Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina ataja Fursa zilizopo katika sekta anayoiongoza

Tanzania imebarikiwa kuwa nchi ya amani na utulivu ikilinganishwa na nchi zingine za Afrika Mashariki. Nchi hii pia imebarikiwa rasirimali nyingi sana ikiwemo madini, ardhi yenye rutuba, hifadhi mbali mbali za wanyama, ma

ziwa, bahari na vingine vingi.

Pamoja na kuwa rasirimali hizo zinachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa Tanzania, lakini kwa kiasi kikubwa bado kuna fursa nyingi sana ambazo watanzania hawajazitumia ipasavyo katika kuwaletea kipato.

Wiki hii Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imepata bahati kubwa ya kutembelewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Luhaga Mpina na kutueleza mambo mengi ikiwemo fursa za uwekezaji zilizopo katika wizara na sekta anayoiongoza.

Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kwa kuwa na mifugo mingi baada ya Ethiopia, Takwimu kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi zinaonyesha kuwa kwa sasa Tanzania ina Ng’ombe takribani millioni 30, Mbuzi millioni 18.8, Kondoo millioni 5.3, Nguruwe millioni 1.9 na kuku millioni 38.8.

Pamoja na kuwa na ng’ombe wengi sana, Tanzania inazalisha lita bilioni 2.4 za maziwa kila mwaka ikilinganishwa na Kenya ambayo inazalisha lita billioni 5.2. Hii inaonyesha kuwa ufugaji tunaoufanya Tanzania sio wa kibiashara ikilinganishwa na wenzetu Kenya. Kwa Mujibu wa Waziri Mpina, Kenya ina Ng’ombe wa maziwa wapatao millioni 4.2 ikiinganishwa na Tanzania ambayo ina Ng’ombe wa maziwa wapatao 780,000.

Hata hivyo pamoja na kuzalisha maziwa lita billioni 2.4 bado viwanda vyetu vya maziwa vinatumia na kuchakata asilimia mbili tu ya maziwa yazalishwayo nchini hivyo kuwaacha wakulima na hali ngumu ya kukosa soko la uhakika la maziwa yao. Badala yake Tanzania inaagiza kwa wastani wa lita millioni 13 za maziwa kutoka nje ya nchi yenye thamani ya zaidi ya Sh billioni 50.

Sababu hii ni mojawapo ya sababu zilizomnyanyua waziri Mpina kutoka wizarani kwake – na kumfanya kuwa Waziri wa kwanza nchini Tanzania kuomba kutembelea TPSF yeye mwenyewe bila kuombwa –  kuja TPSF kutafuta sababu zinazopelekea Watanzania na wawekezaji kwa ujumla washindwe kuwekeza katika sekta hiyo.

“Ndugu Simbeye, serikali imekuwa ikijitahidi kufanyia kazi changamoto mnazozileta kwetu zinazokwamisha uwekezaji, lakini pamoja na maboresho tunayoyafanya bado hatuoni uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye ufugaji. Nimeamua kuja kusikiliza mwenyewe maana huenda kuna changamoto nyingine ambazo zimejificha na serikali haizijui. Natamani nione biashara na viwanda vikishamiri katika sekta ninayoiongoza,” alisema Mheshimiwa Mpina.

Mkurugenzi wa TPSF Godfrey Simbeye naye anaeleza kuwa ujio wa Waziri Mpina ni hatua kubwa sana inayoonyesha jinsi serikali ilivyotayari kuisikiliza sekta binafsi na ilivyotayari kufanya kazi na Sekta Binafsi nchini.

“Mheshimiwa Waziri, nashukuru sana kwa ujio wako hapa TPSF, wewe ni Waziri wa kwanza kuja kututembelea bila sisi kukuomba, tunachangamoto nyingi sana zinazotukabili na kutufanya tushindwe kuwekeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika sekta ya mifugo na uvuvi. Lakini tunaomba tukuandikie matatizo na changamoto tulizonazo baada ya kuwasiliana na wanachama wetu walio kwenye sekta hii, tutakuandikia na kukutumia rasmi changamoto zetu lakini pia mapendekezo ya namna bora ya kutatua changamoto hizo,” anaeleza Bwana Simbeye.

Wizara ya kilimo na Uvuvi ni wizara pekee ambayo hadi sasa imetekeleza agizo la muheshimiwa Rais John Magufuli la kuhakikisha kila wizara inaanzisha dawati maalumu la kusikiliza, kutatua na kuwasaidia Wawekezaji kutatua changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo (Private Sector Facilitation Desk).

Kwa mujibu wa Muheshimiwa Waziri Mpina pamoja na kuwa Tanzania ina Ng’ombe wengi bado inaagiza nyama kutoka nje ya nchi na kuwa viwanda vya nyama vilivyopo havizalishi kama inavyotakiwa. Tanzania inaagiza tani 2000 za nyama kila mwaka na wakati huo huo inauza nje tani 2000 za nyama.

“Utaona kuwa kiasi cha nyama tunachouza nje kwa bei rahisi kabisa, ndio kiasi hicho hicho tunachoagiza kutoka nje kwa bei ya juu, natamani kuona wawekezaji wengi wakiwekeza katika sekta hii kwa sababu fursa zilizopo ni kubwa.”

Hadi sasa Tanzania haina kuwanda kikubwa cha kutengeneza ngozi pamoja na kuwa serikali ilitekeleza ombi la ssekta binafsi la kuweka masharti magumu ya ngozi ghafi inayouzwa nje ya nchi.

“Mlileta maombi ya kuzuia uuzaji wa ngozi ghafi nje ya nchi na serikali iliweka ushuru wa asilimia 80 kwa anayetaka kuuza ngozi nje ya nchi ikiwa ghafi, jitihada zote hizi zililenga kuhakikisha kuwa viwanda vya ndani vinapata ngozi ya uhakika na kwa bei nzuri. Matokeo yake wakulima wamebaki kuozewa na ngozi zao kwa kukosa soko kwa sababu viwanda vya ndani havinunui ngozi zao, naomba mniambie tufanye nini kama serikali ili nyinyi sekta binafsi muweze kuwekeza,” anasema Mpina.

Kwa upande wa Uvuvi, mheshimiwa Mpina anaeleza kuwa uwekezaji katika sekta hii bado umedorola sana licha ya kuwepo na fursa kubwa za kuleta maendeleo. Kuwepo kwa Samaki aina ya Sangara ni mojawapo ya fursa muhimu sana zilizopo nchini kwani Sangara wanatoa zao la Bondo ambalo linauzwa kwa bei kubwa sana.

Katika soko la ndani zao la Bondo linauzwa kwa Sh.80,000 kwa kilo wakati kilo kama hiyo inauzwa kwa zaidi ya shilingi millioni moja katika masoko ya kimataifa. Tanzania mwaka jana iliuza liko 700,000 za Bondo zenye thamani ya shilingi billioni 90. Samaki aina ya Tuna pia walitajwa kuwa miongoni mwa mazao yenye bei kubwa sana ambapo kilo moja ya samaki hawa inauzwa kati ya shilingi 80,000 hadi 100,000 katika masoko ya kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *