Vidokezo vya Kuboresha Huduma kwa Wateja

  1. Husisha wateja wako kila fursa inapopatikana.

Mawasiliano ni muhimu sana kwa sababu wateja wako wanapenda kujisikia wamethaminiwa na wamehesimiwa. Wangependa pia kupata amani kuwa wanaweza kuamini kuwa utatimiza ahadi kwao.

Kufuatilia soko na kufahamu mapema kuhusu mabadiliko katika mahitaji ya wateja kutakuwezesha kufikiri kwa ubunifu na kuwatangulia washindani wako. Hili litafanyika kwa:

  • Kuwasiliana mara kwa mara na wateja wako ili kuelewa mabadiliko katika mahitaji yao.
  • Kupata mrejesho mara kwa mara kutoka kwa wateja kwa kupitia fomu/ dodoso maalum kwao, ambapo unapata nafasi ya kutathmini biashara yako kwa maoni ya watu muhimu katika biashara yako.
  • Kufuatilia yanayojiri katika uchumi na kuchambua namna mabadiliko yanavyoweza kuathiri wateja wako.
  • Kufuatilia washindani wako ili kuelewa uko nafasi gani katika soko na namna gani utajitofautisha.
  1. Wape wateja urahisi, ili wapate kitu kile kile wanachohitaji

Haina maana kuwasikiliza wateja ikiwa huna mpango wa kuwapa wanachotaka. Sio mara zote mahitaji na matakwa ya wateja yatakuwa yanafanana, hasa katika hali ngumu za kiuchumi. Inabidi kuhakikisha unatoa huduma kwa ajili ya viwango tofauti tofauti vya bajeti za wateja. Weka mifumo ya wafanyakazi wako kufanya kazi kwa kutimiza hili.

  1. Ajiri watu sahihi

Ubora wako unaweza kupimwa kwa kulinganishwa na ubora wa mfanyakazi mdhaifu kuliko wote katika biashara yako. Hivyo unahitaji kuwa mwangalifu katika kuajiri. Haijalishi safu ya uongozi imeahidi nini, utekelezaji unategemea sana uwezo wa kiutendaji wa watendaji wa ngazi za chini. Kuhusu ubora wa wafanyakazi, usilenge tu kutizama sifa na ujuzi wa mwajiriwa, bali pia tengeneza mpango unaojitosheleza wa mafunzo. Ajiri watu kwa ajili ya mitizamo yao, ambayo ni vigumu sana kubadilishwa kwa kutumia mafunzo. Watu walio mtizamo sahihi ni wepesi pia kujifunza.

  1. Endeleza wafanyakazi wako

Hata kama wafanyakazi watajiunga au kuajiriwa wakiwa na mtizamo sahihi unaoendana na falsafa yako ya biashara, inawezekana baadaye wakabadilika ikiwa hautawahusisha ipasavyo katika kufanya maamuzi na kuwapa nafasi ya kukua/ kuendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *