Mbinu muhimu za kukabiliana na ushindani katika soko

foodprocessing

Ili bidhaa iweze kupata wateja sokoni kirahisi inategemea zaidi kiwango chake ikilinginishwa na bidhaa za washindani au kukidhi mahitaji ya wateja.

Soko ni hitaji muhimu katika uanzishaji na ukuaji wa biashara yoyote japo watu wengi wanatokea kuchukulia jambo hili kama la kawaida. Kwa maana rahisi zaidi, utafiti wa masoko ni kila kitu unachoweza kukifanya kutaka kujua wateja wako ni akina nani, na wanahitaji na kutaka nini.

Hii ndio mbinu pekee inayokusaidia kukabiliana na ushindani kwa kuwaridhisha wateja wako huku biashara yako ikikua. Pamoja na kuwapa wateja huduma au bidhaa wanazozihitaji, pia unaweza kupanga bei ambayo wataimudu, kuwafikishia huduma au bidhaa kwa urahisi na kuwavutia wateja wanunue.

Utafutaji wa soko ni muhimu hata kama bidhaa yako ina uzuri kiasi gani. Ni zoezi lisilo na kikomo kwani huanzia katika wazo la biashara hadi siku za uhai wa bishara yako. Kama mjasiriamali unayetaka kufanikiwa zaidi, hili ni jambo muhimu sana kwa maendeleo mazuri ya bishara yako.

Taarifa muhimu unazoweza kuzipata kwa wateja ni zile zitokanazo na maswali juu ya bidhaa au huduma, mathalani wanazionaje bidhaa zako au huduma, nini wanapenda kutumia zaidi, wanawaonaje washindani wako, kujua ubora na ubunifu wa bidhaa za washindani wako sambamba na bei wanazotoza ili uweze kubuni zaidi na kutoza gharama inayoendana na bidhaa au hudumu kwa kuangalia hali halisi ya soko.

Hivyo kama mjasiriamali ni lazima uwe na taarifa za kutosha juu ya bidhaaa yako ili kuweza kukidhi matakwa ya wateja wako.

Ili kufanya zoezi hili liwe na tija kwenye biashara yako, kuna mambo muhimu ya kuzingatia.

Bidhaa

Upatikanaji wa masoko unategemea aina ya bidhaa na aina ya wateja walengwa. Lazima kuwepo na uuwiano wa moja kwa moja. Mfano hauwezi kutengeneza ice cream sehemu yenye baridi kali maana hii haina utofauti na kuuza vocha za muda wa maongezi katika jamii isiyo na simu. Hivyo ni muhimu sana kujifunza ni aina gani ya bidhaa sambamba na wateja wako na mazingira kwa ujumla.

Bei

Kwa mjasiriliamali, kupatikana kwa mteja na faida yako kunategemea bei utakayoipanga. uzingatie ubora, gharama za uzalishaji ili kupata bei halisi sambamba na kuona sokoni washindani wako wanawatoza wateja wao kiasigani. Unapoangalia gharama kumbuka kuna gharama za moja kwa moja na gharama zisizodhahiri mfano pango, ulinzi, uchakavu wa vifaa na bima.

Ubora

Ili bidhaa iweze kupata wateja sokoni kirahisi inategemea zaidi kiwango chake ikilinginishwa na bidhaa za washindani au kukidhi mahitaji ya wateja. Bidhaa bora inajitangaza kwa kiasi kikubwa kwani wateja wenyewe wanakuwa sehemu ya matangazo kwa kuipa sifa kwa watumiaji wengine na kurahisisha uuzikaji wa bidhaa husika.

 

Ufungashaji na Matangazo

Ufungashaji wa bidhaa unaleta muonekano wa ubora wa bidhaa. Muonekano mzuri unamvutia mteja kununua bidhaa yako na unaiwezesha bidhaa yako kudumu. Kumbuka pia kifungashio ni njia mojawapo muhimu inayoitangaza bishara yako. Wewe mwenyewe kama mteja, hebu jiulize ni kwa kiasi gani huwa unavutiwa na namna bidhaa fulani kama vile vyakula, vinywaji, nguo, nk. Hapo unaweza kupata jibu kuhusu umuhimu wa ufungashaji.


Hivyo masoko ni sehemu muhimu ya kuifanya biashara ikue au ife. Utumiaji wa mbinu sahihi za kuwafikia wateja ndio unaweza kumfanikisha mjasiriamali kwani faida hutokana na ukubwa wa mauzo ambao unaendana na kukua kwa uzalishaji/huduma na baadae kukua kwa biashara husika kwani soko ni moyo wa biashara. Kukua kwa soko ndio kukua kwa biashara na kukosekana kwake ndio kuanguka kwa biashara.
Kwa taarifa zaidi