ya Ujuzi ya Kisekta ambapo sekta sita zimepewa kipaumbele nazo ni Kilimo, Utalii, TEHAMA, Ujenzi, Uchukuzi na Nishati. Jukumu lingine ni kuanzisha Baraza la Taifa la Ujuzi baada ya haya ya Kisekta kuanza kazi.

 

Lengo la kuundwa kwa Mabaraza ya Ujuzi ya Kisekta ni kuwaleta pamoja wadau wote kutoka sekta Binafsi na Sekta ya Umma ili kujadiliana namna bora ya kuboresha nguvu kazi nchini.

Kwa miaka mingi Waajiri nchini wamekuwa wakipata changamoto kubwa ya kupata rasilimali watu yenye ujuzi inaohitajika katika kutekeleza majukumu yao. Changamoto hii imekuwa ikisababisha kuongezeka kwa gharama za uendeshaji wa biashara. Waajiri hulazimika kutafuta wataalamu wenye ujuzi stahiki kutoka nje ya nchi au kutumia fedha nyingi katika kugharamia mafunzo kwa watumishi katika sehemu za kazi. Hivyo mradi huu ni muhimu sana kwetu Sekta Binafsi na tunaahidi kuutekeleza kwa ufanisi mkubwa kwa maslahi mapana ya Waajiri na Taifa kwa Ujumla.

Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania, TPSF, ni chombo kilichoundwa kwa dhamira ya kuunganisha asasi zote za kibiashara, uzalishaji na utoaji huduma nchini Tanzania, kwa kusudio la kuwa na sauti moja ya sekta binafsi wakati wa majadiliano na serikali, ili kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji hapa nchini. TPSF iliundwa na kuasisiwa Novemba 4, 1998 na imesajiliwa na Msajili wa Makampuni kama kampuni isiyokuwa na mtaji wa kutengua, yaani ni kampuni inayofanya shughuli ambazo si kwa madhumuni ya kujipatia faida ya kifedha.

 

TPSF imekuwa ikitetea maslahi ya sekta binafsi  kupitia njia ya ushawishi kwa serikali. Ushawishi huu hufanyika kupitia Baraza la Taifa la Biashara katika ngazi ya kitaifa, lakini pia ushawishi huu hufanyika katika ngazi ya mkoa na wilaya kupitia mabaraza ya biashara ya mkoa na yale ya wilaya. Lengo kuu la kufanya majadiliano na serikali ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na mazingira rafiki ya ufanyaji biashara nchini.

Pamoja na kufanya ushawishi, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ili kuwasaidia wajasiriamali nchini kukuza biashara zao. Miradi hiyo imepelekea kunufaisha wajasiriamali wengi sana na kusaidia kwa kiasi kikubwa kupanua biashara. Mfano wa Miradi hiyo ni ule wa kusaidia kukuza mitaji uliojulikana kwa jina la Matching Grant Programme (MGP), ule wa kufundisha na kukuza ujasiriamali uliojulikana kama Business Development Gateway (BDG) na mwingine ni ule wa kukuza ushindani katika mnyororo wa thamani (Value Chain) uliojulikana kama cluster competitiveness program (CCP).

Wengi wa wale walionufaika na miradi hii wamekua sana kibiashara na wametapakaa nchi nzima ikiwa ni pamoja na zanzibar.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *