Ardhi Tanzania

Ardhi

Ili kupata ardhi Tanzania, sheria inatoa uwezekano wa kutumia mwanasheria ili kumwakilisha mteja wake anayetaka kupata ardhi

Kwa mujibu wa sheria ya ardhi ya mwaka 1999, ardhi yote ipo chini ya umiliki wa jumuiya, na itabaki chini ya usimamizi wa Rais kama mdhamini kwa niaba ya raia wote wa Tanzania. Sheria inatambua aina tatu ya ardhi ndani ya Tanzania ambazo ni ardhi ya jumla, ardhi ya kijiji na ardhi ya hifadhi.

Ardhi ya jumla ni ardhi ambayo imepimwa na ni ile iliyopo maeneo ya kandokando ya mji.

Ardhi yakijiji: hii ni ardhi iliyopo vijijini katika vijiji vya Tanzania. Baadhi ya vijiji vimepima ardhi yake ila kwa ujumla vijiji vingi havijafanya upimaji wa ardhi. Ardhi ya kijiji haiwezi kutumiwa kwa minajili ya uwekezaji hadi itakapobadilishwa kuwa ardhi ya jumla kupitia kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC).

Ardhi ya Hifadhi: ardhi hii hujumuisha hifadhi ya misitu, mbuga za wanyama na sehemu za burudani kwa ajili ya jumuiya

Namna ya Kupata Ardhi

Kwa Mtanzania anayehitaji kumiliki ardhi ambayo siyo sehemu ya ardhi ya kijiji, atahitajika kutuma maombi kwenda kwa Kamishna wa Ardhi wa Wizara ya Ardhi.
Ila kwa mjasiriamali wa Kitanzania ambaye atahitaji kupata ardhi ya kijiji, atafuata hatua kama zinavyoelezewa katika sheria ya ardhi ya kijiji ya mwaka 1999. Sheria inaeleza kuwa Mtanzania mmoja mmoja au kikundi au walio katika muundo wa kikampuni wana haki ya kupata ardhi kwa matumizi mbalimbali kama matumizi ya uzalishaji au uwekezaji.

Ili kupata ardhi Tanzania, sheria inatoa uwezekano wa kutumia mwanasheria ili kumwakilisha mteja wake anayetaka kupata ardhi katika makubaliano mbalimbali ya kupata ardhi ya kuwekeza au kwa matumizi mengine. Mjasiriamali anaweza kuchagua mtu mwaminifu kwa ajili ya kufanya manunuzi kwa niaba yake. Kwa mujibu wa sheria ya ardhi ya kijiji ya mwaka 1999, kifungu cha 103 kuhusu usajili wa ardhi ni kwamba wakala aliyechaguliwa kumwakilisha mjasiriamali anaweza kusaini nyaraka za kisheria kwa niaba yake.

Hatua za kupata hati ya kimila ya kumiliki ardhi

Kwa mujibu wa sheria ya ardhi, hatua za kupata hatimiliki ya kimila ni kama zifuatazo:-

i) Peleka maombi ya hati kwa halmashauri ya serikali ya kijiji husika kwa mmiliki wa ardhi ambaye ardhi hiyo ipo chini ya umiliki wake;
ii) Halmashauri itapitia maombi ya kibali;
iii) Utolewaji wa barua ya kupewa hati inayoelezea masharti, kodi za mwaka na masharti mengine;
iv) Mmiliki wa ardhi aandike makubaliano kuhusu makubaliano yaliyofikiwa kwenye fomu uliyotolewa; na
v) Utolewaji wa hatimiliki.

Hatua za kupata kibali cha Ardhi ya Jumla

Kwa maeneo ya miji, mjasiriamali atakayehitaji kusajili ardhi aliyonunua atahitajika kulipia asilimia 4.4 ya thamani ya ardhi aliyoinunua. Hatua za usajili zinachukua wastani wa siku 73 na inapitia hatua kumi zifuatazo:

i. Fuatilia taratibu za usajili wa ardhi yako kwenye ofisi za msajili wa ardhi;
ii. Hapa muombaji atatakiwa kwenda kuchukua nyaraka kutoka wizara ya ardhi inayoainisha kuhusu masuala ya kodi kwa miaka kumi;
iii. Mwombaji itamlazimu kuchukua waraka wa ulipaji kodi wa miaka kumi kutoka manispaa/halmashauri ya mji husika;
iv. Baada ya kukamilika, mwombaji atakabidhiwa ripoti ya tathmini;
vi) Mwombaji ajipange kwa ajili ya ukaguzi wa ardhi utakaofanywa na mthaminishaji kutoka serikalini ili kujua thamani yake;
vii) Baada ya taratibu hizo hapo juu, andaa mkataba wa makubaliano wa mauziano ya ardhi na ithibitishwe kwa kugongwa muhuri na wakili;
viii) Mwombaji atapatiwa uthibitisho wa ubadilishaji wa aina ya ardhi kutoka kwa manispaa husika;
ix) Chukua cheti cha uthibisho wa thamani halisi ya ardhi; na
x) Peleka hati ya kubadilisha umiliki wa ardhi kwa Afisa wa Ardhi ili aandike kumbukumbu za jina la mmiliki mpya kwa Msajili wa Ardhi.

Aina zaArdhi Na Namna yaUmiliki

Kulingana na Sheria ya Ardhi Namba 5 ya mwaka 1999, ardhi ya Tanzania ipo katika makundi matatu yafuatayo:
• Ardhi ya Kijiji (Village Land),
• Ardhi ya Hifadhi (Reserved Land) na
• Ardhi ya Jumla (General Land).
2. Aina za miliki za ardhi
Kuna aina mbili za kumiliki ardhi zinazotambulika kisheria:
• Miliki ya kupewa na Serikali (Granted Right of Occupancy) na
• Miliki ya Kimila (Customary Right of Occupancy).
3. Makundi yaArdhi ya Jumla
• Ardhi iliyopimwa
• Ardhi isiyopimwa
Ardhi iliyopimwa ndiyo pekee inayoweza kutolewa na Kamishna wa Ardhi
4. Maombi ya Ardhi
Ardhi hutolewa na Kamati za kugawa ardhi kwenye ngazi mbalimbali kwa kuzingatia yafuatayo:-
• Kuwasilisha maombi kwa kujaza fomu na
• Maelekezo ya Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Ardhi.
4.1 Madaraka ya Waziri wa Ardhi
Mheshimiwa Waziri wa Ardhi anaweza kuelekeza kuwa ardhi fulani itolewe kwa mnada au zabuni. Kama akielekeza hivyo, Kamati itatoa tangazo lenye nia hiyo kwa muda wa siku 21. Tangazo hilo litaonesha nambari za viwanja vilivyokusudiwa na mahali viwanja vilipo na sehemu ya mnada/uuzaji.
5. Kamati za kugawa Ardhi.
Aina ya maombi yanayoshughulikiwa katika kila ngazi
5.1.Ngazi ya Halmashauri zaWilaya, Miji, Manispaa au jiji
Kamati itatoa viwanja vya aina zifuatazo ndani ya mipaka ya Wilaya:-
• Ujenzi wa Ofisi za Serikali;
• Makazi, biashara na viwanja vya huduma;
• Hoteli na viwanda;
• Ibada na huduma za jamii; na
• Mashamba yasiyozidi ekari 500 vinginevyo kwa kibali cha Mheshimiwa Waziri wa Ardhi.
5.1.2 Ngaziya Wizara/ Taifa
• Uanzishaji wa Miji mipya;
• Viwanja vya Mashirika au Taasisi za kigeni;
• Viwanja vya ufukweni na visiwa vidogo;
• Viwanja vya ujenzi wa makazi ya pamoja (housing estates) vyenye maeneo yasiyozidi hekta tano;
• Ardhi inayotolewa kwa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kwa ajili ya uwekezaji;
• Ardhi kwa matumizi yenye maslahi ya kitaifa; na
• Mashamba yanayozidi ekari 500.
6. Utaratibu wa kumilikishwa ardhi
Baada ya Kamati kukamilisha zoezi la kugawa ardhi, mambo yafuatayo yatafanyika:-
• Kamati itatoa tangazo
• Waombaji waliopewa ardhi watapewa barua za toleo (Letter of Offer)
Waliopewa ardhi watalipia ada na kodi zilizoanishwa na kurejesha stakabadhi za malipo.

Umuhimu wa Ardhi kwa Wajasiriamali

Ni muhimu kwa kila mjasiriamali kumiliki ardhi au ikishindikana kumiliki kabisa hata kukodi ardhi kwa sababu kila mjasiriamali anahitaji eneo la kufanyia shughuli zake. Mbali na hivyo, pia ardhi pia inaweza kutumika na mjasiriamali ili kukopa pesa kutoka benki tofauti tofauti na hivyo kuongeza mtaji wake wa kijasiriamali.

Kodi, ada na tozo Mbalimbali zinazohusiana na Ardhi

Kodi ya kupima mashamba ya kilimo kwa kiwanja kisicho cha biashara ni shilingi 400 kwa ekari na mashamba ya biashara ni shilingi 5,000 kwa ekari
Ada ya upimaji ardhi ni shilingi 300,000 kwa hekta
Nyaraka za ubadilishaji wa majina ni shilingi 30,000
Gharama za kupata nakala ya hukumu kwenye mabaraza ya ardhi ni Shilingi 6,000
Ada ya kuomba umiliki wa ardhi ni shilingi 20,000
Ada za maandalizi ya hati ni shilingi 50,000