Utangulizi

kabla ya kuanzisha biashara hakikisha umepata fedha za kutosha kuendeshea biashara walau kwa mwaka mmoja

Nchini Tanzania, kuanzisha biashara kuna ugumu kiasi ikilinganishwa na nchi nyingine. Mtu hawezi kupata mkopo kutoka kwenye taasisi za fedha kama hana biashara inayojiendesha angalau kwa miezi sita. Kwa hiyo, kabla ya kuanzisha biashara hakikisha umepata fedha za kutosha kuendeshea biashara walau kwa mwaka mmoja, huku ukisubiria kufanya mchakato wa kupata msaada kutoka taasisi husika.


Kabla ya kufikiria namna ya kupata fedha, mtu lazima awe na mapendekezo yaliyo dhahiri na bayana katika kueleza biashara kwa undani. Mtu anaweza kutumia mfano wa mpango wa biashara ulioambatanishwa kama njia ya kujua mambo ya msingi ya kuzingatia wakati wa kuanzisha biashara husika.

Kupata Fedha

Namna ya kupata fedha ni jambo la msingi kuliko yote katika shughuli za biashara, japo linaweza lisiwe jambo rahisi sana, kimsingi linaweza kuwa jambo gumu na la kukatisha tamaa wakati mwingine. Hata hivyo, ukiwa unafahamu na umejipanga vizuri, kupata fedha kwa ajili ya biashara yako linaweza lisiwe suala linaloambatana na maumivu makali. Zifuatazo ni baadhi ya njia za kukuwezesha kupata mtaji

 

1) Akiba ya fedha

Katika hili, mtu anaweza kuendelea kuweka akiba ya fedha ili kuwa na kiwango cha mtaji unaohitajika kuanzishia biashara husika. Baadhi ya njia za msingi zinazotumiwa na watu ni kupitia matumizi ya akaunti za benki kama vile akaunti maalumu au akaunti ya kikomo.


Karibu benki zote za biashara na baadhi ya taasisi za fedha hutoa huduma ya akaunti kikomo. Akaunti ya kikomo ni akaunti ambayo mtu anaweza kuweka pesa kwa muda bila kuitoa huku akipata riba kubwa (ikilinganisha na akaunti za kawaida) ambazo zinawezesha fedha iliyowekwa kuongozeka kama itakaa kwa muda. Benki nyingi hutoa riba katika akaunti ya kikomo kila fedha hizo zinapofikisha walau mwaka mmoja bila kutolewa.


Akaunti maalum ni akaunti ambazo hupatikana kama akaunti maalum kwa ajli ya kundi fulani la watu. Benki nyingi huwa na akaunti maalum kwa ajili ya wajasiriamali ambapo akaunti hizo huwa na makato ya chini na hutoa faida kama mikopo ya riba nafuu na riba ya juu ikilinganishwa na akaunti zingine. Mjasiriamali anaweza kutumia akaunti hizi kama njia ya kujiwekea akiba itakayomsaidia kuanzisha au kuendeleza biashara yake.

2) Ubia

Njia nyingine nzuri ya kuongeza fedha kwa ajili ya biashara ni kuanzisha ubia.

Biashara ya ubia ni pale ambapo watu wawili au zaidi wanakubaliana kufanya biashara moja. Kwa kuwa na mtu zaidi ya mmoja kwenye biashara, kunaipa biashara nafasi kubwa ya kukua kwa sababu changamoto za biashara zinapata kukabiliwa na mtu zaidi ya mmoja.

Zifuatazo ni baadhi ya sifa za Ubia katika biashara

Kukuza mtaji.

Ubia ni muhimu sana kama unataka kuanza au kukuza biashara yako ila mtaji ni kikwazo. Unaweza kuwa na wazo zuri la biashara ila huna mtaji wa kulitekeleza. Na kunaweza kuwa na mtu ambae ana fedha ila hajui afanye biashara gani. Mkikutana watu wa wili kama hivi mnaweza kutengeneza ubia mzuri sana.

Kupata mawazo ya ziada.

Hata kama unajua kiasi gani, hata kama wewe ni mjanja kiasi gani, mbili ni zaidi ya moja. Na kama mbili hii imechaguliwa vizuri basi inakuwa bora sana. Mnapokuwa kwenye biashara zaidi ya mtu mmoja, mnaweza kupeana mawazo mazuri sana ya kuboresha biashara yenu. Vichwa viwili vinapokaa pamoja kuboresha wazo, ni lazima litakuwa wazo bora sana.

Kupunguza majukumu na kuongeza ufanisi.

Wewe kama mmiliki wa biashara una majukumu mengi sana. Hata kama umeajiri watu wa kukusaidia, bado una majukumu mengi ya kuhakikisha kila kitu kwenye biashara kinakwenda sawa. Mnapokuwa zaidi ya mmoja, mnagawana majukumu haya ya biashara na hivyo kila mbia kuwa na majukumu machache na hivyo kuongeza ufanisi kwenye uendeshaji wa biashara yenu.

Kutatua matatizo.

Hakuna biashara ambayo haina matatizo, unapokuwa unaendesha biashara mwenyewe ni rahisi sana kuzidiwa na matatizo haya na usijue ni hatua gani ya kufuata. Lakini mnapokuwa zaidi ya mtu mmoja ni rahisi kufanyia kazi matatizo yoyote yanayojitokeza kwenye biashara yenu.

3) Familia na Marafiki

Kutumia wanafamilia na marafiki ni njia nzuri mbadala ya kukuza mtaji wa biashara. Hapa mtu anayependa kuanzisha biashara anaweza kutafuta msaada wa fedha kutoka kwa wote wanafamilia na marafiki ambao wanaweza kusaidia jitihada zake.

4) Udhamini wa Fedha

Wajasiriamali wanaweza kupata mikopo kwa ajili ya biashara zao kwa kutumia udhamini wa fedha. Nchini Tanzania, serikali imeunda mpango wa udhamini kwa Wajasiriamali katika taasisi za fedha ili kuwezesha ukopeshwaji wa waagiza bidhaa nje wapate huduma kubwa na nzuri kutoka katika taasisi hizo.

Katika mpango huo, taasisi za fedha zinathibitishiwa kwamba endapo mfanyabiashara atakwepa kulipa deni, mpango utalipa sehemu ya hasara. Kwa hiyo, wajasiriamali tajwa ambao ni wazawa wanaojihusisha na uagizaji bidhaa nje ya nchi wanaweza kunufaika na mpango huo wa kupata fedha ili kupanua biashara zao.

Wajasiriamali wanaostahili wanatakiwa wawe na vigezo vifuatavyo

• Biashara iwe imesajiliwa na inamilikiwa na raia wa Tanzania
• Iwe ni miradi ya kibiashara yenye faida au inayoonyesha uwezo wa kupata faida
• Kuwa tayari kutoa dhamana ya lazima pamoja na dhamana binafsi kwa matakwa ya kuruhusu dhamana ya mpango
• Awe ameomba uwezeshwaji wa mkopo kutoka katika taasisi ya fedha kuhusiana na miradi stahiki ambapo taasisi hiyo ya fedha imeomba dhamana kutoka katika mpango huo.

Vyanzo vya dhamana ya fedha kwa mikopo Tanzania
Benki Kuu ya Tanzania
Tel: +255-22-2233000-20

Benki ya Maendeleo ya Afrika (African Development Bank)
Tel: +255 (22) 2125281
+255 (22) 2125286

CRDB Bank
Tel: 022-2116714/2133067

5) Mikopo

Njia nyingine ya kupata fedha ni kupata mkopo kutoka kwa mabenki na taasisi ndogo za kifedha.

Imesemwa mara nyingi kuwa biashara ndogo hupata changamoto kukopa fedha. Sio mara zote kauli hii ina ukweli. Mabenki biashara yao kubwa ni kukopesha.

Hata hivyo, kukosa uzoefu kuhusu masoko ya fedha kwa wamiliki wengi wa biashara ndogo huweza kusababisha hali hii ya kukosa mikopo kutoka benki. Unapoomba mkopo huku ukiwa hujajiandaa vya kutosha kunapeleka kiashiria kibaya kwa mkopeshaji wako. Anapata ishara kuwa hapo kuna hatari kubwa iwapo atakukopesha.

Ili kufanikiwa kupata mkopo, ni lazima uwe umejiandaa na kujipanga. Ni lazima ujue kiasi sahihi unachohitaji, kwa nini unakihitaji, na utakirejesha namna gani. Unatakiwa kuweza kuwashawishi wakopeshaji kuwa wewe sio mkopaji atakayewatia hasara.

Ili kuweza kupata fedha kutoka kwenye taasisi ndogo za fedha na mabenki, kuna matakwa ambayo ni lazima mtu ayatekeleze. Yafuatayo ni matakwa hayo:

Lazima awe Mtanzania mwenye umri wa miaka 18 au zaidi

Lazima awe na leseni ya biashara (nakala halisi na nakala kivuli)

Lazima awe na taarifa ya fedha katika biashara yake

Lazima awe na Hati ya Kibali cha Kodi (nakala halisi na nakala kivuli)

Lazima awe na barua ya maombi ya mkopo aliyoandikiwa meneja wa tawi husika

Barua ya utambulisho wa makazi kutoka kwa kiongozi wa serikali za mitaa na barua ya mdhamini

Nakala ya utambulisho binafsi/kitambulisho cha kupiga kura/pasi ya kusafiria na utambulisho wa mdhamini

Picha za ukubwa wa pasi na mdhamini (nakala tano kwa kila mmoja) zenye usuli wa buluu

Dhamana kama ilivyoainishwa na taasisi ya fedha husika, kwa kawaida vinavyotumika ni mali isiyohamishika kama vile nyumba, shamba na vitu vingine kama gari na mali zenye thamani kama itakavyoainishwa na chanzo cha fedha

Kabla ya maombi ya mkopo, kuna masuala kadhaa ambayo lazima yazingatiwe na mwombaji. Yafuatayo yafikiriwe kabla ya kutafuta mkopo:

 1. Aina ya biashara

Kabla ya kutafuta mkopo, mtu lazima ajue aina ya biashara anayojihusisha. Hii ni muhimu kwa sababu itasaidia kusaidia tathmini ya mapato ya biashara kwa jumla na uwezekano wa kulipa mkopo.

 1. Kiasi halisi kinachohitajika

Katika hili, mtu anahitaji kujua kiasi halisi anachohitaji kuanzishia biashara. Ili kujua kiwango kinachotakiwa, mtu anahitaji kujua matakwa yote ya kuanzisha biashara husika. Kwa mfano, mahitaji yanayohitajika ni kama yafuatayo:

 1. Sehemu – nyumba/chumba ambapo mtu anahitaji kuwekeza biashara yake

 2. Vifaa/mitambo inayohitajika

 3. Kazi inayohitajika na gharama zinazoambatana nayo

 4. Gharama za usajili na leseni kwa ujumla

 5. Bima

 1. Riba iliyopangwa na mpango wa marejesho

Kujua riba inayotakiwa ni lazima kwa sababu inasaidia kuandaa marejesho ya mkopo. Kwa kujua riba inayotakiwa kulipa itasaidia kujua jumla ya fedha itakayotakiwa kulipwa na hivyo kuwezesha mpango rahisi wa marejesho.

 1. Mapato ya biashara

Haya nayo yanasaidia kuandaa mpango wa marejesho ya mkopo. Kujua mapato ya biashara kunatoa fursa ya kujua kiwango ambacho mtu anaweza kulipa kwa mpango wa wiki au kwa mwezi. Kuwa na wazo ambalo biashara yako itazalisha kutasaidia kujua kama kutakuwa na mapato/faida inayotosha kuweza kulipa mkopo au mtu atatafuta chanzo cha fedha cha ziada ili kulipa mkopo utakaochukuliwa.

 1. Dhamana inayotakiwa katika mkopo

Mwisho mtu anahitaji kujua dhamana inayotakiwa katika mkopo husika. Hii ni lazima kwa sababu kushindwa kulipa mkopo kutapelekea kuuzwa au kutaifisha/kufilisi mali iliyowekwa kama dhamana. Kulingana na hilo, mtu anahitaji kujua mali halisi zitakazohesabiwa kama dhamana pia anatakiwa kujua madhara atakayoyapata endapo dhamana hiyo itauzwa.

Zifuatazo ni changamoto zinazowakabili wajasiriamlai tajwa katika kupata mikopo:

 • Wajasiriamali hao kuwasilisha nyaraka za uongo na taarifa za uongo

 • Matumizi mabaya ya mikopo iliyotolewa

 • Uchelewaji kulipa mkopo

 • Viwango vikubwa vya riba

 • Kushindwa kutoa dhamana

 • Benki nyingi haziendeshi dirisha kuwakopesha wajasriamali tajwa

 • Mgawanyo usio sawa kwa taasisi za kifedha, yaani, nyingi ziko mijini na kando kando mwa miji

Mambo ya kufanya na yasiyofaa wakati wa kutafuta mkopo

Mambo ya kufanya wakati wa kutafuta mkopo

 • Lazima uwe na wazo la biashara

 • Mpango mzuri ulioandaliwa mahsusi kwa kuonesha jinsi mkopo utakavyotumika

 • Kuwe na mpango sahihi wa marejesho ya huo mkopo

 • Wekeza mkopo utakaopata kwa biashara iliyolengwa

 • Ongeza muda wa kulipa mkopo, kwa mfano, kama waweza lipa ndani ya miezi sita omba kulipa ndani ya miezi 12 ili kuwa katika upande salama.

Mambo yasiyofaa wakati wa kutafuta mkopo

 • Usitumie kwa matumizi yako binafsi nje ya biashara iliyodhamiriwa

 • Wekeza mkopo katika biashara tofauti na iliyokusudiwa

 • Kutokuwa na mpango wa kulipa marejesho

 • Panga kutorosha bila kulipa mkopo

 • Kutoa taarifa za uongo

Zifuatazo ni huduma zingine zinazoweza kutolewa na taasisi za kibenki na fedha:

 • Kufungua akaunti (mabenki)

 • Kuweka na kutoa fedha (mabenki)

 • Huduma ya Intaneti an Benki kwa simu (Mabenki)

 • Mafunzo (wote)

 • Nyingizeo

 • Kadi za ATM

Orodha ya mabenki Tanzania

Taasisi zinazotoa huduma za fedha

Kikokotoo cha Mkopo

Mambo ya kuzingatia kabla ya kupata mkopo mdogo

1. Tambua unachohitaji

Kama huna uhakika ni kiasi gani kampuni yako inahitaji ili kuanzisha au kupanua biashara, kutana na mshauri au mhasibu kabla ya kwenda kwa wakopeshaji. Jiandae kuwasilisha nyaraka dhidi ya maombi yako na jibu maswali kuhusu uwezo wako kifedha, aina ya biashara na mipango ya baadaye. Pia uwe tayari kuongea haswa kuhusu utakavyotumia mkopo. Kwa mfano, unaweza onesha jinsi fedha zitakavyotumika kununa vifaa, kuanzisha eneo jipya la biashara au kulipa wafanyakazi wa ziada.

2. Tafuta Mtaalamu

Kama wahitaji msaada wa kupata mkopo sahihi kwa biashara yako au mwongozo wa kukusaidia katika mchakato wa maombi waweza tafuta msaada toka vituo vidogo vya Uendelezaji Biashara mfano wa vituo hivyo ni vituo vya Biashara vya wanawake na taasisi za ushauri wa biashara ndogo vyaweza saidia katika mchakato.

3. Boresha mpango wako wa biashara

Biashara yoyote lazima iwe na mpango wake. Kabla ya kuomba mkopo kwa ajili ya biashara hakikisha Una mpango wa biashara unaojieleza kuhusu kampuni yako kwa ukweli na usahihi. Hakikisha umeandikwa kwa ufasaha kiasi cha kuwavutia wawekezaji. Kagua masuala yafuatayo:

 • Jinsi gani umeonesha kwamba unaelewa namna ya kuuza bidhaa au huduma yako na kuweza kufaidika kwa kufanya hivyo?

 • Dibaji yako ina nguvu/uwezo kiasi gani?

 • Umejiamini vipi katika tathmini ya soko na ushindani?

 

Mpango wa biashara

Mwongozo wa kutengeneza mpango wa biashara

4. Weka karatasi zako vizuri

Maombi ya viwango yanahitaji nyaraka na idadi mahsusi. Tenga muda wa kutosha kupitia na kuweka taarifa zako sawasawa kabla ya kuendelea na mchakato wa kukopa. Ni vizuri kuandaa mkutano na mshauri wa fedha ili kufanikisha azma hiyo.

Zifuatazo ni baadhi ya nyaraka utakazohitaji:

i. Nyaraka za kampuni kama vile nyaraka za kuingizwa kampuni (Article of incoporation), kufanya biashara, leseni ya biashara na kadhalika
ii. Orodha ya mali za biashara na mali binafsi inayoweza kutumika kama dhamana
iii. Majina na anwani za walau wadhamini waaminifu watatu
iv. Taarifa ya fedha kwa miaka mitatu ya fedha (kama ipo)
v. Nyaraka za marejesho ya kodi kwa miaka mitatu iliyopita

5. Jiandae kuonesha jinsi utakavyotumia fedha za mkopo

Waweza ambatanisha ripoti ya taarifa ya fedha inayoonyesha matarajio ya mzunguko wa fedha kwa miaka mitatu hadi mitano ijayo. Katika Ankara hiyo, onesha jinsi utakavyotekeleza manunuzi na jinsi unavyotarajia kulipa mkopo.

Kuwa sahihi (be specific). Onesha jinsi utakavyotumia fedha kufungua masoko mapya au matumizi ya biashara mahsusi yatakayotoa majibu chanya.

Kama unatafuta fedha kwa ajili ya mkopo, utahitaji kusisitiza namna utakavyolipa mkopo. Kwa upande mwingine, wawekezaji wa usawa (Equity investors) wanataka kuona uwezo wa nguvu ya kulipa mkopo.

Rekodi ya mapato na matumizi ya fedha

Makadirio ya mtiririko wa fedha

6. Kagua mkopo

Benki nyingi zinatumia vipimo vya mikopo (credit scoring) ili kuamua kama unahitimu kwa mkopo au la. Kwa kawaida, kwa mikopo ya kibiashara, vipimo hivyo hutumia vigezo vya historia ya ukopaji ili kuamua kama uko katika hatari au la.

Hata kama benki yako haiegemei katika njia hii, itakagua katika historia ya kumbukumbu zako ili kuamua ukopaji wako wa baadaye. Kuna uwezekano mzuri waweza ulizwa udhamini wako binafsi katika mkopo. Kwa hiyo, historia yako ya mkopo ni ya maana.

7. Weka maombi yako nadhifu

Taarifa za fedha zako zinaweza kuwa vigezo vya maana kukusaidia kupata mkopo lakini unadhifu unahesabika pia. Usisahau vitu vidogo vyaweza wapendezesha watoa fedha na kuimarisha taswira ya kitaalamu.

Weka fomu zako nadhifu na rahisi kusomeka. Vaa kinadhifu, mavazi yanayofaa katika mikutano ya kibiashara. Onesha kadri unavyoweza kuonesha uaminifu na onesha una uwezo mkubwa.

8. Uwe Mtulivu/mvumilivu

Ili kupata fedha haijalishi kiwango cha biashara yako kiasi kwamba ni mchakato mrefu unaogharimu muda na kuchosha. Wamiliki wengi wa biashara ndogo ndogo hawajali itachukua muda gani kupata fedha wanazohitaji na si ajabu kuishiwa fedha za uendeshaji biashara katika mchakato huo.

Hakikisha unazingatia muda katika majukumu yote utakayotekeleza, kuanzia kwenye urekebishaji wa mpango wa biashara hadi kutohoa orodha ya mabenki, taasisi za kukopesha fedha au wawekezaji wa nje.

KABLA YA KUAMUA KUHUSU VYANZO VYA FEDHA, JIULIZE MASWALI YAFUATAYO

 • Unahitaji nyongeza ya mtaji au unaweza kumudu kuendelea kwa kuzungusha vizuri zaidi fedha zilizopo?
 • Unaelezeaje hitaji lako? Unahitaji fedha ili kupanua biashara au kama tu kinga dhidi ya uwezekano wa kupungukiwa na fedha?
 • Hitaji lako ni la haraka kiasi gani? Unaweza kupata mkopo wenye masharti rafiki ikiwa ulijipanga mapema na kuomba mkopo kwa wakati, kuliko ukitafuta mkopo kwa haraka.
 • Biashara yako ina hatari zipi? Kila biashara ina hatari zake, na kiwango cha hatari kitaathiri gharama za vyanzo mbalimbali vya fedha na namna ya kupata fedha.
 • Biashara yako iko katika hatua gani katika ukuaji wake? Mahitaji huwa yanabana zaidi wakati biashara inahama kutoka hatua moja kwenda nyingine.
 • Fedha itatumika kwa ajili gani? Wakopeshaji wengi hutaka fedha ziombwe kwa ajili ya matumizi mahsusi.
 • Soko liko katika hali gani? liko katika hali ya kuporomoka, liko imara, au linakua? kila hatua katika soko inahitaji namna tofauti ya kutazama uhitaji wa fedha na vyanzo vya fedha. Biashara zinazofanikiwa wakati zingine zikiporomoka zitapata fedha kwa urahisi na masharti nafuu kuliko zingine..
 • Biashara yako ni ya msimu? Mahitaji ya fedha kwa biashara ya msimu mara nyingi huhitaji vyanzo vya fedha za muda mfupi.
 • Mikopo inayotolewa kwa biashara za msimu, kama biashara za ujenzi huwa imebuniwa katika namna ambayo itaisaidia biashara katika vipindi vigumu.
 • Safu yako ya uongozi ina ubora gani? Uongozi ni jambo linalotizamwa sana na vyanzo vingi vya fedha.
 • Pengine la muhimu kuliko yote, hitaji lako linaendana vipi na mpango/ mchanganuo wako wa biashara? Ikiwa huna mchanganuo wa biashara, lipe kipaumbele suala la kuandika mpango huo. Vyanzo vyote vya mitaji vitapenda kuona mpango wako wa kuanzisha au kupanua biashara.

 

BIMA KWA WAJASIRIAMALI WADOGO NA WA KATI

Bima ni mabadilishano kama fidia kati ya mmiliki wa biashara na kampuni ya bima katika kiwango maalumu kwa muhula/kipindi maalumu. Mara baada ya kusajili biashara, hasa kabla ya kuanza biashara, shurti mmiliki afikirie masuala ya bima. Kulipia bima kwa biashara yako ni kuzuia biashara yako kuingia hasara endapo tatizo lolote lisilotarajiwa kama vile moto, wizi au majanga ya asili yatatokea. Biashara inapokatiwa bima, wakala wa bima atafidia hasara itakayotokea.

1. Faida

 • Usalama dhidi ya matukio yasiyotarajiwa kama vile wizi na moto

Mfanyabiashara anaweza lipia bima biashara yake ili asidhurike na madhara kama vile wizi na moto. Kwa maana hiyo, mhusika hupata fidia yote baada ya kutokea tukio.

 • Njia rahisi za fidia ya hasara endapo bahati mbaya yaweza kutokea

Mtu anaweza lipia bima ya biashara yake ili asidhurike hasara ikitokea. Kama biashara imelipiwa bima, baadhi ya hasara zaweza kulipwa/kufidiwa na hivyo kuwezesha uwepo wa biashara.

 • Bima yatoa fursa katika huduma bila kulipia fedha halisi kwa wakati husika, kwa mfano, bima ya afya

Hii ni kwa ajili ya aina zingine za bima kama vile bima ya afya. Mtu hupata fursa kamili kwa ajili ya huduma za afya bila kulipa hata senti. Hapa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wanaweza kuwa na uhakika wa usalama kwa afya za familia zao wanapougua.

 • Huruhusu ukuaji wa biashara kwa urahisi bila kudhurika na changamoto

Katika hili, biashara inaweza kushamiri bila kuwa na wasi wasi kuhusu changamoto zisizotarajiwa zikitokea wakati biashara imelipiwa bima

2. Mambo ya kuzingatia wakati wa mahitaji ya bima kwa ajli ya biashara

 1. Aina ya bima ambazo mtu anaweza kujiunga

Kuna aina nyingi za bima, kwa mfano, bima ya moto, bima ya wizi na bima ya magari. Si budi mtu akajua mpango mahsusi kwa kujiunga na bima

 1. Uhalisi wa kampuni ya bima

Katika maeneo mengi, kuna mawakala wa bima bandia. Kwa hiyo, kabla mtu hajalipia huduma ya bima, si budi awe na ufahamu wa uhalisi wa kampuni ya bima. Mambo/masula ya mtu kuzingatia ni kukagua katika maeneno/masula yafuatayo:

 1. Nyaraka zilizothibitishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wakala wa Usajili wa Leseni(BRELA)

 2. Ofisi na maeneo halisi ya kampuni

 3. Nakala za risiti (hata hivyo, hizi zisiwe uthibitisho pekee kwani wakati mwingine zinaweza kuwa za kughushi)

 4. Orodha ya makampuni nchini au orodha ya makampuni ya biashara nchini ili kuhakikisha kama kampuni inatambulika kisheria

 1. Kulinganisha makampuni kadhaa ya bima ili kubaini kampuni inayotoa huduma zinazofaa katika gharma ambazo waweza kuzimudu

Kutokana na kuwepo makampuni mengi yanayotia huduma za bima kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati, kabla ya kujiunga na mpango wa kampuni yo yote ya bima, mtu anapaswa kukagua gharama kwa kulinganisha na makampuni kadhaa ili kupata huduma itakayofaa

 1. Hakikisha kuwa una nyaraka muhumi

Kimsingi, nyaraka muhimu hutegemea namna ya mali/huduma ya bima mtu atakayojiunga nayo, kwa mfano,

 1. Nyaraka za usajili na leseni

 2. Hati ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN)

 3. Nyaraka halisi/zilizothibitishwa zinazoonesha umiliki na thamani ya mali/biashara

Angalizo: Nyaraka zinazotakiwa hutofautiana kutegemea na makampuni (Tafadhali angalia orodha ya makampuni iliyoambatanishwa)

 1. Lipia bima kwa vitu muhimu sana katika biashara

Ingawa si wazo jema kuacha kusajili baadhi ya vitu/mali, lakini mara nyingi mtu aanze kusajili vitu/mali muhimu zaidi katika biashara. Kwa mfano, kwa biashara ya vyakula, vitu vya kwanza kulipia bima ni jiko.

 1. Lipia bima dhidi ya majanga yanayoweza kutokea

Japokuwa si rahisi kutabiri kutokea kwa janga, lakini kutegmea na aina ya biashara na eneo biashara itakapofanyika, kuna majanga muhimu ambayo mtu anatakiwa kuambatana nayo. Kwa mfano katika biashara ya hoteli, moto, wizi na mali ni vitu vya lazima kujiunga katika mipango yake wakati mipango ya biashara ya usafirishaji inaweza kuhuisha mali, ajali na wizi.

3. Aina za bima kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati

 1. Wizi

Aina hii ya bima inaweza kuhusisha madhara dhidi ya kutokea kwa wizi wa mali za biashara

 1. Moto

Hii mtu anaweza kulipia bima ya nyumba na vifaa vyake dhidi ya moto

 1. Majanga ya asili

Hii inahusu kulipia biashara kutokana na madhara yanayotokana na majanga ya asili kama vile mafuriko dhidi ya biashara

 1. Mpango wa Bima ya Afya/Matibabu

Aina hii ya bima inaweza kuwa katika aina mbili zifuatazo:

 1. Aina ya kwanza ya bima ya afya ni kutoa huduma ya afya kwa watu. Katika aina hii ya bima, watu wanaweza kupata huduma za afya baada ya kujiunga na mpango wa bima ya afya.

 2. Aina ya pili ya bima ya afya ni kulipia madhara ya aina zote yanayoweza kutokana na ajali au kifo wakati wa kazi au katika mazingira ya kazi

 1. Bima ya mali

Katika aina hii ya bima mtu alipie bima ya mali. Kuna aina nyingi zinazoweza kulipiwa bima kama zifuatazo:

 • Mizigo ya bandari: Sera hii inahusisha kinga dhidi ya upotevu wa mizigo wakati inasafirishwa baharini (kwa meli), angani (kwa ndege) au ardhini (kwa barabara au reli).

 • Magari:Sheria inataka magari yote katika barabara za umma kuwa na bima au kinga dhidi ya dhima kwa kuumia kwa mwili na kwa abiria.

ANGALIZO: Biashara yo yote inayoendeshwa nchini kisheria yaweza lipiwa bima

4. Orodha ya Sheria Zinazoongoza Huduma za Bima

 1. Sheria ya Bima ya mwaka 2009

Sheria iliyoanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Bima Nchini (Tanzania Insurance Regulatory Authority). Chini ya Sheria hii, mamlaka imepewa nguvu ya kuongoza na kusimamia biashara ya bima na masuala yote yanayohusiana na bima Tanzania Bara na Zanzibar.Sheria inaipa mamlaka nguvu ya kusimamia na kuratibu shughuli zote za bima. Sheria inaainisha kanuni za maadili kwa ajili ya bima na taarifa zote muhimu za kuendesha biashara ya bima wakati ambapo mamlaka ya usajili wa biashara za bima amepewa Kamishna wa Bima au Naibu Kamishna wa Bima. Sheria inaelekeza kwamba yeyote atakayeanzisha biashara ya bimalazima awe mkazi wa Tanzania lakini kama ni kundi angalau theluthi moja ya wajumbe wa bodi wawe ni wakazi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sheria inaelekeza taratibu na nyaraka muhimu za kuanzisha biashara ya bima. Pia sheria inaelekeza haki ya bima ya tatu kama vile kuwa na bima dhidi ya dhima kama kufilisika pamoja na haki ya kupata taarifa kwa mwendesha biashara ya bima.

 1. Kanuni za Bima Ndogo za 2003

Kanuni hizi zinahusu wakala wa bima ndogo na mwekeza bima anayehusika na bima kwa ujumla kuhusu bima ndogo au bima ndogo ya maisha. Huduma chini ya kanuni hizi zinahusu banda, mifugo, vifaa vya uvuvi, mazao ya kilimo, zana za biashara ndogo au vifaa au ajali ya mtu binafsi au kundi, elimu, muda wa mkopo, maisha ya familia na bima ya mkataba wa mazishi.

Kutunza Kumbukumbuku za Fedha

Utunzaji wa kumbukumbu za kifedha ni muhimu sana katika ustawi wa biashara yoyote. Utunzaji wa kumbukumbu ni kipengele muhimu katika kumuwezesha mjasiriamali kujua mapato na matumizi ya biashara.

Kujua mapato na matumizi ya fedha zinazopatikana kutokana na biashara zako husaidia kwa kiasi kikubwa kufanya maamuzi bora ya biashara kuhusu vyanzo vya mapato, kodi, matumizi binafsi ya mmiliki wa biashara na hata kustaafu katika biashara.

Katika biashara yoyote, kumbukumbu bora za kifedha ni msingi wa umakini katika utunzaji na udhibiti wa fedha.

Umuhimu wa kumbukumbu

Taarifa: Kila biashara inahitaji kutunza kumbukumbu za miamala yake ya kifedha ili waweze kupata taarifa kuhusu hali yao kifedha, ikiwa ni pamoja na:

Taarifa fupi ya mapato na matumizi na mgawanyiko wake katika vipengele mbalimbali.

Matokeo ya shughuli za biashara – ziada (faida) au upungufu (hasara).

Mali na madeni – au vitu vinavyomilikiwa na biashara na vile ambavyo biashara inadaiwa.

Imani/ uaminifu: Kutunza kumbukumbu sahihi za kifedha kunachochea uadilifu, uwajibikaji na uwazi. Pia kunasaidia kuondoa hisia za kukosa uaminifu baina ya mwajiri na waajiriwa. Pale ambapo unakuwa huna kumbukumbu sahihi za fedha unaweza ukadhani unaibiwa na wafanyakazi wako, kwa hiyo kumbukumbu zitakusaidia kujiepusha na hisia mbaya.

Pia kuwa na kumbukumbu sahihi za kifedha kutasaidia taasisi za kifedha kukuamini na kukupatia mikopo kwa urahisi. wakopeshaji wengi hupenda kujua maendeleo ya biashara yako kabla

Matakwa ya kisheria: Kutunza kumbukumbu za kifedha kutakusaidia sana kukidhi baadhi ya matakwa ya kisheria. Mfano mzuri ni kuwa utunzaji sahihi wa kumbukumbu utakusaidia kufanyiwa makadirio sahihi ya kodi. Wajasiriamali wengi wamejikuta wakikadiriwa kodi kubwa kwa sababu tu hawana kumbukumbu sahihi za mapato na matumizi ya biashara zao.

Mipango ya baadaye: Pamoja na kuwa taarifa za kifedha zinaripoti mambo yaliyokwishatendeka, zinasaidia utawala kuweka mipango ya mbeleni na kuelewa zaidi kuhusu uendeshaji wa biashara. Ukiwa na taarifa za miaka miwili mitatu ni rahisi kupata taswira ya mwenendo wa biashara.

Namna za kutunza kumbukumbu za kifedha

Ili uweze kutunza vyema kumbukumbu za fedha unatakiwa kuchagua mbinu sahihi za kuhifadhi taarifa zako za kifedha. Kuwa na mbinu sahihi kutasaidia kuonesha namna ulivyotumia fedha, pamoja na vyanzo vya fedha hizo. Kumbukumbu za kifedha zinaweza kutunzwa katika mfumo wa kuandika kwa mikono katika vitabu vya fedha, au kutumia mfumo wa kompyuta ambao unaweza kutumia mojawapo ya programu za kihasibu za kompyuta.

Kuna njia kuu mbili za utunzaji wa kumbukumbu za fedha ambazo ni:

 • Kurekodi kwa kuzingatia miamala ya fedha taslimu tu
 • Kurekodi kwa kuzingatia msingi wa muamala, hata ikiwa ni deni

Namna hizi mbili zinatofautiana kwa vitu mbalimbali, kubwa ikiwa ni tofauti ya ni wakati gani muamala unarekodiwa kuenye vitabu vya fedha.

Miamala inayohusisha fedha taslimu haina kuchelewa, maana biashara na malipo ya fedha vinafanyika kwa wakati mmoja.

Miamala inayohusisha kukopa huwa na muda kati ya kutolewa kwa huduma/ bidhaa na malipo kufanyika.

Mfumo wa kurekodi fedha taslimu tu

Hii ni namna rahisi sana ya kutunza kumbukumbu za kifedha na haihitaji ujuzi wa juu katika utunzaji wa mahesabu. Sifa zake ni:

 1. i) Malipo yanaandikwa kwenye jedwali la fedha taslimu mara yanapofanyika, kadhalika makusanyo pia yanaandikwa katika jedwali hilo mara yanapotokea.
 2. ii) Mfumo huu haujishughulishi na pesa zilizolipwa zamani, au kiasi cha malipo ambayo bado yanadaiwa.

iii) mfumo huu hauweki moja kwa moja kumbukumbu za madeni au mali za biashara

 1. iv) Mfumo huu hautunzi kumbukumbu za miamala isiyohusisha fedha taslimu moja kwa moja, mfano Uchakavu/ kutumika kwa vifaa/ mitambo. .

Mfumo wa kutambua madeni katika kuweka kumbukumbu

Huu ni mfumo rasmi wa kihasibu unaoweka kumbukumbu kwa kutambua na kuandika pande mbili za kila muamala unaofanyika, ambazo zinahusisha kutoa na kupokea.

Pande mbili za jedwali hutumika, yaani upande wa kushoto na upande wa kulia. Mfumo huu ni wa kisasa na unahitaji ujuzi wa kanuni za kihasibu.

Matumizi/ gharama huandikwa kwenye kitabu kikuu cha mahesabu pale biashara inapoingia gharama hizo, na sio kusubiria hadi zitakapolipwa. Hali kadhalika, mapato hutambulika na kuingizwa kwenye vitabu pale biashara inapoyapata, na sio kusubiria hadi fedha hizo zikusanywe.

 • Mfumi huu unajishughulisha na aina zote za miamala.
 • Mfumo huu hupelekea kuwa na taarifa sahihi ya mali na madeni ya biashara.

Kumbukumbu katika mfumo huu huwa na jedwali la mapato na matumizi, ambalo hujumuisha mapato na matumizi yote yaliyofanyika kwa kipindi fulani, pamoja na taarifa ya hali ya kifedha ambayo huonesha, licha ya mambo mengine, madeni inayodai na kudaiwa biashara katika siku ya mwisho ya kipindi hicho.

Mifano ya nyaraka muhimu zinazotunzwa ni:

 • Jedwali la fedha taslimu/ zilizoko benki
 • Vocha (Makusanyo, Malipo na kitabu cha kumbukumbu)
 • Rajisi ya malipo ya awali
 • Taarifa ya benki/ uoanisho wa taarifa ya benki na taarifa ya fedha taslimu

Jedwali la fedha taslimu

Hili ni jedwali linalotunza taarifa za miamala ya kifedha (malipo na makusanyo) yanayotokea katika biashara. Katika jedwali hili, makusanyo na malipo yanayofanyika na biashara huandikwa.

Jedwali hili hutumika kurekodi, kuainisha na kutoa muhtasari wa miamala ya fedha taslimu katika namna ambayo itamuwezesha yeyote anayehitaji taarifa za yaliyomo katika jedwali hilo kufanya maamuzi yenye kuzingatia taarifa. Jedwali hili likitunzwa vema, mtu anayelisoma atapata taarifa kuhusu salio la fedha taslimu lililokuwepo mwanzo wa kipindi, kiasi gani cha fedha taslimu kimeingia (makusanyo), kiasi gani cha fedha taslimu kimetoka (malipo) na salio la fedha taslimu mwishoni mwa kipindi husika.

Itaendelea…..

Imeandaliwa na Veneranda Sumila